YANGA 3-2 BLACK LEOPARD HIVI NDIVYO ILIVYOKUA UWANJA TAIFA JIONII YA LEO
UTURUKI,
Uturuki, Uturuki, naam hizo ndizo zilikuwa shangwe za mashabiki wa Yanga leo
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuifunga timu ngumu kutoka Afrika
Kusini, Black Leopard katika mchezo wa kirafiki.
Yanga iliyokuwa
kwenye kambi ya mafunzo nchini Uturuki kwa wiki mbili kabla ya kurejea Dar es
Salaam Jumapili iliyopita, imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 jioni hii dhidi ya
timu hiyo inayoshirki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Tegete, mfungaji wa mabao mawili ya Yanga leo |
Hadi mapumziko,
Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake
aliyefufua makali, Jerry John Tegete dakika ya 33.
Tegete, alifunga
bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana
Niyonzima kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Nkosiyaba Xakane na refa
Hashim Abdallah wa Dar es Salaam akatoa adhabu hiyo.
Kipindi cha
pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alifanya mabadiliko, akiwatoa pacha
kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wenye uraia wa Rwanda, Mbuyu
Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwaingiza Simon Msuva,
Juma Abdul na kipa Said Mohamed.
Mabadiliko hayo,
hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya
kwanza tu tangu kuanza kipindi cha pili, lililofungwa kwa kichwa na Humphrey
Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa timu hiyo ya Jangwani na kumtungua kipa
Said Mohamed Kasarama.
Baada ya
kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya
63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi maridadi ya Niyonzima.
Jerry Tegete
aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha pasi ya beki Juma Abdul
na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe za ‘Uturuki, Uturuki’,
kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini Uturuki kwa wiki mbili
zilizopita.
Beki Nadir Haroub
‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la hatari Humphrey Khoza dakika ya 88 na refa akawapa penalti Leopard
ambayo ilikwamishwa kimiani na Rodney Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.
Katika mchezo
huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Said Mohamed dk 46,
Mbuyu Twite/Juma Abdul dk46, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan,
Athumani Iddi ‘Chuji’, Kabange Twite/Simon Msuva dk 46, Frank Domayo, Jerry
Tegete, Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi dk75 na Haruna Niyonzima.
Black Leopard;
Ayunda Mtshati, Ernort Zaga, Nkosiyaba Xakane, Harry Nyirenda, Humphrey Khoza,
Muganga Dyange Jean, Mongezi Bobe, Thomas Madiba/Mhletse Maako, Abbas Amidu,
Edgar Manake/Karabo Tshepe na Rodney RomagalelaMashabiki wa Yanga wakishangilia soka maridadi ya timu yao kwa kuimba Uturuki, Uturuki, Uturuki...