ZAO LA NDIZI KULIMWA KIBIASHARA NA KUTAFUTIWA MASOKO YA KIMATAIFA ILI KUKUZA UCHUMI WA MKOA WA KAGERA
Wakulima na Wajasiliamali wa zao la ndizi Mkoani Kagera wapewa somo na
shirika lisilokuwa la Serikali la BTC Tanzania (Belgium Training Cooperative
Tanzania) juu ya kulima kwa wingi zaidi zao hilo kibiashara na kufundishwa
mbinu mbalimbali za kutafuta masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.
Kutokana na zao la ndizi kuwa ndiyo zao tegemezi kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imepokea ufadhili kutoka nchini Ubelgiji kupitia shirika la BTC Tanzania wa
kutekeleza miradi mbalimbali itakayoendeleza zao la ndizi ili liwe zao la
biashara Kitaifa na Kimataifa.
Kupitia BTC Tanzania vikundi vya wakulima wa zao la ndizi ikiwa ni
pamoja na wajasiliamali walijengewa uwezo
jinsi ya kuongeza uzalishaji wa
zao hilo, kuongeza thamani (mnyororo wa thamani wa zao la ndizi) pamoja na
uwezo wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 10 Februari, 2016 katika Ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera yalikuwa ya mwanzo kabla ya miradi hiyo ya
kukuza uchumi wa Mkoa kupitia zao la ndizi haijaanza kutekelezwa kwa ngazi za
chini kabisa vijijini.
Miradi hiyo ya kuendeleza zao la ndizi kwa kuliongezea thamani na
kulitafutia masoko itatekelezwa na Makampuni mawili yasiyokuwa ya Serikali chini ya Belgium
Training Cooperative Tanzania ambayo yatahusika na wakulima moja kwa moja hadi
ngazi za chini nayo ni, Ndugu Tanzania
LTD na Bluwat and Investment.
Ndugu Tanzania LTD, Hii ni
Kampuni ambayo itakuwa inajihusisha na uongezaji wa thamani ya zao la ndizi
pamoja na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Bluwat and Investment, ni
Kampuni itakayojihusisha na kuwafundisha wakulima katika vikundi jinsi ya
kutunza fedha zao (kuweka akiba), na jinsi ya kuanzisha SACCOS za kukopeshana, na
pia watawaelekeza wakulima jinsi ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao kwa
ujumla.
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wanahamasishwa kuchangamkia fursa hiyo ili
kujiajiri katika sekta hiyo ya kilimo na kulifanya zao la ndizi kuchangia
uchumi wa nchi na kwa mwananchi mmoja mmoja ambaye ni mkulima hasa kwa zao la ndizi ambalo limekuwa
likistawi kwa wingi Mkoani humo.