UWT YAUNGA MKONO UAMUZI YA RAIS KUHUSU MAKANIKIA NA MIKATABA YA MADINI.
Jumuiya ya
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt
John Pombe Magufuli na kupongeza jitihada zake za kupambana na aina zote za
ubadhirifu, dhulma na unyonyaji uliobainika kwenye mikataba ya uchimbaji na
usafirishaji madini, na hivyo kuhakikisha maliasili za Taifa zinatumika kwa
manufaa ya watanzania wote.
Pia, Umoja
wa Wanawake Tanzania unatoa pongezi kwa wajumbe wa Kamati kwa weledi, uzalendo
na ujasiri mkubwa wa kubainisha hasara kubwa iliyopatikana kwa Taifa letu
kutokana na usafirishaji wa makanikia, na hivyo UWT inakubaliana na kuunga
mkono mapendekezo yote ya Kamati na uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe
Magufuli wa kutaka kurekebisha mikataba na sheria za usimamizi na uchimbaji wa
madini nchini.
Aidha UWT
inapongeza hatua za awali za mazungumzo yaliyofanywa leo tarehe 14/06/2017
baina ya Mhe Rais Dkt Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold
Corporation ambao ni wamiliki wa Kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L.
Thornton na kukubaliana kuhusu malipo ya fedha zilizopotea na kushirikiana
katika ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
Kufanikiwa
kwa mazungumzo hayo, na marekebisho ya sheria na mikataba ya madini kutawezesha
Watanzania kupiga hatua ya kujikomboa na umasikini, hususani Wanawake ambao wameendelea
kukosa huduma za msingi za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji na malazi bora. Wanawake
wengi wanahangaika kwa kukosa mitaji ya biashara na mikopo ya wajasiriamali wadogo
huku wakisumbuliwa kulipa tozo, ushuru na kodi za kero.
UWT inatoa
rai kwa wananchi wote kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kujivunia utanzania wetu. Tunamuombea Mhe Magufuli, MwenyeziMungu
azidi kumpa afya njema, moyo wa ujasiri, uzalendo na upendo kwa watanzania.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
AMINA MAKILAGI (MB)
KATIBU MKUU
JUMUIYA YA UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA.
14/06/2017