Bukobawadau

HATIMAYE LULU AZUNGUMZA ASEMA HAKUMSUKUMA KANUMBA



Baada ya kugoma kutoa maelezo kwa takribani siku nzima ya jana, mwanadada Lulu hatimaye amezungumza na polisi na kuelezea kilichotokea baina yake na marehemu Steven Kanumba. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema Kanumba alikufa kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu.

 "Kanumba amefariki usiku wa kuamkia leo (jana) majira ya saa tisa usiku, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi kati yake na rafiki yake wa kike anayejulikana kwa jina la Elizabeth Michael 'Lulu' mwenye umri wa miaka 18.

Alisema kabla ya ugomvi huo kutokea kati yao wakiwa chumbani, simu ya Lulu iliita na akaamua kutoka nje kupokea kitendo kilichomuudhi Kanumba.

Kamanda Kenyela alisema Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti akitaka aelezwe kwanini alitoka nje kupokea simu huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.

Aliongeza baada ya Lulu kuona Kanumba akimfuata aliamua kukimbia kutoka nje ya geti , lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba  alimkamata na kumrudishwa ndani.

Kamanda Kenyela, alisema Kanumba akiwa amemshikilia waliingia wote chumbani na kufunga mlango.

Hata hivyo, alisema haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu anadi kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba.

Kamanda huyo alisema Lulu anaeleza kuwa baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini.

Alibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Kanumba alikuwa amekunywa Whisky (pombe kali) aina ya Jacky Daniel, hata hivyo, bado wanachunguza zaidi kujua kama kweli Kanumba alilegea tu na kuanguka, ama alipigwa na kitu kizito kichwani au alisukumwa kwa nguvu na kumfanya aangukie kisogo.

“Uchunguzi ukikamilika tutampeleka mahakamani kwa tuhuma za mauaji,” aliongeza Kamanda Kenyela.


SOURCE: mwananchi.co.tz
Next Post Previous Post
Bukobawadau