MGOMO WA MADAKTARI TANZANIA WAMALIZIKA
Serikali ya Tanzania imewasimamisha kazi Maafisa wa Ngazi za juu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wa nchi hiyo katika hatua muhimu ya kumaliza mgomo wa madaktari unaoendelea nchini humo.
Akitangaza uamuzi wa serikali Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyewatembelea madaktari waliogoma, amewataja waliosimamishwa kazi mara moja kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Blandina Nyoni na Mganga Mkuu Dk Deo Mtasiwa.
Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wanasimamishwa kazi ili pia kupisha uchunguzi dhidi yao kwa vile pia wana tuhuma nyingine kinyume na maadili ya kazi.
Waziri Mkuu Pinda amesema wengine wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kusubiri uamuzi wa Rais, ni pamoja na Waziri wa Afya Dk Haji Mponda na Naibu wake Dk Lucy Nkya.
Mgomo wa madaktari ambao umedumu nchini Tanzania kwa takriban wiki tatu sasa umesababisha kuzorota kwa huduma mbalimbali katika hosptali za umma na nyingine kufunga vitengo muhimu.
Madaktari hao wanadai nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi pamoja na marupurupu mengine ambapo serikali imekubali kuyashughulikia.
Katika makubaliano na Waziri Mkuu madakatari waliogoma wamekubali kumaliza mgomo na Ijumaa wanatarajiwa kurejea kazini.
chanzo BBC swahili.