Bukobawadau

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UWEKEZAJI HALMASHAURI YA MANISPAA YA BUKOBA



Ndugu wananchi hivi majuzi Chama Cha Mapinduzi Mkoa kilitoa maelekezo ya kuwa serikali itoe ufafanuzi juu ya miradi ya uwekezaji inayotekelezwa katika eneo lake.  Aidha Mkuu wa Mkoa  ameniagiza kutoa taarifa hiyo kupitia tamko hili.

Napenda kutoa taarifa ya ufafanuzu kama ifuatavyo:

1.  UTANGULIZI:
Wazo la kuanzisha miradi ya uwekezaji katika Manispaa ya Bukoba, lilitokana na azima ya kuongeza mapato ya Halmashauri kufikia bilioni Nne (4 bilioni) ifikapo  mwaka 2015.  Aidha nguvu hii ya kiuchumi ingewezesha Halmashauri ya Manispaa kufikia ndoto yake ya kupata hadhi ya kuwa Jiji ifikapo au kabla ya mwaka 2020.

Katika kufikia malengo hayo viupaumbele vya Halmashauri, mpango mkakati wa uendelezaji wa mji wa Bukoba wa mwaka   2008 – 2028  ahadi za  Mhe. Mbunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka  2010, ahadi za Rais na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 – vilizingatiwa.

Miradi iliyoainishwa kutekelezwa ni kama ifuatavyo:-
1.            Ujenzi wa Kiteuga Uchumi
2.            Upimaji wa viwanja 5000
3.            Ujenzi wa Stendi ya mabasi Nyanga.
4.            Mradi  wa Kuosha Magari.
5.            Ujenzi wa Soko Kuu.
6.            Uendelezaji makazi Kashai na Miembeni.
7.            Ujenzi wa Chuo cha Ualimu
8.            Ujenzi wa Kituo cha Maarifa (Center of excellency)
9.            Ujenzi wa bwawa la maji kwa ajili ya Utalii

Miradi minne ya mwisho bado ipo katika hatua ya kufikiriwa na hivyo taarifa yangu itajikita katika miradi 5 iliyoanza utekelezaji.


Ili kufanikisha utekelezaji wa  miradi hii tulizingatia ushirikishwaji wa sekta binafsi – (PPP)  kama ilivyo matakwa ya Kisera.  Aidha, kwa  madhumuni ya kuongeza ufanisi katika kufikia malengo tumeingia mikataba  ya makubaliano na Shirika la Mzinga na Kampuni ya Procurement and Technical Service Limited (PTSL). 

Maeneo ya Ushirikiano
1.  Shirika la Mzinga  -  (Mzinga Co operation)
Hili ni Shirika la Jeshi la Wananchi wa Tanzania lililopewa dhamana ya kushirikiana  na taasisi za Serikali katika  masuala ya mchakato wa maendeleo kwa kutoa huduma za kiushauri na kiufundi.  Makao makuu yake yako Morogoro.
                            
2.   Kampuni ya PTSL - (Procurements and Technical Services Ltd)
Hii ni Kampuni iliyoandikishwa chini ya Sheria ya ma kampuni kufanya shughuli za biashara ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kuanzisha na kutafuta mitaji ya shughuli za kibiashara aidha, Kampuni hii imeshiriki katika kuandaa makongamano mbalimbali kama maonesho ya ALAT Taifa na ALAT Mkoa Kagera.  Makao makuu ya Kampuni hii yako Dar es Salaam.

Mchakato wa kuwapata washirika wa maendeleo ulipata baraka za Baraza la Madiwani katika kikao chake cha tarehe 10/5/2011.




