Bukobawadau

KILIO CHA MDAU KATIKA MOJA YA MITANDAO YA KIJAMII AKIELEZA KUWA ANA MCHUMBA LAKINI KWAO AMEAMBIWA NI WACHAWI,HIVYO ANAHITAJI USHAURI WAKO!!

 “Ndugu wana Jf (Jamii Forum), najitokeza leo, naombeni ushauri wenu, nimepata mchumba ambaye ni mzuri, mpole na tunaependana sana.
LAKINI tatizo nina taarifa kutoka kwa wazee, kuwa kwao ni wachawi. NAOMBENI ushauri wenu, najaribu kumwacha nashindwa maana nampenda, nisaidieni”.
Anaendelea kwa kusema kuwa, “walionipa taarifa ni wazee ambao wanaijua familia yao yaani watu wa pembeni ya huo ukoo na si wazee wa upande wangu. Kuhusu ulokole, wazee wangu msimamo wa dini ni wa wastani”.
Kabla sijasimulia kisa kifupi nilichoelezwa na mmoja wa wasomaji kuhusu kisanga kinachofanana na hofu aliyo nayo jamaa kuhusu wazazi wa binti anayemchumbia, sikia maoni na ushauri waliotoa wachangiaji wa awali. Bado maoni yanakaribishwa kuhusu suala hili.
Naam. Sikia ushauri wa wasomaji hawa;
“Maoni yangu ni kuwa asikubali kusikiliza maneno ya watu. Kama yeye anampenda ajaribu kufuatilia kwa kina na kumtegemea Mungu zaidi. Mimi Joseph kutoka Dar”.
Mwingine anasema, “…Anti mie niko tofauti na hao wengine. Kama huyo binti kwao ni wachawi, asiangalie mapenzi ya mwanzoni tu, afikirie mbele itakuwaje. Ujue mwanzo wa mapenzi huwa matamu kama asali. Huoni, husikii?
Mtakapozoeana huwa kama chungwa na pindi mkikosana huwa kama shubiri. Hapo sasa atataka ushauri kwa wazazi ambao mmeshaambiwa ni wachawi. Pia lingine haoni kuwa watatofautiana na wenzake kiimani mchawi/mlokole. Aangalie hayo ndio aamue.(mama Lulu, Kitunda)”.
…Mwingine anasema, “napenda nichangie kama ifuatavyo. Yaani namwambia huyo kijana kwenye mapenzi ya kweli kuna mitihani mikubwa mno bila kuwa na msimamo utajikuta unahangaika kila siku.
Mimi mwenyewe nilikuwa nina mchumba na ndugu zangu walikuwa wakinisihi kila siku nimwache kwani kwao ni wachawi. Lakini miaka yote tisa niliyoishi naye sikuuona ubaya wake wala huo uchawi na mpaka sasa tuna mtoto. Asimwache. (Jane wa Dar).
Baada ya makala ile, alinifuata jamaa mmoja ofisini na kunieleza kisa chake ambapo alionyesha dhahiri kuwa ingawa alijitahidi kuondokana na dhana ya uchawi iliyokuwa ikielezwa upande wa wakwe zake(wazazi wa mke), lakini baadaye alikuja kuamini baada ya kumfuma mkewe akimwekea dawa chini ya godoro.
Anasema yupo mwanadada mmoja alimpenda sana na kuamua kumuoa. Wazazi wa mkewe huyu waliishi kijijini lakini wazazi wa kijana walikuwa mjini ambako ndiko jamaa huyu alikuwa akiishi.
Baada ya kuoana walikaa kwa muda na wazazi wa kijana ndipo baadaye wakahamia kwenye nyumba yao waliyojenga. Anasema kabla ya kuoa alitahadharishwa kuwa wazazi wa mchumba wake walikuwa ni wachawi kule kijijini na waliogopwa sana.
“lakini mimi sikujali kwani nilijua nikishamuoa mke wangu sitaishi naye kule kujijini bali nirtakuwa naye mjini kwa wazazi wangu ambao ni wacha Mungu wazuri.
Nilifunga ndoa ya nguvu na pande zote mbili zilifurahi. Lakini bado katika hisia zangu nilikuwa nawazia zile taarifa kwamba wakwe zangu ni wachawi.
Hata nilipokuwa nao hofu ilikuwa haniishi ingawa nilikazania sana maombi kama ambavyo wazazi wangu walikuwa wananishauri kila wakati kwamba nimtangulie Mungu mbele katika kila jambo.
Nilibahatika kuwa na watoto wawili wa kile. Tokea nipate taarifa za uchawi nimekuwa nikimwangalia kwa karibu mke wangu nione kama zipo dalili zozote zinazoashiria kujihusisha na mambo ya ushirikina.
Takriban miezi mitatu iliyopita nilianza kumwona mkewa wangu tofauti hasa baada ya kurejea kutoka kwao ambako alikwenda likizo pamoja na watoto wetu.
Mara mbili nimezinduka usingizini simkuti kitandani na ninapomtafuta, mara ya kwanza nilimkuta jikoni akikoroga dawa fulani ya kienyeji akasingizia kuwa ni dawa ya tumbo alipewa kwao wakati akiwa likizo.
Nilipomwambia ainywe akadai alishakunywa ile ilikuwa imebakia, ni chungu. Nikarudi kulala naye akanifuata.
Mara nyingine nilizinduka lakini safari hii nilikuta akiweka dawa iliyofungwa chini ya godoro. Wakati ananyanyua nikasikia na kufumbua macho nikamkuta.
Safari hii hakuwa na ujanja, nikambana anieleze dawa ile ilikuwa ya nini na kwanini aniwekee chini ya godoro upande wangu.
Alianza kutetemeka na kuomba msamaha. Nikaichukua dawa ile na kumweleza bayana kula lazima suala hilo lijulikane kwa wazazi wote katika kikao nitakachoitisha.
Tokea siku ile niliamini kuwa kweli taarifa za uchawi katika familia ile ni za kweli. Ilibidi nichukue dawa ile kama ushahidi nikaitisha kikao cha washenga na wakwe wa pande zote mbili.
Pale kikaoni niliitoa na mke wangu akaamriwa afungue kilichokuwemo ndani na aeleze kikao dawa ile ilikuwa inalenga kufanya nini chini ya godoro.
Aliishika huku akilengwa machozi na kuomba msamaha huku akiwageukia mara kwa mara wazazi wake, jambo ambalo lilishangaza. Yaani ilikuwa ni mkutano uliotawaliwa na jazba huku upande wa mke wangu ukiapa kuwa hawana uchawi labda bibie alikwenda kununua kwa waganga wa jadi huko mjini.
Mjadala wa suala hili haukuisha na tulikubaliana kukutana tena ili nije na maamuzi  juu ya mke huyu. Hata hivyo, bado najishauri nimwache au la. Je, wadau mnasemaje juu ya hili?”, Ndivyo anavyomaliza kaka huyu akiomba maoni na ushauri.
Mpenzi msomaji wangu, Maisha Ndivyo Yalivyo. Bila shaka umemsikia mwenzetu huyu katika mazingira ambapo alimfuma kabisa mkewe akimwekea dawa chini ya godoro.
Ukiwa tayari kwa maoni, ushauri kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe;  fwingia@gmail.com
Wasalaam.
Next Post Previous Post
Bukobawadau