SOMA MAONI YA MDAU JUU YA SIASA ZA BUKOBA NA MH. KAGASHEKI
Kwa bahati mbaya Mh. Balozi
Kagasheki MB, alipohutubia maelfu ya wakazi wa jimbo analoliongoza la Bukoba
mjini, alijisahau kwamba siku hizi dunia ni kijiji na hivyo hotuba yake
ingeliweza kusikiizwa na kufuatiliwa kutoka kila pembe ya dunia tena ndani ya muda
mfupi sana. Inawezekana kabisa kwa kulisahau hilo alijiaminisha kuwa
amesikilizwa na watu ambao kwa bahati mbaya sana na wakiwa ni wahanga wa mfumo
wa uongozi wetu, hawana uwezo wa kuisikiliza na kuichambua hotuba yake na
kumuelewa zaidi ya yale aliyokuwa akiyatamka.
Mheshimiwa hakujua kuwa, Tanzania
ya leo siyo ile ya zamani, upashanaji habari ni mkuwa sana. Tumemsoma kwenye
magazeti na hata kukusikiliza yote uliyoyaongea. Baada ya kuisikiliza video ya hotuba
yake, nimegundua mambo kadhaa ambayo ninapenda kuwashirikisha wadau:
i.
Ameonyesha mfano mbaya kwa jamii, kuitisha
mkutano wa hadhara kwa ajili ya kumshambulia na kumdhalilisha Meya wa Manispaa
ya Bukoba. Kumwambia mtu hodari wa siasa kama Mh. Amani kwamba yeye ndiye
umemchonga ni dharau kubwa sana. Wengi tunao uhakika kuwa kama ni siasa, Mh.
Amani ni mwanasiasa wa siku nyingi ambaye amekwisha wahi kuwa Mwenyekiti wa CCM
mkoa wa kagera, miaka ya mwisho ya 90 mpaka mwaka 2000. Anafahamu fika kwamba
hawachezi katika ligi moja kwenye uwanja wa siasa. Hivyo inawezekana tu
alimshawihi na pengine kumpa uwezeshaji wa kifedha lakini siyo kumchonga! Na
alikiri kuwa alimuona kuwa anao uwezo wa kusukuma maendeleo.
ii.
Kumbe alitaka baada ya kuwa amemsaidia katika
yote mpaka akawa meya, basi Mh. Amani awepo tu na asifanye lolote la kusukuma
maendeleo, mbona sasa haeleweki huyu Mh. Kagasheki!
iii.
Miradi yote ambayo Mh. Amani ameipa msukumo
hakuianzisha yeye na wala hajawahi kulidai hilo. Ni miradi iliyofanyiwa maamuzi
na kuidhinishwa na mabaraza ya madiwani katika miaka ya nyuma wakati wa uongozi
wa mzee Luhangisa, ambaye kwa kipindi chote cha uongozi wake tuliishuhudia
Bukoba ikidumaa na kubaki kuwa kama pimbi katika kila eneo. Mh. Amani
alichokifanya wakati wake ni uhodari na ujasiri wa kuweka mikakati na
kuisimamia kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa. Hata Mh. Kagasheki amekiri
kuwa mradi wa soko ni moja kati ya mipango aliyoahidi lakini je amefanya
jitihada gani ili kufanya utekelezaji? Kuwa na mipango bila kuwa na mbinu za
kuitekeleza haina maana yoyote.
iv.
Mh. Kagasheki, amedhihirisha kuwa yeye alitoa tu
ahadi lakini hakuwa na uwezo wa kuzitekeleza. Hakujua ni nini la kufanya ili
hiyo mipango iweze kutekelezeka. Kwa bahati mbaya mamlaka yenye uwezo wa
kutekeleza miradi ni manispaa kupitia kwenye baraza la madiwani. Kwa kuwa Mh.
Kagasheki hakuwa anahudhuria vikao vya baraza la madiwani ni dhahiri yeye
aliisha jiweka kando na mipango ya Bukoba. Sasa ameonja uwaziri kamili, ndiyo
anakumbuka kuwa oh, kumbe yeye ni mbunge! Na siyo siri miradi yote ikitekelezwa
na hata isipotekelezwa aliyeikwamisha tumekwisha mjua. Kajitangaza hadharani ni
Mh. Kagasheki.
v.
Kwa aliyoyasema mwenyewe wakati wa mkutano wake
ni dhahiri kuwa Mh. Kagasheki, hapingi utekelezaji wa miradi hasa ule wa soko
bali anahofia utekelezwaji wa mradi huo utampatia sifa lukuki Mh. Amani, kwani
ni juhudi zake zilizowezesha kupatikana kwa taasisi ya kutoa mkopo kwa ajili ya
huo mradi. Ukweli ambao Mh. Kagasheki aliukwepa kuuweka wazi japo anaufahamu
kama msomi na mtu ambaye kwa bahati nzuri ameishi kwa sehemu kubwa ya maisha
yake katika nchi zilizoendelea, ni kwamba miradi yote ambayo Mh. Amani, Baraza
la madiwani na uongozi wa manispaa wameipa kipaumbele, ni miradi yenye uwezo wa
kujiendesha. Soko ni mradi wenye vyanzo imara vya kuzalisha fedha kwa ajili ya
manispaa, alikadhalika mradi wa stendi na ule wa viwanja elfu tano, yote ni
miradi ambayo inao uwezo wa kutengeneza fedha na ikajilipa. Ndiyo maana wameweza
kuiuza miradi hiyo na ikaonyesha kuwavutia taasisi za kutoa mikopo na wawekezaji.
Na hilo ndilo ambalo Mh. Kagasheki hakutaka kuueleza umma kwa nia na lengo la
kupotosha ukweli.
vi.
CHADEMA katika mkutano wao kesho yake, kama ilivyoandikwa
kwenye gazeti la Tanzania Daima la leo (27 Novemba 2012) kwamba Mh. Kagasheki
anachochea vurugu na hilo liko wazi. Mkutano wake wa juzi ilikuwa ni
kuwachochea wanachi wamchukie Meya wao ili wamuone kama mtu asiyefaa. Inasikitisha
kwa mbunge kufundwa na viongozi wa CHADEMA wa ngazi ya wilaya. Na bado
wakaonyesha kuwa wao hawapingi mradi wa soko bali walisimamia kuhakikisha
wafanyabiashara wajulikane wanahamishiwa wapi. Katika gazeti la Tanzania Daima
la jana (26 Novemba 2012) ililipotiwa kwamba katika kikao cha Baraza la
madiwani ambacho Mh. Kagasheki alihudhuria, taarifa iliyotolewa ni kwamba
mipango ya kuwahamisha wafanyabiashara kwenye eneo la soko la muda inaendelea
vizuri. Yeye mwenyewe katika hotuba yake hili kalisema. Pi suala la utafiti wa
udongo na meza ya maji pia alikiri kuwa kikao kilitaarifiwa kuwa limo mbioni
kufanyika. Je, kama siyo kuwa Mh. Kagasheki anapinga mradi kwa sababu zake na
uroho wa madaraka ni nini?
vii.
Madai yake ya kutoshirikishwa katika maamuzi ya
Manispaa hayana msingi na ni uongo mtupu, kwani yeye ni Diwani kwa mujibu wa
sheria kwa hiyo anapaswa ki-kanuni kuhudhuria vikao vyote vya Baraza la
ma-diwani. yeye amekuwa Naibu waziri na baadaye Waziri kamili, gazeti moja
liliandika kuwa kikao cha wiki iliyopita ndicho kilikuwa cha kwanza kuhudhuria
tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2010. Je, kama alitelekeza wajibu wake wa
kuhudhuria vikao, ni sahihi kwamba Baraza la madiwani lisikutane kumsubiri yeye?
Je, imo katika kanuni za uendeshaji wa mabaraza ya madiwani? Haya ni mapungufu
makubwa sana aliyoyaonyesha!
viii.
