MAONESHO YA NANE NANE 2012 KAGERA YAENDELEA KYAKAILABWA - BUKOBA
Meya wa Manispaa ya Bukoba Mh. Anathory Aman akikata utepe wakati wa ufunguzi wa nane nane.
Maonesho ya NANE NANE 2012 Mkoa wa Kagera yanaendelea Katika uwanja wa Kyakailabwa baada ya kuanza tarehe 01/08/2012 na kufunguliwa rasmi tarehe 03/08/2012 na Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe. Anathory Amani aliyetembelea maonesho hayo na kujionea teknolojia mbalimbali za ujasiliamali na uzalishaji wa kisasa katika sekta ya kilimo.
Wananchi mnahamasishwa kufika Kyakailabwa na kutembelea mabanda ili kujionea na kujifunza tekinolojia mbalimbali za uzalishaji wa mazao wenye tija. Wananchi pia na wafanya kazi mtapata nafasi ya kupata elimu juu ya usindikaji mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi kutoka kwa wataalam mbalimbali ili wananchi kujikwamua kutoka katika kilimo kisichokuwa na tija.
Aidha Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe. Anathory Amani akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo aliwasistiza wakulima kuwatumia wataalam waliopo katika kuboresha kilimo na kuwa walimu wa wakulima wenzao ili kuinuana kwa kuzalisha kwa wingi.
Pia Mhe. Amani aliwasihi wananchi kuacha dhana potofu kuwa mbolea za viwandani zinaharibu ardhi bali aliwashauri kuwa na utaratibu wa kulima sehemu ndogo itakayokuwa na uzalishaji wenye tija ili kukabiliana na gharama kubwa ya mbolea kuliko kulima sehemu kubwa isiyokuwa na uzalishaji wenye tija.
Maonesho ya NANE NANE 2012 Mkoa wa Kagera yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo wadau mbalimbali kama Sekta binafsi, Taasisi mbalimbali za serikali na zisizokuwa za Serikali, wafanyabiashara ndogo ndogo na wakubwa, wakulima na wafugaji wanashiriki katika maenesho hayo yenye hamasa kubwa. “Kilimo kwanza, zalisha kisayansi na teknolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu.”
Imetolewa na:
Sylvester Raphael,
Afisa Habari Mkoa,
KAGERA.