Yanga kupeleka Kombe Bungeni
MABINGWA Afrika Mashariki na Kati Kagame Cup na Tanzania Bara, Yanga, leo wataondoka Dar es Salaam kwenda Mkoani Dodoma kwa ajili ya kupeleka Kombe la Ubingwa kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza Dar es Salaam jana mratibu wa ziara hiyo maalum, Cellina Agustino alisema kesho wachezaji wa Yanga wakiwa na kombe hilo wataingia Bungeni.
Agustino alisema mara baada ya tafrija fupi itayakayofanywa na wabunge hao wachezaji wa Yanga muda wa jioni watafanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Jamhuri na keshokutwa Jumamosi watakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Polisi Dodoma.
Alisema kupelekwa kwa kombe hilo bungeni ni ombi la wabunge baada ya Tanzania kufanya vizuri katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja kulibakisha kombe hilo la Afrika Mashariki na Kati nchini Tanzania.
Agustino alisema mechi hiyo ya kirafiki ina lengo la wakazi wa Dodoma kuiona timu yao ambayo imechukuwa Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara miezi miwili iliyopita na Julai 10 ilinyakuwa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup).
Alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika, ambapo Yanga itakuwapo mkoani humo kwa muda wa siku nne na kurejea Dar es Salaam siku ya Jumapili.