Bukobawadau

MICHAEL SATA WA ( PF)PATRIOT FRONT AFANYA HISTORIA ZAMBIA!!!Akiondoa chama kilicho Ongoza Miaka 20

ZAMBIA imeandika historia mpya katika mfumo wa utawala wake, kufuatia kiongozi wa wa chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF), Michael Sata kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo.Sata (74), ambaye pia anajulikana kwa jina maarufu la "King Cobra" alitangazwa jana kuwa nshindi wa nafasi hiyo dhidi ya rais aliyekuwa madarakani, Rupiah Banda wa chama cha MMD.Mgombea huyo wa upinzani ambaye aligombea nafasi hiyo mara nne na kushindwa, safari hii alipata kura 1,150,045, sawa na asilimia 43, wakati Banda wa aliambulia kura 961,796, sawa na asilimia 36.1. Idadi ya watu waliojiandikisha ni 5.2 milioni.

Sata anakuwa rais wa tano kuiongoza nchi hiyo ambayo ilijinyakulia uhuru wake mwaka 1964 kutoka kwa Uingereza kwa kuking’oa madarakani chama cha MMD kilichokaa madarakani kwa miaka 20.

Jaji Mkuu wa Zambia, Ernest Sakala jana alitoa tangazo la matokeo hayo ambayo yalikuwa yansubiriwa kwa hamu na wananchi nchini humo.Hata hivyo, mapema, vurugu ziliripotiwa kutokea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ikiwa ni hatua ya kuyapinga matokeo hayo.

Awali watu wawili waliuawa kufuatia ghasia katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na Mkuu wa Polisi katika ukanda wa Shaba, watu wamejitokeza katika barabara za mji wa Kitwe na Ndola wakirusha mawe ambapo vurugu kubwa bado zinaendelea kushika kasi katika maeneo hayo.


Habari kutoka nchini humo zinaendelea kusema kuwa, ghadhabu hizo zimechochewa na agizo la Serikali kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza matokeo bila ya idhini ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (ECZ).Vurugu ziliendelea kushika kasi katika mji wa Kitwe uliopo kilometa 300 kutoka Mji Mkuu wa Lusaka, ambapo waandamanaji waliteketeza soko. Rais Banda alimshinda Sata mwaka 2008 kwa tofauti ya kura 35,000, matokeo ambayo yaliozusha ghasia kutokana na wafuasi wa chama hicho cha upinzani kudai wamedhulumiwa.Tangu uchaguzi wa mwaka 2008, watu wengine milioni moja walijiandikisha kupiga kura, wengi wao wakiwa ni vijana wasio na ajira.

Hali hiyo inaashiria kuwa vijana hao walipiga kura za hasira dhidi ya chama tawala.Juzi, ghasia kubwa ziliripotiwa kuibuka katika Jimbo la Kaskazini mwa Zambia la Ukanda wa Shaba, kwenye ngome kuu ya Sata, kufuatia kusitishwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi, yaliyokuwa yakionyesha kwamba kiongozi huyo anaongoza. Matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Irene Mambilima yalikuwa ni yale yaliyokusanywa katika majimbo 85 kati ya 150.

Historia ya Sata
Jina lake kamili ni Michael Chilufya Sata ambaye alizaliwa mwaka 1937 katika Jimbo la Kaskazini eneo la Mpiga.
Sata alikuwa Ofisa wa Polisi, na pia alishakuwa mfanyakazi wa shirika la reli nchini Zambia wakati wa utawala wa kikoloni.Alianza kuingia kwenye siasa mwaka 1963, wakati ambapo Zambia ilipokuwa katika harakati ya kujitoa katika utawala wa kikoloni.Mwaka 1985, Sata alikuwa kiongozi wa chama kilichokuwa na wafuasi wengi zaidi mjini Lusaka cha UNIP, kikiongozwa na Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Keneth Kaunda.