Mh. Kagasheki, amedhihirisha kulewa u-waziri na
wala siyo ubunge! Amejipa nguvu ya kuwa na kura ya turufu (VETO) juu ya baraza
la madiwani. Huu ni udhalilishaji wa demokrasia. Alihutubia ule mkutano kama
kwamba yeye ndiye peke yake anayepaswa kuamua juu ya jambo lolote linalohusu
Bukoba. Hii ni dharau kubwa sana! Japo, hili halishangazi maana haya yanatokea
katika majimbo mengi na ndilo chimbuko la migogoro kati ya wabunge na ma meya na
wenyeviti wa ma baraza ya madiwani. Wabunge wamekuwa wakijikuta kwamba siyo
watekelezaji wakuu wa shughuli za Kanseli zao ambako ki-utaratibu maMeya na
wenyeviti ndiyo wenye mamlaka za usimamizi chini ya kanseli zao. Na hivyo
baadhi ya wabunge wenye kutaka kuhodhi nafasi hizo kama inavyojidhihirisha kwa
Mh. Kagasheki wamekuwa wakileta mitafaruku isiyo na sababu.
ix.
Mh. Kagasheki, alitoa orodha ya miradi
aliyoichangia kabla hajawa mbunge. Ninayoikumbuka ni pamoja na shule kule kata
ya Nshambya, kuweka taa za barabarani na kuweka kifusi na zege eneo la wauza
ndizi kwenye soko kuu. Ninampongeza sana kwa kuyafanya hayo yote wakati huo
akiwa anatafuta ubunge na kweli yalimsaidia akaupata. Lakini kwa watu tunaotaka
kuwa na maendeleo makubwa na na endelevu, hatutakiwi kuona kwa kutumia taa ya
baiskeli! Hivi vitu vyote alivyovifanya Mh. Kagasheki, vilikuwa na mtizamo
mdogo, finyu na malengo binafsi zaidi kulio ya umma. Hakuna unaloweza kuliweka katika
mzani pamoja na miradi mikubwa inayosukumwa na Mh. Amani, Kanseli na uongozi wa
manispaa! Mh. Kagasheki analeta mzaha wa wazi katika hili. Je, tangu awe
mbunge, ni lipi la ubunifu na lenye mtizamo mpana na wa muda mrefu ambalo
amelifanya katika jimbo? Kusaidia wafiwa na wagonjwa, na kutoa michango kwenye
vikundi vya akina mama ni mambo ya kupita tu (hand outs). Tuonyeshe mradi wa
shilingi bilioni mbili tu! Kagasheki ameshindwa kuelezea manufaa ya kuwa na
miradi mikubwa kama hiyo inayoingiza pesa nyingi katika eneo dogo kama la
Bukoba na mguso (effects) wake katika hali nzima ya jamii na unchumi wa eneo,
hususan kuleta ajira na kuongeza mzunguko wa pesa hivyo kupunguza umaskini wa
kipato. Amelifanya hilo makusudi lakini anachowakosesha watu wa Bukoba ndicho
ambacho hawakijui, kwamba kutekelezwa kwa miradi mingi katika eno fulani ndiyo
neema. Bukoba imekuwa nyuma sana kwa kuvutia miradi mikubwa na hivyo kuyakosa
hayo manufaa, ndiyo maana umasikini unazidi kuongezeka siku hadi siku.
Kagasheki, kama kiongozi angelitegemewa awe mtu wa mwishio kufanya jambo lolote
linaloweza kuichelewesha au kuikwamisha hiyo miradi.
x.
Kagasheki ni mtu mwenye husuda, anayafanya hayo
kwa kuhofia kuwa miradi hasa wa soko kwa sababu una mguso kwa idadi kubwa ya
wapiga kura japo siyo wengi na hata wangelikuwa wengi maendeleo yamekuwa na
tabia ya kuleta maumivu kabla ya kuleta faraja. Kagasheki analifahamu vyema
hilo. Anapozungumzia mradi wa kiwanja cha ndege japo anajipatia sifa zisizo za
kwake kwani huo mradi ulikuwemo kwenye mipango ya serikali kabla hata hajawa
mbunge. Lakini pamoja na hayo, aliusemea
bungeni baada ya kuwa mbunge hadi kuufanikisha, na hiyo ndiyo sifa
anayoistahili pamoja na kwamba haikuwa na ubunifu binafsi. Anakumbuka vyema
suala la kufidia nyumba zilizobomolewa kwa ajili ya kuutekeleza mradi huo.
xi.