A:  KITEGA UCHUMI
Halmashauri imepanga kujenga jengo la Kitega Uchumi lenye ghorofa 10 katika eneo la stendi ya sasa .  Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa baada ya stendi kuhamia Kyakailabwa.

i)   Utekelezaji hadi sasa:
·        Kutafuta Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kuandaa andiko      la awali la maradi.   Halmashauri ilimteua kwa njia ya zabuni “ARCH PLAN INTERNATIONAL” ya Dar es Salaam kufanya kazi hiyo kwa thamani ya TShs. 109 milioni na tayari amelipwa TShs.  milioni 10.
·        Mkandarasi ameshaandaa andiko la awali na kukamirisha  tathimini ya awali inaonesha jengo hilo litagharimu Shilingi bilioni 11.


·        Halmashauri kwa kushirikiana na Mkandarasi Mshauri imewasiliana na NSSF kuhusu uwezekano wa kufadhili mradi huu.

-        NSSF walitaka Halmashauri kupata dhamana ya Serikali, ambapo Serikali ilikubali kuipa Halmashauri Udhamini kwa njia ya “Letter of Comfort” badala ya “Guarantee”.
-        Halmashauri imeshawasilisha uamuzi wa Serikali kwa NSSF na mazungumzo yanaendelea.
Changamoto:
1.      Mwelekeo na mazungumzo na NSSF umepungua kasi, hii inatokana na  NSSF kutopendelea utaratibu wa Letter of Comfort badala ya Guarantee.
2.      Kuchelewa kuhama kwa standi kutoka eneo la sasa kwenda Kyakailabwa.

Ufumbuzi wa Changamoto:
1.      Kuendeleza mazungumzo na NSSF ili waweze kufadhili mradi huo.
2.      Kuendelea kuuza mradi huo kwa wafadhili wengine ili kupata fedha za kutekeleza mradi.
3.      Kuongeza kasi ya kuhamisha standi.

B:  MRADI WA VIWANJA 5000
     Mradi huu ulizaliwa na wazo kutoka kwenye Mpango Mkakati wa      uendelezaji wa mji wa Bukoba wa mwaka 2008 – 2028.

Mpango huo, ulipendekeza upimaji viwanja vya kutosheleza watu 40,000.   Sawa na viwanja 8,000.  Kwa wastani wa watu 5 kwa Kaya.  Katika Kata za Nyanga, Buhembe, Nshambya Kahororo, Kashai, Kitendaguro na Ijuganyondo.

i)   Maandalizi ya awali ya mradi       
·        Halmashauri iliandaa andiko la mradi na kuwasilisha katika Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kupata fedha za kulipa fidia na kupima.  Andiko lilionesha uhitaji wa Shilingi za Kitanzania bilioni 1.6 (TShs. 1.6 bilioni).
·        Kutokana na Halmashauri nyingi kushindwa kurejesha fedha kwenye mfuko wa wizara wa upimaji viwanja, wizara ilishindwa kupata fedha kwa wakati huo kutupatia kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. 
·        Halmashauri ilianza juhudi za kutafuta fedha kutoka vyombo vingine vya fedha ili kutekeleza mradi huo.
·        Katika harakati hizo Halmashauri ilifanikiwa kuingia mkataba wa makubaliano na Mfuko wa Dhamana Tanzanaia (UTT) ili kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.  Mkataba huu upo kwa mfumo wa ushirikiano (joint venture).

Halmashauri iliingia mkataba wa makubaliano na UTT kutekeleza mradi huo mnamo tarehe 20/6/2011.    Aidha, wataalamu wa Halmashauri na wataalamu wa UTT walipitia upya Andiko la Mradi ili kupata uhalisia wa gharama za utekelezaji wa mradi.  Gharama za mradi zilifikia Shilingi za Kitanzania bilioni 2.6 (TShs. 2.6 milioni).

(ii)  Utekelezaji wa Mradi
       Utekelezaji  mradi ulianza baada ya mkataba kusainiwa, kazi  zifuatazo  zimefanyika:-

1.      Kufanya tathmini na kulipa fidia kwa wananchi 1,000 wenye thamani ya Shilingi  bilioni 2.2 (TShs. 2.2 bilioni).
2.      Kupima viwanja 4,898 kwa gharama ya TShs. 290,000,000/=.  Kazi hii imefanywa na Chuo cha Ardhi Morogoro.
3.      Kufungua barabara zenye  urefu wa Km. 54.01 kwa gharama ya TShs. 366,371,818.00.  Kazi hii imefanywa na mkandarasi Kajuna Investment.
4.      Kuuza viwanja ambapo mradi unategemea kupata Shilingi bilioni 8 (TShs. 8 bilioni) ambapo hadi tarehe 27/11/2012 kiasi cha TShs. 3,064,532,000.00 kimekusanywa kutokana na uuzaji wa viwanja na kuwezesha kurejesha UTT Shilingi bilioni 2.54 (TShs. 2.54 bilioni) ambazo ni mtaji mama wa utekelezaji wa mradi.  Fedha zote za mradi zimepokelewa na kuhifadhiwa kwenye akaunti ya pamoja ya mradi  (BMC and UTT) iliyofunguliwa Benki ya Posta.

-       Viwanja vitaendelea kuuzwa hadi Februari, 2013 ambapo tunategemea kufunga mradi  na kugawana faida kwa uwiano wa 60%  (UTT)  na 40% (BMC).

·        WAKATI WA KUUZA VIWANJA
Katika uuzaji viwanja kuna makundi mawili maalumu yaliyowekewa utaratibu mahususi wa kununua viwanja:

1.   Wale wenye maeneo yaliyotwaliwa.
-   Hawa watapata punguzo la Shs. 400,000/=  kwa kiwanja kimoja miongoni mwa viwanja atakavyonunua vyenye ujazo mkubwa (High Density)..

2.   Wale waliochangia gharama  za upimaji zamani.
-   Hawa watapata punguzo la thamani  ya fedha ya sasa itakayo kokotolewa kutokana na mwaka waliochangia na kiasi walichochangia.  Aidha wale ambao hawatakuwa tayari kununua viwanja katika kundi hili watarudishiwa fedha zao kwa thamani ya sasa baada ya kugawa faida kati ya UTT na BMC.

iii)     Changamoto za Mradi
Katika kutekeleza mradi huu tumekabiliana  na changamoto zifuatazo:-
1.    Wakati wa uhamasishaji mradi ulipokelewa kwa muono tofauti katika maeneo ya mradi ambapo tulilazimika kutumia muda mrefu katika uhamasishaji.  Kwa mfano tulilazimika kuahirisha mradi  Kata ya Kitendaguro kwa kuwa jamii haikupokea mradi kwa mtazamo chanya.
2.    Baadhi ya watu kutojitokeza wakati wa kufanya uthamini.
3.    Kuchelewa kulipa fidia kwa baadhi ya watu kutokana na migogoro ya kifamilia.
4.    Upimaji kuvuka eneo lililokadiriwa kulikopelekea wamiliki wa ardhi 280 maeneo yao kutwaliwa na mradi bila kulipwa fidia katika awamu ya kwanza.
5.    Kasi ndogo ya kulipia viwanja iliyopelekea kuongeza muda kulipia viwanja.
6.    Uwepo wa kesi za malalamiko ya fidia kwa baadhi ya maeneo.

     iv)   Ufumbuzi wa Changamoto:
   (1)    Kutafuta fedha kiasi cha TShs. 768,496,379.50 kuwalipa fidia wananchi 280 ambao ardhi yao iliingia kwenye mradi bila matarajio. Mazungumzo yameanza kati ya BMC na UTT yako hatua za mwisho kuona namna bora ya kuwalipa wathirika wa mradi huo.

        (2)   Kuendelea kuhamasisha ununuzi wa viwanja.
            (3) Kuendelea kutoa elimu na  kutatua mgogoro pale  unapojitokeza katika eneo la mradi.

v)    HITIMISHO:
   Ni matumaini ya Halmashauri kuwa malengo ya mradi yatafikiwa.   Kupitia mradi huu Halmashauri inatarajia kupata gawiwo la Shilingi bilioni 2 (TShs. 2 bilioni). aidha, faida ya muda mrefu ya mradi huu ni kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri kupitia 20% ya Kodi ya ardhi na kodi ya  majengo (property tax).

