Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI- UTEUZI WA KAIMU MUFTI MKUU



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTEUZI WA KAIMU MUFTI MKUU WA WAISLAM TANZANIA
Muda mfupi baada ya aliyekuwa mmoja wa Wajumbe wa Baraza Kuu la Ulamaa la BAKWATA Sheikh Abubakar Zuberi, kuteuliwa kukaimu nafasi ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), DK. Willibroad Slaa amemtembelea nyumbani kwake kumpongeza na kumtakia majukumu mema akimhakikishia ushirikiano kama jirani na kiongozi.
Sheikh Abubakar Zuber ambaye ametangazwa leo kukaimu nafasi hiyo ya juu katika uongozi wa dini ya Kiislam kwa siku 90 hadi hapo atakapochaguliwa Mufti Mkuu kwa mujibu wa taratibu za dini hiyo, anaishi Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, jirani na zilipo Ofisi za Makao Makuu ya CHADEMA.
Mbali ya kumtakia kila la heri, Katibu Mkuu Dk. Slaa amemuahidi Mufti Sheikh Zuberi kuwa CHADEMA iko tayari wakati wowote kutoa ushirikiano atakaouhitaji katika kutimiza wajibu wake huo.
“Shehe Zubeir, jirani yangu napenda kutumia fursa hii kukupongeza sana kwa namna ambavyo wenzako wamekupatia imani kubwa na kukuteua ili uwaongoze Waislam kiroho. Ni imani kubwa ambayo binafsi naamini utaweza kuitumikia wakati mkiendelea kusubiri taratibu zingine za uchaguzi.
“Nitumie fursa hii pia kusema tukiwa majirani zako hapa Mtaa wa Ufipa, tukiwa viongozi ambao tunao wanachama, wapenzi na wafuasi wetu wenye dini tofauti wakiwemo Waislam, naomba kukuhakikishia ushirikiano kutoka kwetu wakati wowote katika kutimiza majukumu yako haya makubwa na nyeti.
“Shehe wangu kwa muda wote tumeishi pamoja hapa tukiwa majirani… ukitimiza wajibu wako uliokuwa nao nasi tukiendelea kutimiza majukumu yetu katika jamii ya Watanzania, nakutakia kila la heri katika kuwatumikia na kuwaongoza kiroho Waislam wa Tanzania,” alisema Dk. Slaa nyumbani kwa Sheikh Zuberi leo mara baada ya uteuzi wa Kaimu Mufti Mkuu wa Waislam kufanyika.
Imetolewa leo Jumatatu, Juni 22, 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Next Post Previous Post
Bukobawadau