JESHI LA ZIMA MOTO LATOA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO KWA WATUMISHI WA OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
Moto ukiwashwa na Afisa wa Jeshi la Zima Moto Mkoa Kagera Tayari kwa Mafunzo kwa Vitendo
Afisa wa Jeshi la Zima Moto Mkoa Kagera Bw. James Kisaka Akionyesha Mfano Jinsi ya Kuzima Moto Kwenye Chanzo.
Mtumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Akijifunza Kwa Vitendo
Huyu Mama Anaitwa Consolatha Mtumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera Hakubaki Nyuma Katika Mafunzo Hayo
Bw. Richard Kwitega Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Utumishi Akijaribu Kama Mtungi una Gesi ili Akazime Moto, Hiyo ni Hatua ya Kwanza Kabla ya Kuekea Kwenye Chanzo cha Moto
Hawa ni Maafisa Jeshi la Zima Moto Mkoa Kagera Walishiriki Kutoa Mafunzo
Watumishi Wote Wakipata Maelezo ya Mwisho Baada ya Kupata Mafunzo kwa Vitendo.
Jeshi la Zima Moto Mkoani
Kagera laendesha mafunzo ya tahadhari na hatua mbalimbali za kuzima na
kudhibiti moto pale unapokuwa umetokea katika sehemu mbalimbali hasa kwenye
majengo. Mafunzo hayo yametolewa kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kagera leo tarehe 15/01/2013.
Kutokana na watumishi
pamoja na wananchi walio wengi kutokuwa na elimu ya kujikinga au kuzuia moto unapotokea,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera iliona ni vyema kuwapiga msasa watumishi wake ili
kujiweka tayari endapo ajali ya moto inaweza kutokea iwe nyumbani au ofisini
kwa watumishi.
Katika mafunzo hayo
yaliyotolewa kwa nadharia na vitendo yalijikita katika aina za moto, na ni
jinsi gani unaweza kuzima au kuzuia aina hiyo ya moto. Aina hizo za moto ziko
katika madaraja manne ambayo ni daraja A, ni aina ya moto unaotokea kutokana na
uoto wa asili (sold fire).
Daraja B, moto huu hutokana
na mafuta , Daraja C, ni moto unaotokana na gesi, na daraja la mwisho ni
D, moto unaotokana na vyuma vizito
mfano viwandani. Moto unaotokana na uoto wa asili unaweza
kuzimwa na maji aidha madaraja mengine yanaweza kuzimwa na povu, au aina ya poda
kavu (dry powder).
Aina hizi za gesi na poda kavu vinavyotumika kuzimia moto vinahifadhiwa
kwenye vifaa maalum ambavyo hujulikana kama mitungi. Watoa mafunzo kutoka Jeshi la zima
moto Kagera wanashauri mitungi hiyo kufanyiwa ukarabati kila mara baada ya
miezi sita.
Aidha Jeshi hilo lilitoa
ushauri kwa watumishi na wananchi wote kuwa, janga la moto linapotokea katika
majengo, jambo la kwanza ni kuhakikisha wewe mwenyewe kwanza upo salaama pale
king’ora kinapolia kwa ofisi zilizo na ving’ora hivyo na baadae unaweza
kuchukua hatua za kuanza kuzima moto uliotokea.
Mafunzo katika vitendo kwa watumishi na wananchi waliokuwepo katika eneo
la viwanja vya Bukoba Club waliweza kupata wasaa wa kujaribu kwa vitendo kuzima moto na kuuliza maswali mengi
ambayo walikuwa hawana elimu nayo na kupata ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa Jeshi
la Zima Moto.
Tahadhali, Jeshi la Zima
Moto Mkoani Kagera limetoa wito na
tahadhali kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kujikinga na ajali za moto kwa
kutoacha watoto peke yao nyakati za usiku, aidha pia wanannchi walihamasishwa kufunga
vifaa maalum vinavyohisi moto na kutoa
taarifa katika nyumba zao ambapo siyo vya gharama kubwa kama wananchi walio
wengi wanavyodhani.
Na; Sylvester
Raphael
Afisa Habari Mkoa
KAGERA @2013