PATO LA TAIFA LA TANZANIA LAKUA kwa 7.1%
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea hali ya Ukuaji wa Pato la Taifa kwa 7.1% katika kipindi cha robo mwaka 2012
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya hali ya uchumi nchini na kufafanua kuwa pato la taifa la Tanzania limekua kwa asilimia 7.1 katika kipindi cha robo ya mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 6.1 za mwaka jana.
Ukuaji huo wa asilimia 7.1 unatokana na ongezeko la uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi na zile za utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa lengo la utoaji wa taarifa hizo kwa vipindi vifupi vya vya robo mwaka unalenga kuwapatia wadau wa Takwimu za Pato la Taifa uwezo wa kutathmini mabadiliko ya ukuaji wa uchumi nchini.
Na. Aron Msigwa