Bukobawadau

WANAMASUMBWI KAGERA KUPATA UFADHILI –BFT

Mama Kipingu Akiongea na Wanafunzi Shule ya Sekondari Rugambwa na Kuwahamasisha Kujiunga Mchezo wa Ngumi (Masumbwi)

 Wasichana Baada ya Kuhamasika Wakiamsha Mikono Juu Baada ya Kuulizwa Ambao watakuwa Tayari Kujiunga na Mchezo wa Masumbwi.
 Mama Kipingu (Mwenye Track Suit Ya Njano) Akiwa Katika Ofisi ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Rugambwa.
 Mama Kipingu Akiagana na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Rugambwa Baada ya Kumaliza Kazi yake.
 Picha ya Pamoja  Mama Kipingu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Rugambwa.

Wanamichezo wa mchezo wa Ngumi (Masumbwi) Mkoa wa Kagera hasa watoto wa kike wenye kipaji cha mchezo huo neema kwao yaja ya kuendeleza na kuinua vipaji vyao.

Matumaini ya kupata neema hiyo katika Mkoa wa Kagera imeoneshwa na Mama Zuena ambaye ni Mke wa Kanali Mstaafu Idd Kipingu ambaye ni Mwakilishi wa Wanawake Maendeleo ya Vijana, Ajira kwa Wachezaji  Shirikisho la Ngumi Tanzania.

Mama Kipingu ameamua kutafuta na kuhamasisha  vipaji kwa mchezo wa Ngumi (Masumbwi) hasa hasa kwa akina mama na watoto wa kike walioko shuleni na ameanzia mkoa wa Kagera baada ya kuambiwa kuwa hapa mkoani anaweza kupata wachezaji wazuri kutokana na hiostoria ya Mkoa wa Kagera katika Masumbwi.

Baada ya kufika katika Mkoa wa Kagera alikwenda moja kwa moja katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Rugambwa ili kuuhamasisha mchezo huo ambapo wanafunzi wa shule hiyo walihamasika sana na mchezo huo na kuonesha nia ya kujifunza kama watapata vifaa.

Mama Kipingu aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa anatarajia kuwatumia vifaa vya mchezo huo ili kuanza kufunzwa masumbwi na baadae wapatikane wawakilishi kutoka mkoa wa Kagera na washiriki kitaifa. Pia alitembelea na Wilaya ya Karagwe na kuhamasisha masumbwi.

Aidha Mama Kipingu alikili kuwa tatizo kubwa katika michezo ni mikoa kuachwa bila kutembelewa na kutafuta vipaji isipokuwa wanaangaliwa tu wale walioko   Dar es Salaam na mikoa ya jirani, lakini mikoa mingine inaachwa. “Ili kuondokana na tatizo hilo tumeamua kuitembelea mikoa na kuhamasisha mchezo huu.” Alisistiza Mama Kipingu.

Wanamichezo wale wote wanaopenda  mchezo wa Masumbwi Mkoa wa Kagera wa Kike na Kiume wanaombwa kuja kwa Afisa Michezo Katika Mkoa wa Kagera ili watambuliwe kwa ajili ya kupatiwa vifaa na kuweka utaratibu wa kufundishwa na kufanya mazoezi ya mchezo huo na watafaidika na ufadhili huo toka Shirikisho la Ngumi Tanzania.

Imetolewa na:
Sylvester Raphael,
Afisa Habari Mkoa,
KAGERA.
Next Post Previous Post
Bukobawadau