KIFO CHA MDAU WA CONTINENTAL AL HAJI AMIR ROSHAN-TFF YATOA RAMBIRAMBI
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji, Marehemu Amir Roshan (pichani kushoto). Roshan alikuwa akiwakilisha mikoa ya Kagera na Shinyanga na alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu tangu afanyiwe operesheni ya kichwa mwishoni mwa mwaka 2010.
Roshan ambaye alianza kuingia kwenye uongozi wa TFF wakati huo ikiwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mjini Kibaha mwaka 1993, amezikwa jana mchana kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa vipindi vitano mfululizo. Alichaguliwa katika uchaguzi wa mwaka 1993, jijini Dar es Salaam (1996), jijini Arusha (2001), jijini Dar es Salaam (2004) na jijini Dar es Salaam (2008).
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ameelezea masikitiko yake na mshtuko mkubwa kutokana na kifo cha kiongozi huyo wa muda mrefu kwenye mpira wa miguu, hasa Kanda ya Ziwa akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA).
Osiah amesema TFF inatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na familia ya mpira wa miguu kwa kumpoteza ndugu yao kipenzi, na Shirikisho litamkumbuka kwa mchango wake kwenye mpira wa miguu na dhamana aliyoibeba kwa muda mrefu akiongoza mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa na Taifa.
Msiba huu ni pigo kwa familia ya Roshan, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji.
Mungu aiweke roho ya marehemu Amir Roshan mahali pema peponi. Amina