Aliyechoma watoto wake midomo jela miaka 5
Kamanda wa Polisi Morogoro, Faustine Shilogile.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imemhukumu kifungo cha miaka
mitano jela, Jaribu Juma (29), baada ya kupatikana na hatia ya kujeruhi
na kufanya ukatili dhidi ya watoto.
Hukumu hiyo iliyotolewa huku mshtakiwa huyo akiwa hana ndugu hata mmoja
aliyefika mahakamani hapo kushuhudia, imetolewa na Hakimu wa mahakama
hiyo, Godfrey Isaya, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na
mawakili wa Serikali, Sunday Hyera na Akisa Mhando.
Katika shtaka la kwanza la kujeruhi mtoto wa kwanza, mshtakiwa huyo
alihukumiwa kwenda jela miaka minne, vivyo hivyo kwa kosa la pili, la
kujeruhi mtoto wa pili, ambapo amehukumiwa adhabu kama hiyo ya miaka
minne, huku kosa la tatu la ukatili dhidi ya mtoto akihukumiwa kulipa
faini ya shilingi laki tatu, au kwenda jela miaka mitano, na kwa kosa la
nne la ukatili dhidi ya mtoto mwingine, akipewa adhabu kama hiyo.
Hata
hivyo, akifafanua hukumu hizo, Hakimu Isaya alisema kuwa mshtakiwa
akiamua kutumikia adhabu zote kwa kifungo cha jela, adhabu hizo zote
zitakwenda sambamba, hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitano jela, na
kwamba iwapo atalipa faini kwa kosa la tatu na la nne, basi atakwenda
jela miaka minne.
Hakimu Isaya alisema mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 tangu hukumu kutolewa.
Kabla ya kutoa adhabu hizo, alisema mahakama imezingatia kuwa mshtakiwa
ni baba wa watoto hao, na hilo ni kosa lake la kwanza, lakini ni baba
aliyegeuka hatari kwa watoto wake na kujenga malezi na makuzi mabaya
dhidi yao, tabia ambayo sio nzuri kwa wazazi na imekuwa ikijitokeza sana
kwa jamii hivyo haipaswi kuachiwa.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 13, mwaka huu,
ambapo bila halali na kwa kujua kufanya hivyo ni kosa kisheria,
aliwachoma moto midomo watoto wake wawili, Malick Jaribu (5) na Ibrahim
Jaribu (10) baada ya kuwatuhumu kula karanga walizoachiwa kwaajili ya
kuuza.
Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa huyo alizua tafrani mahakamani, baada ya
kugoma kuingia kwenye chumba cha mashtaka kusikiliza hukumu, ambapo
alijiangusha chini na kujigalagaza, jambo lililowalazimu askari polisi
kuingilia kati na kumnyanyua mshtakiwa huyo hadi ndani.
Aidha akijitetea kabla ya kutolewa hukumu hiyo, mshtakiwa huyo aliiomba
mahakama kumuonea huruma kwa vile alikuwa ni baba wa familia, na tegemeo
kwa watoto wake ambao amedumu nao kwa zaidi ya miaka minne sasa, na
kuomba mahakama iwapo itabaini kurudia tena kosa kama hilo, impe adhabu
kali ili iwe fundisho kwake na kwa wengine.
“Mheshimiwa hakimu, sikudhamiria kufanya hivi na ndio maana nimemua
kukiri mbele hya baraza lako tukufu, lakini siwezi kusema mengi,
mahakama itoe tu adhabu itakavyoona ili iwe fundisho kwangu na kwa
wengine,”alisema mshtakiwa huyo ambaye awali aliomba mahakama kumuonea
huruma kwa vile kosa hilo lilikuwa ni la kwanza.
CHANZO:
NIPASHE