Muswada wa Katiba Mpya: Hotuba ya Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni (Tundu Lissu)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
Mh. Tundu Lissu.
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011
(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo.
Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika kuondoa Hati ya Dharura na hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kutunga sheria uliowekwa na kanuni za 80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007. Katika kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika - liliiagiza Serikali kufanya mambo yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu cha tarehe 15 Aprili 2011:
(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi kuufikiria Muswada huu. Katika kufanikisha hili, “... iandae Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada huo badala ya kupewa tafsiri tu na watu wengine;
(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi kuuelewa na kuutolea maoni;
(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani tayari tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)
Mheshimiwa Spika,
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “... Muswada huu uko ndani ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge,Muswada ulikwishasomwa kwa mara ya kwanza na kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya kuanza kujadiliwa.
Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “... kwa lengo la kuisaidia katika uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa Kamati ilikuwa ni kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “... kufanya marekebisho katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri ... anayehusika na Muswada huo kufanya mabadiliko....” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa lengo la kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima.
Mheshimiwa Spika,
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na Serikali. Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na kuonyesha imesainiwa tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani uliopigiwa kelele sana na wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili zilizopita, ikiwa ni wiki moja baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko na Serikali bila kupata ushauri wa Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4) ya Kanuni za Bunge. Badala ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011.
Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani kama nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa Zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima.
Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa nay a kimsingi katika Muswada wa Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni busara na ni sound policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa Muswada, itawajibika “... kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba (na) kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi....” Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar....” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “... kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar....”
Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi,msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano!
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, ibara ya 7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.”
Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”
Muswada unapendekeza kumpa Rais - baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji kufanya hivyo, Rais – “kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za rejea, kwa mujibu wa ibara ya 8(3), “... zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa Sheria hii.”
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi - kwa mujibu wa wa ibara ya 17(1)(d) na (2) ya Muswada - kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa Rasimu ya Muswada wa Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji mjadala wa kitaifa na maamuzi ya wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba Mpya.
MAMLAKA YA RAIS
Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana ya kiutendaji na ya kiutungaji sheria.
Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za serikali na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha ambao umefanywa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali.
Sio vibaya, katika kuthibitisha jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977: “... Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote....” Na kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya mwaka 1978 na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu – ya kuwa dikteta!
Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya kidemokrasia.
Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais hawa ni watu wasiokuwa tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha kiutendaji na moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Tume ni mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama watendaji wengine wa Tume ni watumishi wa serikali walioteuliwa wa Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais baada ya kukubaliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine wa Tume nao ni watumishi wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya Muswada Mpya, ni wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa wajumbe, watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa Tume. Kwanza, badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama inavyopendekezwa katika Muswada, tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’ (multiparty Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini.
Hii haina maana kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa katika ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa Tume ya Vyama watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili kuwawezesha kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya.
Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba wajumbe walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama tunavyopendekeza watatakiwa wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pendekezo hili litahakikisha kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa vetted na chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga kuaminiana baina ya Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu ambacho ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kisiasa.
Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume vile vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu wa kiutawala na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma bali hufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa.
Hii ni kwa sababu, kisheria na hata kivitendo, watendaji na watumishi karibu wote wa umma hujiona wanawajibika kwa mamlaka zao za uteuzi, yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na watumishi hawa wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali ambao nao ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya maamuzi yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama tawala.
Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa kutoka kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka na uhuru unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili isiingiliwe kweli na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10 ya Muswada, inabidi mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais na/au Waziri ambaye ni mdau mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa Katiba Mpya.
Na namna ya pili ya kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na watumishi hawa nje kabisa ya utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya kuwataka waombe kazi, kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio huru.
Mheshimiwa Spika,
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao (security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili.
Kwa maana hiyo, mapendekezo ya ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa Tume, haijaweka utaratibu wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe pale kunapokuwepo tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa katika ibara ya 12(2) na Jedwali la Pili la Muswada.
Kutokuweka utaratibu huu kuna hatari kubwa kwani, kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya nidhamu pale ambapo sheria haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii ina maana kwamba bila kuweka utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe wa Tume, Rais ndiye atakuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu yeye ndiye aliyewateua!
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina mbili. Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa Tume.
Pili, kwa vile – kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya – hadidu za rejea ni hati ya kisheria inayotakiwa kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu hati hii iwekwe wazi katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais.
Watanzania lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe wa Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na wafahamu kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya mtu mmoja hata kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa Tume kwa wananchi kwani itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume kwa hadidu za rejea zilizowekwa wazi katika sheria.
Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari ibara za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi za Tume, mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa namna ya kuzifanya.
Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba Rais ana mamlaka makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya, mapendekezo ya ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na yanaweza kuondolewa bila kuathiri maudhui ya Muswada. Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9,haijulikani Rais atatoa maelekezo gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na namna ya kuzitekeleza.
Kwa upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza kuleta mkanganyiko na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo Rais atatoa hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama yanavyopendekezwa na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo, ni kwamba ibara ya 8 ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri ili kuweka wazi zaidi hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.
Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho makubwa. Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba Mpya katika Bunge la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu Wakuu ambao wote ni wateuliwa wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayoruhusu uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha matokeo yake ya mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama chake cha CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
SIFA ZA WAJUMBE
Mheshimiwa Spika,
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa Tume:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii.
Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya.
Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika Muswada, hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza masharti yote husika ya kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni ya wananchi wa Tanzania kwa kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi za uwakilishi za umma kama Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri za Serikali za Mitaa hawajui wala hawazingatii maslahi ya umma na kwa hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba!
Kama ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na kwa hiyo kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za kuteua Tume! Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa Katiba Mpya inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi kuwa Wabunge, Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa vilivyowapendekeza watu hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa hawana sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!
Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani, hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge havipati fursa ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa katika hatua muhimu za uundaji wake. Pili, lengo kuu vile vile ni kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama chake cha CCM, wanadhibiti mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya uundaji wake.
Endapo watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM watakuwa na nafasi kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na mchakato walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa sababu, kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya nyuma, wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa kupendekeza mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika historia yetu na mfumo wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume inakuwa na utaalamu, uzoefu na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume wawe ni wale wenye sifa zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na (d) ya Muswada.
Kwa sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine visivyojulikana wazi kwa wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na ‘vigezo vingine ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais mwanya wa kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika taasisi za uwakilishi au katika vyama vya siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo kiongozi husika ana sifa za kitaaluma zinazotakiwa!
MISINGI MIKUU YA KITAIFA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi mikuu inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha ... kutokugusika na utakatifu (inviolability and sanctity) wa mambo yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na badala yake yamewekwa maneno mapya ‘... kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo....’ Mabadiliko haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu iliyojitokeza wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la pendekezo hilo lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata mkubwa kama vile suala la Muungano.
Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa ibara mpya ya 9(3), “... Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.” Tafsiri halisi ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa juu ya ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na kuboresha masuala hayo.’
Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na kuboresha ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wenye Serikali mbili. Hii ni kwa sababu katika mambo yote yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa, ni ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na mgogoro mkubwa kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano.
Ukiacha ‘ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa kuwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya uhai wa Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa mujibu wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Kamhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar, Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar’ ni mambo yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili mradi tu mabadiliko hayo yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na wa Tanzania Zanzibar.
Kwa sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada kwamba ‘misingi mikuu ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na kuidumisha tu halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga mambo ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe kabisa ili kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga mkono, kila jambo linalohusika na Katiba Mpya.
NAFASI YA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Itakumbukwa kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika mchakato wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo cha Zanzibar ni kuwepo hisia kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa katika Muswada huo.
Muswada sio tu kwamba umetekeleza matakwa yote ya ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda mbali zaidi kwa kuifanya Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa Tanzania. Hii imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.
NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike kwa ‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais ‘kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Vile vile, ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa Tume; ibara ya 8(1) na (2) inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu uteuzi wa Katibu wa Tume, zote zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa Zanzibar. Aidha, ibara ya 13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume inalazimu makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao ni wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na watendaji wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti ya Tume. Kwa mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza kazi yake, Tume itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar.
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar, “... atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya.
Maana yake ni kwamba Rais wa Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana na Rais wa Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge la Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni nchi huru kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu ishirikishwe kwa usawa, bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote ya kikatiba yanayopendekezwa na Muswada.
Kama Profesa Palamagamba Kabudi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alivyosema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa, Zanzibar sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo hakuna tena nchi inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa sababu tangu kusainiwa kwa Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa, masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala ya iliyokuwa Tanganyika.
Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na kwa usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena na iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo! Hii ndio kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza kuirudisha Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!
Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu.
Kwanza, Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa habari kwamba alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la Mapinduzi. Pili, mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali hiyo.
Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar yanawakilishwa ndani ya ‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya Muungano. (ibara ya 54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa madaraka uliopo katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe wanaoweza kuongoza mikutano ya Baraza hilo.
Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu wa Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “... ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano....” Kwa maana hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar kuwa sio tu mshiriki sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaenda kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia na Hati za Muungano wenyewe. Kwa mapendekezo haya, endapo Rais wa Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa wajumbe wa Tume au Katibu wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha mchakato mzima wa kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano!
UWAKILISHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.”
Hii ina maana kwamba wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza Katiba inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar kushirikishwa kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki.
BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika, Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa kutokana na uwakilishi wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika Sehemu ya Tano ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii. Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama wawakilishi nao pia watateuliwa na Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa kiserikali!
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya Muungano, wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa majimbo ya uchaguzi. Kwa composition ya sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya Zanzibar ni hamsini. Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba, Baraza la Wawakilishi Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna wabunge wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’
Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni ishirini na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho, kuna wabunge wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge watatu ambao wote ni wa kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa lenye wabunge 353, wabunge wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu au karibu 23.5% ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa majimbo hamsini ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na wawakilishi ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sasa ni themanini na moja. Kwa maana nyingine ni kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya 20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati ya wajumbe 545 wa Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa na 30% ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada kwani ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “... idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar ... haitapungua theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la Katiba ni wajumbe 182.
Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada kuhusu uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182 ambayo ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati ibara ya 21(1) inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wachaguliwe kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya 21(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke upande mwingine.
Sambamba na pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara ya 21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima atoke upande mwingine.
Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana potofu kwamba Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano.
Hii inathibitishwa pia na pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka Katiba Mpya ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Tanzania Bara na vile vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba iwe ni kwa masuala ya Muungano yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na kura ya turufu kwa mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari wakati Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya Muungano.
Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”!
UDHOOFISHAJI WA UPINZANI
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana athari nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya 20(2) ya Muswada yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi 400 katika Bunge la Katiba ambalo lina wajumbe 545.
Kwa upande mwingine Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa maana ya uwakilishi katika Bunge la Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge hilo, licha ya kuwa na wabunge wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania Bara na licha ya kupata kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF wa mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, upinzani wa kisiasa Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na hasa Bungeni na kwenye chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa ikishirikiana na CCM kuipinga CHADEMA.
Kwa mapendekezo haya, kambi ya CCM na CUF katika Bunge la Katiba inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe 465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo! CHADEMA ambayo kwa sasa ndio chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake 48 na vyama vya kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na jumla ya Wabunge sita.
Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini!
Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia, athari mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika Bunge la Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na kupunguza nguvu na ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee kinachobeba matarajio na matamanio ya Watanzania wengi wanaotaka mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba Bunge la Katiba lenye uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo pengine itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi mkuu’ uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni wazi kuwa lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya Katiba ya sasa!
‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya Tanzania. Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne za Katiba hiyo. Kama ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba kitendo cha kutunga Katiba Mpya vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya Zamani, basi sisi Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi wote tulikula kiapo cha kuilinda, kuihifandhi na kuitetea.
Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa kuu ya kuwa wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa.
Kuligeuza Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Bunge la Katiba ni sawa na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa hawana haki ya kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa sababu ya kuwa na kilema cha kisheria kinachowakataza kuchaguliwa kuwa Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya Katiba ya sasa inatamka wazi kwamba “... ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote....” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni ya Watanzania ambao wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali, ubaguzi wa aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba ya kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki katika Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais.
Pili, Bunge la Katiba ni chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi na kwa mila na desturi zinazokubalika na kutumika kimataifa, wajumbe wa Bunge la Katiba huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali vyama vya siasa na huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe wa Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na masharti yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika, Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa kihistoria wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika michakato wa kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa ibara ya 27(1), kutakuwa na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya 30, watu wote walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa na haki ya kupiga kura katika kura hiyo ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya 32(2), matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa zaidi ya 50% ya kura zote zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa Zanzibar.
Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa kisheria ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na urithi wa kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961.
Hata hivyo, mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya hatari. Kwanza, ibara ya 27 inapendekeza kwamba kura ya maoni itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko pengine miswada yote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama unaopendekezwa katika Muswada huu.
Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo Muswada huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi ulivyo – Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa taifa letu kwa njia ya amani na maridhiano.
Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara.
Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya kanuni ya 86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge hili likatae Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali imeleta Muswada Mpya na wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila kufuata masharti ya kanuni ya 84(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo ya Bunge hili tukufu kuhusu kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria, kuuelewa na kuutolea maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara ya 21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi, na haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI & WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA