Bukobawadau

FAMILIA YA KARUGENDO INATOA SHUKRANI KWA WALE WOTE WALIOSHIRIKI KATIKA KUMUUGUZA MWANAO 'MWOLEKA' MPAKA UMAUTI.

Yametimia! Mtoto wetu mpendwa Mwoleka Christopher Karugendo, ameaga dunia tarehe 20.2.2012 kwenye hospitali ya Muhimbili. Tutampumzisha kwenye nyumba yake ya milele leo jioni 22.2.2013 kwenye makaburi ya Segerea- Dar-es-salaam.

Tumesikitika, tumeumia na kuteswa sana kwa fiko cha mtoto wetu ambaye tulikuwa tumejipanga kumhudumia kwa nguvu zetu na upendo wetu mkubwa. Zaidi ya mwaka mzima tumekuwa kukihangaika na mtoto wetu. Tumejaribu kila njia hadi kumpeleka India, na hospitali mbali mbali, lakini imeshindikana.

Pamoja na kuteswa na kifo hiki cha mtoto wetu, tumeteswa pia na vifo vingi vya watoto tulivyoshuhudia pale Muhimbili. Watoto wanakufa kwa magonjwa yanayotibika kama kuharisha. mtoto wetu pia amekufa kwa ugonjwa kuharisha. Kama taifa hatujafanikiwa kuwa na mpango mzuri wa kuwahudumia watoto. Kwa nini mtoto afe kwa ugonjwa wa kuharisha? Hili limetuumiza sana.

Tunapenda kuwashukuru nyote mlio tusaidia kwa njia moja ama nyingine katika jitihada za kuyaokoa maisha ya Mwoleka. Asante sana, tunawapenda sana, tuendelee kumwombea Mwoleka, ili apumzike kwa amani. Mtoto wetu Mwoleka atadumu moyoni mwetu milele!


 HISTORIA FUPI YA MTOTO MWOLEKA CHRISTOPHER KARUGENDO IKITOLEWA NA   PRIVATUS KARUGENDO
 Mtoto wetu Mwoleka Christopher Karugendo, alizaliwa tarehe 10.3.2012 majira ya saa mbili na nusu za usiku kwenye Hospitali ya Kairuki Dar-es-Salaam. Muda mfupi baada ya kuzaliwa ilibainika kwamba mtoto alikuwa na tatizo la kutokuwa na uwezo wa kunyonya. Tatizo hili liliendelea kuwa kubwa hadi akawa analishwa kwa mpira kupitia puani. Hali hii ilipelekea Mama na mtoto kuendelea kukaa hospitali kwa Kairuki zaidi ya mwezi mmoja.
Katika jitihada za kutaka kuyaokoa maisha ya Mtoto Mwoleka, ulifanyika uamuzi wa kumhamishia Muhimbili. Huko nako Madaktari na manesi walijitahidi kumsaidia mtoto ili aweze kunyonya bila ya mafanikio. Siku zilivyokuwa zikisogea ndivyo matatizo mengine yalianza kujitokeza; shingo la mtoto halikuweza kukaza na mwili nzima ulikuwa hauna nguvu.
Mwezi wa sita 2012, kwa msaada wa ndugu na marafiki, ulifanyika uamuzi wa kumpeleka mtoto Mwoleka India kwa matibabu zaidi. Madaktari na manesi wa Hospitali ya Appolo – Chinai India, walijitahidi kufanya vipimo vya kila aina na hatimaye kugundua kwamba kulikuwa na tone la damu kwenye ubongo wa mtoto. Walituelezea kwamba hilo ndilo tatizo kubwa na ndicho chanzo cha mtoto kushindwa kunyonya na viungo vyake kulegea, na kwamba tatizo hilo litakwisha lenyewe kadri mtoto atakavyoendelea kukua.
Madaktari wa India, walishindwa kutamka jina la Mwoleka, wao walimbatiza mtoto wetu jina la Woleka. Na dada zake wakalifupisha zaidi hadi kuwa Baby Wo. Hivyo mtoto wetu alijulikana kwa wengi kama Baby Wo.
Baada ya kutoka India, tulishuhudia jinsi Mtoto Mwoleka, alivyokuwa akipiga hatua hadi kuacha kulishwa kwa mpira. Tulikuwa tumejipanga kumhudumia mtoto wetu kwa nguvu zetu na upendo wetu wote. Ni bahati mbaya kwamba, lilijitokeza tatizo jingine la kubanwa kifua, na tatizo hili lilimsumbua sana mtoto hadi kufikia kulazwa mara kwa mara Muhimbili. Hata hivyo, madaktari waliweza kumshughulikia vizuri. Kusema kweli tulianza kuwa na matumaini makubwa na kuanza kujipanga kusherehekea siku yake ya kuzaliwa tarehe 10.3.2013.
Bila kutarajia, ukajitokeza ugonjwa mwingine wa kuharisha na mtoto kulazwa Muhimbili. Mtoto wetu aliharisha siku saba bila kukoma na huu ndio ugonjwa ulioyachukua maisha yake tarehe 20.2.2013 majira ya jioni.
Tunawashukuru nyote mliojitahidi kwa njia moja ama nyingine kuyaokoa maisha ya Mtoto wetu. Kwa namna ya pekee tunawashukuru madaktari na manesi wa Hospitali ya Kairuki na Muhimbili, pia madaktari na manesi wa Hospitali ya Appolo –Chenai India bila ya kuwasahau madaktari, manesi na wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke ambao kwa muda wote huo walikuwa bega kwa bega na mfanyakazi mwenzao Dr.Rose Birusya, ambaye ndiye mama wa mtoto Mwoleka.
Tumesikitika, tumeumia na kuteswa sana kwa kifo cha mtoto wetu Baby Wo. Tunaomba Mungu amlaze mahali pema peponi. Amina.
Next Post Previous Post
Bukobawadau