Bukobawadau

AJALI YA NOAH YAUA WATU WATANO

ABIRIA watano wa gari dogo la biashara aina ya Noah, akiwamo dereva wa wake, wamekufa na wengine 11 kujeruhiwa akiwamo mmoja vibaya, baada ya gari hilo kugongana na basi kubwa la abiria.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 2.45 asubuhi katika barabara kuu ya Mwanza – Musoma katika eneo la Lugeye ambapo Noah namba T 716 BMV iligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Zakaria namba T 655 BDP aina ya Scania. Noah ilikuwa ikitoka Magu kwenda Mwanza Mjini.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, dereva wa Noah alipofika Lugeye ghafla aligeuza mwelekeo akitaka kurudi alikotoka.

Alisema waliojeruhiwa walikuwa katika basi la Zakaria ambapo 10 wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Magu na mmoja Mbarouk Taka (52) aliyevunjika mkono alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza Mjini.

Kamanda Barlow alisema abiria wote watano kwenye Noah walipoteza maisha na waliotambulika ni pamoja na dereva Deus John (42) na Peter Rudisha (40) huku wengine watatu ambao wote ni wanaume wakiwa bado kutambuliwa na miili yao imehifadhiwa Bugando.

Alitoa mwito kwa madereva kuwa makini barabarani kwa kuthamini maisha ya wanaowabeba kwenye vyombo vyao vya usafiri.
Next Post Previous Post
Bukobawadau