Bukobawadau

SERIKALI YAZINDUA UTOAJI WA CHANJO MPYA ZA NIMONIA NA KUHARA MKOANI KAGERA

   wajumbe wa kikao cha Huduma za Afya wakisikiliza kwa makini

 Mwenyekiti wa kikao mkuu wa mkoa Mhe. Massawe akiongea neno




SERIKALI YAZINDUA UTOAJI WA CHANJO MPYA ZA NIMONIA NA KUHARA MKOANI KAGERA
Serikali mkoani Kagera imezindua  na kuweka mikakati ya kutoa chanjo mpya za Nimonia (kichomi) na Kuhara (Rotavirus) kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja ili kudhibiti madhara yanayotokana na magonjwa hayo ambayo hayakuwa na chanjo hapo awali.

Mikakati  hiyo iliwekwa na wajumbe wa kikao cha Huduma za Afya za Msingi mkoa wa Kagera kilichofanyika jana tarehe 28/11/2012 katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa na kuongozwa na Mhe. Massawe Mwenyekiti wa kikao hicho.
Katika ufunguzi wa kikao hicho Mhe. Massawe alisema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kutoa chanjo za kuwakinga watoto na akina mama na magonjwa mbalimbali kama kifua kikuu, Polio, Surua, Dondakoo, Kifadro, na  Homa ya inni.
Magonjwa ya Nimonia na Kuhara  ambayo hayakuwa na chanjo hapo awali sasa chanjo yake imepatikana na  serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  itatoa chanjo hizo Januari 2013. Watoto wanaotarajiwa kuchanjwa mkoa wa Kagera ni 100,836 pia chanjo zitatolewa Tanzania nzima.
Mkuu wa Mkoa alisistiza kuwa chanjo hizo za Nimonia na Kuhara zitapunguza vifo vya watoto na akina mama katika mkoa wa Kagera na Tanzania nzima ambapo alitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote kuwahamasisha wananchi kuwapeleka watoto ili wakachanjwe muda utakapofika Januari 2013.
Mhe. Masswe alitoa agizo kwa Halmashauri zote za mkoa wa Kagera kuhakikisha zinasimamia sheria ndogo  kwa wazazi na wananchi watakaokataa kuwapeleka watoto wakachanjwe na kwa Halmashauri  zisizokuwa na sheria ndogo zitunge sheria hizo na kuzisimamia ili chanjo ifanikiwe kwa asilimia 100%.
Katika chanjo ambazo zilitolewa mwaka 2011 mkoa wa Kagera zilifanikiwa kwa asilimia 87%, mwaka huu 2012 asilimia 88.6% hii ni chini yakiwango cha kitaifa asilimia 95%. Ambapo Mratibu wa Chanjo mkoa wa Kagera Bw. Jackson Minja alisema mkoa umejipanga kutoa chanjo za Nimonia na Kuhara kwa asilimia 100%.
Mkoa wa Kagera una jumla ya vituo 315 vya kutolea huduma za afya zikiwemo Hospitali 15, Vituo vya afya 32, na Zahanati 268 ambapo watumishi wa afya ni 665 asilimia 50% ya watumishi  wote wanaohitajika na upungufu ni watumishi 3186 ambapo mkoa na Halmashauri za wilaya zinaendelea kuomba vibali vya ajira kuajiri watumishi wanaohitajika.
Imetolewa Na; Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa
KAGERA @2012
Next Post Previous Post
Bukobawadau