C:  UJENZI WA KITUO CHA MABASI
Halmashauri katika kuboresha huduma ya usafiri wa mabasi na kupambana  na changamoto ya kuwa na kituo kidogo cha mabasi (kisichokidhi mahitaji) imeamua kujenga kituo kipya cha mabasi katika eneo la Kyakailabwa  Kata ya Nyanga.

i)   Shughuli zilizofanyika:
·        Kuainisha eneo la mradi.  Eneo lina ukubwa wa mita mraba 91,200
·        Kulipa fidia kwa wamiliki 8 ambao ardhi yao ilitwaliwa, ambapo jumla ya Shilingi za Kitanzania milioni 22 zimelipwa.
·        Kusafisha eneo na kujaza kifusi katika eneo la ujenzi kwa gharama ya  Shilingi za Kitanzania milioni 134 (TShs. 134milioni).
·        Kushirikiana na Mzinga Co operation kuandaa Andiko la Mradi, ambapo ujenzi wa kituo cha kisasa utakaojumuisha eneo la kupaki mabasi, eneo la kuegesha malori, Kituo cha mafuta, jengo la kupumzikia wasafiri, Super market, jengo la kukatia ticket, Utawala  na majengo mawili ya vitega uchumi ni sehemu ya mradi tarajiwa.

Kwa kushirikiana na Shirika la Mzinga Halmashauri inaendelea na mazungumzo na UTT kuomba kufadhili mradi huu.  Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Uzio, ujenzi wa eneo la kupaki mabasi na malori, jengo la kukatishia ticketi, jengo la kupumzikia wasafiri na Vyoo.  Aidha, Shirika la Mzinga  watajenga Supermarket.  Makadirio ya mradi huu (phase 1) ni TShs. bilioni 5 bila kuhusisha gharama ya Supermarket itakayojengwa na Shirika la Mzinga.

Changamoto
i)             Kuwepo kwa kesi mahakamani ya wananchi wawili waliyokataa kuchukua fidia.
ii)           Kupata wabia katika utekelezaji  wa mradi ambao ni mkubwa wa wenye kukadiriwa Shilingi bilioni 26 (TShs. 26 bilioni).
iii)          Maboresho ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kyakailabwa kwenda Buhembe ambayo ni barabara muhimu kuingia stendi mpya.

Ufumbuzi wa Changamoto:
(i)      Kuomba kesi isikilizwe nje ya Mahakama na wadai wamekubali    kufanya hivyo.
(ii)    Kuendelea kuiomba serikali kutekeleza ahadi ya Rais ya kujenga barabara ya Kyakairabwa kwa kiwango cha Lami.
(iii)    Tunatarajia kwamba kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi (Phase I) kutakuwa chachu ya kushawishi wafadhili weingine kujitokeza.

HITIMISHO:
Mradi huu una matumaini ya kutekelezwa na unatarajia kupandisha mapato ya Halmashauri ya stendi kutoka TShs. 156 milioni hadi 1.095 bilioni kwa mwaka. 

D:  MRADI WA KUOSHA MAGARI
Mradi huu umeibuliwa kutokana na ukodishaji wa eneo la Karakana la Halmashauri (Emergent Project).  Mradi huu unahusisha Ubia kati ya halmashauri ya Manispaa na Kampuni ya ACE Chemical Ltd yenye makao makuu Morogoro na tawi lake lipo mjini Bukoba.  Hadi sasa mradi umegharimu TShs. Milioni 297 fedha zote zimetolewa na ACE Chemical Ltd.

Changamoto
1.  Pamoja na kuwa mradi umetekelezwa kwa 75% wenye magari  hawajahamasika kuoshea magari kwenye kituo cha Kisasa.

