Bukobawadau

TZ SAKATA LA NESI FEKI KUKAMATWA

Hatari sana! Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Joyce Jonas, mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 45 na 50, mkazi wa Tabata, Dar, ametiwa mbaroni kwa madai ya kughushi vyeti vya unesi kisha kufanya kazi ya uuguzi katika hospitali mbalimbali, akijishughulisha na upasuaji bila kuwa na utaalamu wa taaluma hiyo.

Tukio hilo lililovuta hisia za wengi, lilijiri hivi karibuni maeneo ya Mwenge, Dar ambapo mtuhumiwa huyo alidakwa katika moja ya hospitali (jina tunalo) na mwenye vyeti ambaye kitaaluma ni nesi kisha kufikishwa kituo kidogo cha Polisi cha Mwenge, Dar.
ILIKUWAJE?
Habari zilidai kuwa Joyce ni binamu wa mmiliki halali wa vyeti vya unesi aliyetajwa kwa jina la Mary Bora.
Ilisemekana kwamba miezi kadhaa iliyopita, Joyce alifika nyumbani kwa nesi huyo na kufanikiwa kuiba vyeti hivyo.
Kitambulisho feki chanye jina la Mary Peter Bura.
Habari zinadai kwamba lengo la mtuhumiwa kuiba vyeti hivyo ni kuvitumia kwa ajili ya kazi aliyokuwa nayo awali ya kuuza duka la dawa baridi za binadamu lililokuwa Mnazi-Mmoja, Dar.
Ilidaiwa kwamba Joyce alipata ushawishi kutoka kwa baadhi ya watu wake wa karibu wakimtaka kutumia vyeti hivyo, kutafuta kazi ya unesi kwani viliruhusu kutokana na kuwa na viwango vya juu.
Ilisemekana kwamba Joyce alidurufu vyeti hivyo kwa kutumia jina halisi la nesi huyo huku akibandika picha yake na kuvirudisha vyeti halisi nyumbani kwa Mary bila mwenyewe kujua.
Ilisemekana kuwa Joyce alifanikiwa kupata kazi kwenye hospitali mbili, moja Kariakoo na nyingine Mwenge (majina tunayo) na kuanza kujiingizia ‘mpunga’ wa maana huku akijuhusisha na upasuaji, zoezi ambalo alikuwa akilifanya kwa kutumia uzoefu tu, kutokana na kujua kushona majeraha madogo.
Habari zilidai kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutumia vyeti hivyo kwa muda mrefu, hatimaye taarifa zilimfikia nesi halisi kuwa jina lake linatumiwa na nesi mmoja kwenye hospitali tofauti.
Ilisemekana kuwa baada ya taarifa hizo kumfikia Mary (mwenye vyeti halisi), alifanya uchunguzi kujua ni nesi gani anatumia jina lake katika hospitali hizo, ilihali yeye si mwajiriwa wa hospitali tajwa.
Ilielezwa kuwa Mary aliunda mkakati kabambe wa kumtia Joyce mbaroni ambapo alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Mwenge kisha akapewa askari alioambatana nao.
Mary, akiambatana na vijana wa IGP Mangu walifanikiwa kumtia nguvuni Joyce akiwa kazini ndani ya hospitali moja maarufu iliyopo Mwenge.
Baada ya kumkamata, Joyce hakuwa na la kujitetea zaidi ya kukiri kuwa ni kweli alifanya ‘uhuni’ huo huku akijitetea kuwa ni ugumu wa maisha ndiyo ulisababisha.
Wakiwa kwenye ujenzi wa taifa, makachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) walipokea taarifa za kuwepo kwa kesi hiyo kituoni hapo ambapo walitinga hapo na kumkuta Joyce akiwa chini ya ulinzi.
Kutokana na uzito wake, madai ya kesi hiyo yalihamishiwa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar.
Wakiwa njiani kuelekea kituoni hapo, Joyce aliwaomba makachero wetu wasifanye chochote, ikiwemo kuandika habari hiyo.
“Jamani,nawaombeni msinipige picha, wala msiandike habari hii, haya ni maisha tu,” alilalamika Joyce.
Baada ya kufikishwa kituoni hapo, Joyce alifunguliwa jalada la mashitaka lenye namba KJN/RB/1883/2014-KUGUSHI na kutupwa rumande kupisha uchunguzi zaidi juu ya madai hayo kisha atafikishwa kortini.

Credit: GPL
Next Post Previous Post
Bukobawadau