Bukobawadau

MAHUBIRI YA LEO J.PILI: 22/07/2012 KUTOKA KWA MDAU MCHUNGAJI KOKU; Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu na Ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote, Amen.



Neno: Injili ya Luka 11:33-36:

Kichwa: Neema ya Mungu Yatuwezesha

Shabaha: Watu wakutane na Neema ya Yesu

UTANGULIZI:

Yesu ni Nuru ya ulimwengu, wote wanaomfuata hawatakiwi kuishi maisha ya giza kamwe (linganisha Yohana 8:12). Je maisha yetu yanayo nuru ya Yesu?

•1. Nuru Maishani Mwetu:

Mtu anapowasha taa nia yake ni kuleta nuru. Mfano wa Yesu tukiusoma sio rahisi kuelewa kwa haraka. Lakini yawezekana maana yake ni hii, Mwanga wa mwili hutegemea jicho, jicho likiwa na afya mwili wote hupokea mwanga unaouhitaji. Hivyo hivyo, mwanga wa maisha hutegemea moyo, moyo ukiwa safi, maisha yote huongezeka katika mwanga au nuru, lakini moyo ukiwa si safi (mkengeufu) maisha yote hutiwa giza.

Yesu aliyetupa nuru yake, anataka nuru hiyo iliyo ndani yetu iwe inaongoza siku zote za maisha yetu.

•2. Vitu Vinavyoleta Giza Maishani Mwetu:

Ni mambo yapi basi yanatuletea giza ndani mwetu? Kati ya mengi nitaje matatu:

•(a) Ugumu wa Mioyo:

Tukiiruhusu dhambi kutawala maisha yetu, polepole huifanya mioyo yetu kuwa migumu. Mwanzoni mtu anakuwa na hofu ya Mungu, lakini kadiri unavyoendelea kutenda dhambi unakuwa sugu.

•(b) Maisha ya Mazoea:

Watu wanaposikia Neno la Mungu huwa linawagusa, lakini baadaye hulizoea na kutolipa nafasi katika maisha yao.

•(c) Maisha ya Kutotii:

Watu wanafundishwa kuijua kweli ya Mungu katika maisha yao, lakini hutenda yaliyo kinyume. Na wanapoitwa kumrudia Mungu, huchukua uamuzi wa kwenda mbali na Mungu.

•3. Neema ya Yesu:

•· Kwa kuwa siku hii ya leo tumesikia juu ya mambo yanayotuletea giza katika maisha yetu, ni vyema basi kila mmoja wetu akajihoji na kuangalia kama ameruhusu dhambi za namna yeyote kutawala maisha yake (soma Marko 7:20), 2

amelipa Neno la Mungu nafasi au amelizoea na tena kama anazingatia ukweli wa mapenzi ya Mungu maishani mwake?

•· Wapendwa, nuru ya Yesu inatuongoza na kutupa uzima wa milele. Yeye hataki jupotee na kupata mshahara wa dhambi ambao ni mauti (Rumi 6:23).

•· Sasa tutapataje kuondokana na giza ambalo husonga mioyo na maisha yetu? Jibu ni rahisi. Ni kumpokea Yesu aliye nuru ya ulimwengu katika maisha yetu. Tukimpa nafasi katika mioyo yetu (Zaburi 119:11), giza linalotusonga hutoweka, shetani hukimbia (Yakobo 4:7) na tunakuwa watoto wa Mungu, watakatifu wanaomzalia matunda ya Roho (Galatia 5:22-23). Bila Yesu sisi hatuwezi kufanya jambo lolote (Yohana 15:5b).

•4. Mwisho:

Ninaamini hakuna anayependa kukaa katika maisha ya giza. Kwa kuwa tumeshajua jinsi ya kutoka katika hayo maisha ya giza, ninapomalizia mahubiri haya ninapenda kuuliza swali hili: Ni wangapi siku hii ya leo wanatamani kuchukua hatua ya kumpokea Yesu aliye Nuru katika maisha yake?

Tumwombe Yesu Mwenye Neema atujalie Neema yake ili tuweze kuishi na kwenenda kama Watoto wa Nuru katika maisha haya hata uzima wa milele.

Na amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu (Filipi 1:7).

Sala:

Bwana Yesu uliye Nuru ya Ulimwengu, tujalie Neema yako ili tudumu kuwa wana wa Nuru. AMEN.
Next Post Previous Post
Bukobawadau