Bukobawadau

SERIKALI YA MKOA KAGERA YATOA ZAWADI NA HERI YA SIKU KUU ZA NOELI NA MWAKA MPYA KWA WATOTO YATIMA NA WAZEE


Katika kusherekea  Siku Kuu za  Kuzaliwa kwa Kristo Mkombozi na kufunga mwaka 2012 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Massawe akiiwakilisha serikali ya mkoa wa Kagera ametoa zawadi kwa watoto yatima  na Wazee wasiojiweza ili kushiriki na makundi hayo maalum katika kusherekea Siku Kuu hizo.
Mkuu wa Mkoa alitoa  zawadi hizo tarehe 24/12/2012 Ikulu ndogo ya mkoa alisema katika kusherekea Siku Kuu za mwisho wa mwaka serikali inaungana na wananchi wake hasa wale ambao ni makundi maalum ili kusherekea nao ili na wao wajisikie kuwa serikali yao ipo nao katika kuadhimisha Siku Kuu hizo.
Vituo vilivyopata zawadi ni pamoja na vituo vya kulelea watoto yatima ambavyo ni UYACHO Hamgembe, Nusuru Yatima (Kashai), ELCT Tumaini Center (Kyakailabwa), vyote vya Manispaa ya Bukoba. Pia kituo cha kuwatunza wazee Kiilima, na Kituo cha watoto  Yatima Ntoma Halmashauri ya Wilaya Bukoba.
Zawadi zilizotolewa ni pamoja na mchele kilo 100, mafuta  ya  uto lita 20, mbuzi 1, na sukari kilo 50 kwa kila kituo kwa vituo vitano vilivyoainishwa hapo juu na gharama za zawadi hizo jumla ni shilingi 2,000,000/=
Aidha Mhe. Massawe alitumia nafasi hiyo kuwatakia  heri na fanaka za Siku Kuu wananchi wote pia na wageni waliokuja mkoani kusherekea  Siku Kuu hizo za Noeli na mwaka Mpya. Aliwahakikishia wananchi hao kuwa washerekee kwa amani na utulivu na  ulinzi na usalaama umeimarishwa kwa kipindi hiki cha Siku kuu za mwisho wa mwaka.
Pamoja na kutoa heri hizo za Siku Kuu Mhe. Massawe alitoa taadhari kwa wananchi kujiwekea tahadhari katika maeneo yao ya makazi kwani kwa wakati huu kuna majambazi wengi, “Tusiache nyumba zetu bila mtu hata mmoja wakati wa Siku Kuu, pia kuepuka ulevi wa kupindukia na kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kutembea mkono wa kulia kwa watembea kwa miguu badala ya mkono wa kushoto ambapo si rahisi kuona gari linalotoka  nyuma yako.” Alisistiza Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa alihitimisha kwa kusistiza wazazi na wananchi wote wa mkoa wa Kagera kuhakikisha wanawatunza watoto wakati wote wa Sikuu Kuu ili kuepuka watoto wasipatwe na madhara ya kupotea au kugongwa na magari pale watakapoachwa bila uangalizi na wazazi wao.
Next Post Previous Post
Bukobawadau