Mradi wa soko una mazingira tofauti, hakuna suala
la kulipa fidia bali ni utaratibu wa kuwahamisha wapangaji halali kwa muda wa
utekelezaji wa mradi. Hili Kanseli imelizingatia na muda wa mradi ulitajwa
kwenye kikao, kwa mujibu wa hotuba yake, bali yeye hataki uwe huo. Anafurahia
kuwa kuna shauri liko mahakamani, kiasi inatia shaka kama hayuko nyuma ya wale
waliopeleka shauri mahakamani. Kagasheki anadai mradi ukienda vibaya wote
katika nafasi za uongozi watakuwa matatani! Kiongozi unashindwa kutekeleza
jambo la maana kwa kutanguliza hofu ya kushindwa! Hivi Kagasheki anashindwa
kutambua madhara ya kuchelewesha miradi mikubwa kama hii! Miradi mikubwa kama
hiyo kadiri unavyouchelewesha ndivyo unayosababisha gharama za mradi
kuongezeka. Kwa hiyo kwa anayoyafanya Kagasheki, yatatokea mawili, ama kuufanya
mradi kwa gharama kubwa zaidi au kutokuufanya kabisa huo mradi.
xii.
Kwa yote mawili hapo juu, yanamfanya Kagasheki
aonekane ni mbinafsi na mroho wa madaraka kuliko anavyowasingizia wengine. Yupo
tayari mradi usifanyke, ili apate kura za ubabaishaji kwa watu wasioelewa ni
kwa kiasi gani maamuzi yake yamewaathiri kwa kuwanyima fursa ambazo huo mradi
ungelizifungua kama nilivyozigusia hapo juu. Kwa hiyo Kagasheki, anasumbuliwa kufanya
siasa za ghiliba ili awahadae wananchi kwa kutokujua kwao ili wamuone ndiye wa
maana alafu baadaye wamchague tena kuwa mbunge wa Bukoba mjini.
Ninawatahadhalisheni, huyu nia yake na kundi lake la ndugu zake linalomsumbua
Mh. Amani wameingiwa na kasumba ya kwamba wao ndiyo familia bora hapo Bukoba
kwa hiyo wanataka waendelee kuwa wao ndiyo watawala. Huu usultani wana Bukoba
tuukatae. Mtu wa kuwa kiongozi apimwe kwa uwezo wake wa kuongoza kwa manufaa ya
kuleta maendeleo kwa walio wengi na siyo kuwatumia watu wenye mtizamo mdogo
kutokana na kukandamizwa kwao ki-elimu ili kuwatawala kwa maslahi binafsi. Kwa
yale ambayo Mh. Amani ameonyesha kuyasimamia katika kipindi kifupi, katika
kusukuma maendeleo ya Bukoba, anastahili kuungwa mkono na siyo kubezwa, kutukanwa
na kudhalilishwa kama alivyofanya Mh. Kagasheki, ambaye amedhihirisha kukiogopa
kitabu kipya. Bahati mbaya wale ambao Mh. Amani anawatengenezea mustakabali
mzuri wa baadaye ili waweze kuishi na kufanya kazi katika mazingira mazuri
ndiyo hao wasiolifahamu hilo.
xiii.
Wala sitaki nieleweke kwamba ninasema moja kwa
moja kuwa Mh. Amani ndiye moja kwa moja tumfikirie kuwa mbunge wa Bukoba hapo
mwaka 2015 ila ninasisitiza kuwa tuwe na uwezo wa kuupima uongozi wa kwa kazi
zilizofanyika na siyo tu kuendelea kumpa mtu uongozi kwa mazoea. Kagasheki
amekuwa mbunge sasa miaka saba inakwisha ni lipi analoweza kuliweka mezani
tukamuona anafaa kuendelea kuwa mbunge wetu? Wale wote ambao tumechukizwa na
kitendo cha Kagasheki kujionyesha kuwa na uchu wa madaraka kuliko kuleta
maendeleo tusimame kidete kuuelimisha umma wa wale wasiotambua, wamjue ili
waanze kumkataa na uchaguzi ujao tupate mbunge mwingine. Ni kosa kubwa
kuongozwa na mtu mmoja kwa zaidi ya vipindi viwili, anabadilika na kujihisi
yeye ndiye sultani wenu, ndilo chimbuko la kuzorota kwa maendeleo.
Ninayo mengi ya kuandika ila ninaishia hapa.
Nico Mutta
Kimara Temboni
Dar es Salaa, Tanzania
nikodamutta@gmail.com