2.  Kuendelea kuwepo kwa vituo holela vya kuoshea magari.
3.  Mtazamo hasi wa jamii  kuhusu  mradi huo.
4.  Kuchelewa kusaini mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji kutokana na kituo kutokamilika kwa wakati.  Maudhui ya mkataba yanategemea kujulikana gharama halisi za ujenzi wa kituo hiki.  Mkataba utakuwa na sura ya mradi kujilipa na hatimae kubaki mali ya Halmashauri (BOT).

Ufumbuzi wa Changamoto:
1.            Kuendelea kuhamasisha waosha magari kutumia kituo kipya cha kuosha magari.
2.            Kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa ya ajira katika kituo hiki.
3.            BMC na ACE kuendelea kuweka mazingira rafiki kuwezesha kituo kufanya kazi kama ilivyo kusudiwa.

HITIMISHO:
Kupitia mradi huu mapato ya Halmashauri yanatarajia kuongezeka kutoka TShs. Milioni sita hadi milioni 22 kwa mwaka na aidha kuongeza ajira ya vijana.


E:   MRADI WA SOKO
Mradi wa ujenzi wa Soko jipya ni utekelezaji wa moja ya ahadi za Mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.  Aidha,  ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa maeneo ya katikati ya mji kama ilivyo kwenye mpango mkakati wa kuendeleza mji wa Bukoba wa  mwaka 2008 – 2028.

i)  Shughuli zilizokwisha fanyika
·        Halmashauri kwa njia ya zabuni ilimteua Mkandarasi Mshauri OGM kuandaa Andiko la Mradi la awali kwa gharama ya Tshs. 522 milioni.
·        Andiko la awali  na mchoro huo viliwasilishwa na kukubaliwa  kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha tarehe 18/10/2011 kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuuza andiko.
·        Kupitia kwa Mtaalam Mshauri (Promoter) (PTSL) Halmashauri ilifanikiwa kufanya mazungumzo na TIB kuhusu  kufadhili ujenzi wa Soko ambapo mnamo tarehe 16/04/2012 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ulisainiwa mkataba wa malipo ya Mkandarasi Mshauri  kati ya TIB na BMC. 
·        Aidha Halmashauri iliingia mkataba wa makubaliano  na TIB wa kumtamtaka mkandarasi mshauri atekeleze majukumu yafuatayo:-
·         
(i)                  Kufanya utafiti yakinifu (Feasibility study).
(ii)                 Kutengeneza Business Plan .
(iii)                Kuandaa gharama za mradi (Bill of Quantities)
(iv)               Kuandaa andiko la zabuni (Tenda /document)

Aidha mnamo tarehe 23/4/2012 ulisainiwa mkataba wa Techinical  Assistant Agreement siku hiyo pia  ulisainiwa mkataba wa mkopo wa Shilingi milioni 200 toka TIB kwenda BMC kuwezesha Halmashauri kutekeleza majukumu yake kwenye mkataba wa Technical Assistant Agreement, na kwamba fedha hizo zingetumika kama sehemu ya malipo kwa Mkandarasi  Mshauri  OGM.
Aidha mkataba huu ulikuwa na kipengele cha ruzuku ya TShs. 90 milioni kutoka TIB kwa ajili ya malipo ya  Mkandarasi Mshauri.

·        Mpango Kazi wa Upembuzi yakinifu.
-      Mpango Kazi uliyokubaliwa na pande zote tatu (TIB, BMC na OGM) ulikuwa kwamba andiko la mradi likamilike ifikapo Machi, 2012 tenda itangazwe April, 2012 na iwe imegawiwa June, 2012 na ujenzi wa Soko uanze Septemba, 2012.