Akiongoza UNIP, Sata alifanya kazi nyingi za kujitolea zikiwamo za kusafisha mitaa, kurekebisha njia za reli pamoja na kutengeneza madaraja ndani ya mji huo.Baada ya hapo, Sata akawa Mbunge wa Jimbo la Kabwata llililopo Lusaka. Alianza kuwa mpinzani wa Serikali iliyopo madarakani, kuanzia utawala wa Rais Kenneth Kaunda.

Alimshutumu serikali ya Kaunda akisema utawala wake una kasoro nyingi ambazo zinavuruga maendeleo ya wananchi.Kutokana na msimamo huo, aliamua kutoka chama cha UNIP na kujiunga na chama cha MMD wakati vuguvugu la vyama vingi mwaka 1991.

Baada ya Frederick Chiluba kumshinda Kaunda mwaka 1991, Sata alikuwa mmoja wa watu maarufu ambaye anakubalika kutokana na kuwa na wafuasi wengi.Ndani ya MMD, Sata alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa, Kazi pamoja na Mambo ya Afya.Mwaka 2001, Sata alikianzisha chama cha Patriotic Front na hapo ndipo alipoanza kufahamika kwa jina la ‘King Cobra’.

Mwaka 2006 alipambana na Levy Mwanawasa katika Uchaguzi Mkuu ulioishia kwa kutangazwa kuwa mshindi wa pili.Mwaka 2008, baada ya Rais Mwanawasa kufariki dunia, Sata aligombea tena nafasi ya urais, safari hii ikiwa ni dhidi ya Makamu wa Rais Rapia Banda.Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na upinzani mkali, Sata alishindwa kwa kura 35,000 na kuzua mgogoro mkubwa kutokana na wafuasi wake kuamini kwamba wameporwa ushindi.

Kushinda kwa Sata kwenye uchaguzi wa mwaka huu, kunatimiza kiu ambayo alikuwa nayo kwa muda mrefu.Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema kwamba Sata ana kazi ngumu ya kuweza kuwaridhisha wananchi wengi wa Zambia ambao wanakabiliwa na maisha magumu pamoja na maelfu ya vijana ambao hawana kazi.

Ni funzo kwa Waafrika
Mwanasiasa Mkongwe nchini Ibrahimu Kaduma, alisema jambo kubwa ambalo viongozi wengine wa Afrika wanapaswa kujifunza kutokana na uchaguzi huo wa Zambia, ni kukubali matokeo kama alivyofanya Banda.“Nafurahi sana kuwa Banda amekubali kushindwa. Ni Zambia tu na Ghana ndio walioweza kufanya hivyo.

Viongozi wengi waliopo madarakani inapotokea kushindwa huwa hawakubali. Ingependeza kama chaguzi zote za nchi zetu (Afrika) zingekuwa hivi,” alisema Kaduma.Kwa upande wake, Profesa Peter Maina, alisema yaliyotokea Zambia ni maendeleo mazuri na somo tosha kwa viongozi wa Kiafrika ambao bado wapo madarakani.“Ni vyema kama viongozi waliopo madarakani wataruhusu kuwe na uchaguzi huru na haki. Tuwe na uchaguzi wa kweli siyo uchaguzi mfano.

Anayeshinda ashinde kweli na anayeshindwa akubali,” alisema Profesa Maina.Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Zanzibar Isimael Jusa, alisema kilichotokea Zambia ni matokeo ya kuwa na tume huru ya uchaguzi.“Michael Sata amegombea mara nyingi tu akawa anashindwa, lakini sasa kutokana na hali ilivyokuwa na wananchi waliamua kufanya mabadiliko na tume ya uchaguzi ikaamua kuwa huru,” alisema Jusa.

Anaeleza pia kuwa, sera za Sata za kutaka rasilimali za madini ya shaba yawanufaishe wananchi wote, ni moja ya mambo yaliyowafanya wananchi kumchagua.“Sasa hata Serikali yetu ijiulize ni kwa namna gani wananchi wanafaidika na rasilimali zao.

CCM ijue kabisa wananchi wakisema basi lazima itakuwa hivyo. Ni vyema tukawa na tume huru na watu waheshimu demokrasia,” alisema Jusa.

CANZO GAZETI LA MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau