LEO TENA KATIKA KUENDELEZA MILA NA DESTURI ZA WAHAYA TUNAGUSIA (OKUZILIMA)
Okuzilima ni kitendo kilichohusisha sherehe ya kijamii, ambacho kwacho familia ya wazazi wa bibi harusi ilikusanya kwa njia ya michango (okutweza) na kupeleka mali (kuzilima), hasa mikungu ya ndizi (ebitoke) na vibuyu vya pombe (amalwa), kwa familia ambako binti yao ameolewa (chini ya mwavuli wa kumzawadia binti yao). Ni wazi kwamba mila hii ilikuza na kuimarisha mahusiano mema na maelewano ya upendo baina ya familia mbili zilizooleana.
Aidha, mila hii pia ilisaidia kujenga mshikamano katika jamii pana ya kijiji au ukoo, kwani watu wote walialikwa na kupata fursa ya kushiriki mchakato wa sherehe kwa michango yao ya hali na mali. Kuchangia huko ndiko okutwela, wakati kuchangisha au kuhamasisha michango ni okutweza.