           Aidha kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na:

·        Kubainisha maeneo kuhamishia wafanya biashara ambapo maeneo  yaliyobainishwa ni jengo la CCM mkoa, Soko la Nyakanyasi, Machinjiyo  ya zamani, Kashozi Road  na eneo la CCM Miembeni.
·        Kutengeneza michororo na BOQ za uendelezaji wa maeneo hayo, ambapo Shilingi za Kitanzania milioni 212 zitahitajika kukamilisha.
·        Kutafuta fedha za kuwalipa wenye mikataba na Halmashauri ya uendelezaji/ukarabati Sokoni hususani mabucha  takribani Shilingi za Kitanzania milioni 19.
·        Kuorodhesha wafanya biashara watakaohamia maeneo mapya na kuomba nafasi kwenye Soko jipya ambapo fomu 1,297 zimechukuliwa,  kujazwa na zimerejeshwa.

·        Kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ya umuhimu wa kuwa na Soko la kisasa.

   ii)   Changamoto
          1.  Kikundi cha wafanya biashara kufungua kesi  mahakamani.
   -  Kikundi cha wafanya abiashara kilitoa kusudio na   hatimaye kufungua kesi ya kupinga ujenzi wa Soko kwa madai makuu mawili.

a)         Halmashauri isiwahamishe Sokoni hadi imeandaa maeneo mbadala ya  wao kufanyia biashara wakati wa ujenzi.
b)          Au kuwafidia Shilingi za Kitanzania  bilioni 5 (TShs. 5.0 bilioni)

Kesi hii itasikilizwa mwezi Machi na hali hiyo kupunguza kasi ya ujenzi wa Soko.

2. Kuchelewa kwa mkandarasi Mshauri kuchukua vipimo vya udongo kulikopelekea kuchelewa kukamilika kwa Andiko la Mradi. Timu ya Mkandarasi Mshauri iliwasili Bukoba tarehe 25/11/2012 kufanya kazi hiyo, hata hivyo kikundi cha wafanya biashara waliyofunguwa kesi mahakamani  kiliwazuia kufanya kazi hiyo.

3.    Halmashauri kuchelewa kurejesha mkopo TIB wa Shilingi milioni 200 (TShs. 200  milioni) uliyotakiwa kurejeshwa tarehe 31/10/2012 ambapo hadi mwezi Novemba 2012 kiasi cha Shilingi milioni 20 tu  (TShs.20 milioni) zilikuwa zimerejeshwa.

Ufumbuzi wa Changamoto
Halmashauri kutafuta fedha TShs.450 kwa ajili ya:
·        Kulipa  deni la TIB TShs. 200 ambalo limeiva muda wake wa kurejeshwa.

Halmashauri imewasiliana na TPB kukopa fedha hizo ambazo zitarejeshwa kupitia faida ya mradi wa upimaji viwanja.

·        TShs. 250 milioni kwa ajili ya kuboresha  maeneo  ya kuwahamishia  wafanya biashara (TShs. 212 milioni), kurejesha fedha za kimkataba kwa wenye bucha waliyoboresha bucha hizo kwenye Soko linalotarajiwa kuboreshwa.  (TShs. 19m.) na kulipia gharama za GEOTECH Shilingi  milioni 19.

·        Kuendelea na mchakato wa manunuzi kuwapata wakandarasi wa kuboresha maeneo mbadala.

·        Kuendelea kutetea maslahi ya Halmashauri katika kesi iliyoko Mahakama Kuu.

HITIMISHO:
Endapo mradi huu utatekelezwa kama ulivyopangwa mapato ya Halmashauri yatokanayo na Soko yatapanda kutoka wastani wa TShs. Milioni 168 kwa mwaka  hadi bilioni mbili kwa mwaka.  Napenda kusisitiza kwamba Halmashauri haijangia mkataba wa ujenzi wa Soko kwa  sababu mchakato wa upembuzi yakinifu haujatufikisha hatua ya kutangaza zabuni ya ujenzi.

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA


HAMIS J.  KAPUTA
MKURUGENZI WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA BUKOBA
Next Post Previous Post
Bukobawadau