BARUA YA KUJIUZULU KWA PAPA
Wapendwa katika Kristu,
Nimewaita kwenye jumuiko hili si kwa ajili ya kushughulikia masuala yetu matatu tu, lakini pia kuwasilisha kwenu uamuzi ulio muhimu kwa uhai wa Kanisa. Baada ya kujitafiti mara kwa mara mbele ya Mwenyezi Mungu, nimethibitisha kwa yakini kuwa nguvu zangu haziwezi tena kwa upeo, kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Kiti cha Mtakatifu Petro, kutokana na umri kunitupa mkono.
Ninafahamu fika kwamba huduma hii ya upapa, yenye umuhimu na ya asili ya kiroho, inapaswa itumikiwe si kwa maneno na vitendo tu, bali kwa sala na mateso pia.
Hata hivyo, kwa dunia ya leo inayoambatana na mabadiliko ya haraka na inayotikiswa na maswali yenye umuhimu wa kina kwa ajili ya maisha ya imani, na ili kuiongoza mashua ya Mtakatifu Petro na kuihubiri Injili, kunahitajika kwa pamoja nguvu ya kiakili na kimwili, ambayo katika kipindi cha miezi michache iliyopita, imeendelea kupungua kwangu kwa kiwango cha mimi kujitambua kwa ufasaha kwamba, sitaweza vya kutosha kutimiza majukumu ya huduma hii kubwa iliyokabidhiwa kwangu.
Kwa sababu hii na nikitambua uzito wa kitendo hiki, na kwa uhuru wangu wote, ninatangaza rasmi kujitoa kwenye utume wa Askofu wa Roma, Mrithi wa Mtakatifu Petro, niliokabidhiwa na Makardinali Aprili 19, 2005, kwa namna kwamba, kuanzia Februari 28, 2013, saa mbili kamili usiku, Kiti cha Roma, Kiti cha Mtakatifu Petro, kitakuwa wazi na Jopo la Makardinali wenye sifa za kumchagua Papa mpya, itabidi likae kufanya kazi hiyo.
Ndugu zangu katika Kristu, kwa moyo mkunjufu ninawashukuru kwa dhati, kwa mapenzi yenu na kwa kazi zote mlizoniunga mkono katika utume wangu, na ninaomba msamaha kwa kasoro zangu zilizojitokeza nikiwa kwenye Kiti. Na sasa nawaomba tulikabidhi Kanisa chini ya ulinzi wa Mchugaji Mkuu, Bwana wetu Yesu Kristu, na tumwangukie mama yetu Mtakatifu, Bikira Maria ili aweze kuwasaidia Makardinali, pendo lake la kimama katika uchaguzi wa Papa mpya.
Ninatazamia kujitoa kwa moyo mkunjufu kuendelea kulitumikia Kanisa la Mwenyezi Mungu, hapo baadaye baada ya papa mpya kupatikana, kwa maisha ya sala.