Bukobawadau

MDAU THEONIST RUTASHOBORWA AFARIKI DUNIA

Marehemu Lutta.
MJUMBE wa Kamati ya Utendaji wa klabu ya Young Africans Sports Club,
Wakili Theonist Rutashoborwa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo
katika hospitali ya Agha Khan alipokuwa amepelekewa usiku huo mara
baada ya kuzidiwa na ugonjwa wa Shinikizo la Damu na Kisukari.

Rutashoborwa alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji wa klabu ya Young
Africans toka mwaka 2010, akiingia katika kamati hiyo iliyoingia
madarakani katika uchaguzi mkuu wa klabu chini ya uongozi wa
Mwenyekiti Llyod Nchunga.
Marehemu amefariki ghafla jana usiku, ikiwa ni mda mchache toka afike
uwanja wa ndege wa Mwl. JK Nyerere akitokea Kilimanajaro ambapo siku
mbili zilizopita alikuwa jijini Mwanza pia kwa shughuli zake za kikazi
za uanasheria.
Msemaji wa familia ya marehemu amesema kuwa mara baada ya kufika
uwanja wa ndege wa KIA jana alianza kujisikia vibaya na kulalamika
kuishiwa nguvu hivyo mara baada ya kufika uwanja wa ndege wa JK
Nyerere alikimbizwa moja moja hospitali ya Agha Khan, ambapo mauti
yalimfika.

Marehemu alishiriki kikamilifu shughuli zote za kamati ya utendaji na
klabu kwa ujumla, na mara ya mwisho alikuwepo jijini Tanga na timu ya
Young Africans wiki mbili zilizopita katika mchezo wa ligi kuu ya
Vodacom kati ya wenyeji Coastal Union na Young Africans.

Marehemu ataagwa Jumatatu katika kanisa Katoliki Parokia ya Kijichi,
na jioni mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea mjini Bukoba,
mazishi yatafanyika siku ya Jumatano katika kijiji cha Bukayaba
kilomita 22 kutoka Bukoba mjini.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amen!

Bwana ametoa na Bwana ametwaa!
Next Post Previous Post
Bukobawadau