GAZETI LA HAHARI LEO; Madaktari Afrika Kusini wagundua madhara zaidi aliyoyapata Kibanda
BUKOBAWADAU
7 Mar, 2013
Madaktari
katika Hospitali ya Millpark, Afrika Kusini wamebaini madhara zaidi
aliyopata Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom
Kibanda kutokana na unyama aliofanyiwa na watu wasiojulikana usiku wa
kuamkia juzi.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni
ya New Habari (2006) Ltd, alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya na
juzi alasiri alisafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Habari zilizopatikana jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na
uongozi wa Tef zinasema madaktari wanaomtibu Kibanda walibaini madhara
zaidi ambayo ni pamoja na kukatika kwa mfupa laini (fizi) unaounganisha
pua na mdomo pamoja na kulegea kwa meno takriban sita.
Taarifa ya
Tef iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena imesema athari hiyo
imesababishwa na nguvu na nyenzo walizotumia watesaji kumng’oa meno...
“Kutokana na hali hiyo ana maumivu makali sana kwenye kinywa chake.”
Kuhusu meno, Meena alisema hayo sita yaliyoelezwa kwamba yamelegea ni
mbali na yale mawili yaliyong’olewa katika tukio la awali.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ya Tef, Kibanda alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu
na baadaye jana jioni, madaktari walikuwa wakitarajiwa kusoma taarifa ya
matokeo ya uchunguzi huo, ili kutafsiri maana ya matokeo yake kisha
kutoa mwelekeo wa nini kinafuata au aina ya tiba inayopaswa kutolewa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006), Hussein Bashe alisema
madaktari walianza kazi hiyo baada ya Kibanda kufikishwa hospitali hapo
juzi usiku.
"Tunashukuru walifika salama, tatizo lilikuwa Uwanja wa
Ndege wa Johannesburg, walichelewa kama saa moja hivi kwa masuala ya
Uhamiaji, lakini baada ya hapo alipelekwa hospitali.”
“Kwa kuwa
alipigwa sindano ya kutuliza maumivu pamoja na usingizi wakati
anaondoka, sasa baada ya kuimarika kiakili, alipelekwa chumba cha
upasuaji kuangalia jinsi gani ya kulihudumia jicho na hicho kilikuwa
kitu cha kwanza na wakati huohuo alianza kufanyiwa uchunguzi ili kujua
ameumizwa kiasi gani.”
Katika hatua nyingine, uongozi wa
Taasisi iitwayo Southern African Investigative Journalism Forum, jana
ulimtembelea Kibanda hospitalini na kueleza masikitiko yake kuhusu
yaliyomkuta.
Uongozi huo uliahidi kushirikiana na taasisi za
kihabari za Tanzania, kuchunguza tukio hilo kwa lengo la kupata majawabu
ya nini kilichojiri na sababu zake.
Leo Tef watakuwa na mkutano wa
wahariri wote kujadili hatua zaidi za kuchukua kwa maana mbili; kwanza
kuhusu matibabu na afya ya Kibanda na pili usalama wa waandishi wa
habari kikazi.
Kibanda alitekwa na watu wasiofahamika ambao
walimshambulia kwa nondo na mapanga na kumng’oa meno mawili, kucha na
kumjeruhi jicho la kushoto usiku wa kuamkia juzi.
BUKOBAWADAU
Bukoba Wadau ni mtandao unao toa habari na matukio yanayo tokea katika mji wa bukoba pamoja na mkoa wa kagera kwa ujumla.
Email:bukobawadau@gmail.com | Phone :Mc baraka:0784 505045, 0754 505043
Instagram @bukobawadau | Facebook @bukobawadau