Hoja ya Nchimbi dhidi ya unyama kwa Kibanda
Na Prudence Karugendo
WAKATI akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani,
DW, kuhusu utete wa usalama unaowakumba wanahabari Tanzania, na kutakiwa ataje
hatua za makusudi zinazochukuliwa na serikali kuwaondolea wanahabari zahama
hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanueli John Nchimbi, alitamka kwa kujiamini
kwamba serikali inalo jukumu la kuhakikisha usalama wa kila raia na si kwa
wanahabari peke yao.
Nchimbi
aliongeza kwamba si kweli kuwa wanahabari ndilo kundi pekee ambalo usalama wake
umegubikwa na utata katika jamii ya Watanzania, akasema mtu akitakiwa kutaja
matukio yanayodhihirisha kuwa usalama wa wanahabari umepotea hayawezi kufika
hata matukio matano. Kwa mtazamo wake mpaka sasa wanahabari wako salama!
Pengine wafe nusu yao ndipo atalipa uzito suala hilo!
Lakini
hatahivyo Nchimbi hakulitaja kundi lingine katika jamii ya Watanzania ambalo
taaluma yake inalifanya kujikuta limepoteza usalama wake kama ilivyo kwa
wanahabari. Maana kwa kuitia uzito hoja yake ya kwamba si wanahabari peke yao
wanaoonekana kupoteza usalama wao kutokana na kuihudumia vilivyo taaluma yao,
angeongeza walau makundi mawili yaliyo katika mkumbo mmoja kama mfano. Pengine
angesema wahandisi au wahasibu. Lakini kushindwa kufanya hivyo ni kama Nchimbi
kakiri kwamba usalama wa wanahabari kwa sasa uko hatarini kama inavyojionyesha.
DW ilimhoji
Nchimbi kufuatia tukio la kinyama la kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, ambaye pia ni mhariri mtendaji wa
Habari Co-operation.
Tukio hilo
ambalo Nchimbi anataka kulijengea hoja ili lionekane ni la kawaida katika jamii
ya Watanzania, limekuja baada ya matukio kadhaa ya mashambulizi yaliyolengwa
kwa makusudi kwa wanahabari. Matukio ya karibuni yakiwa ni pamoja na kuvamiwa
kwa ofisi za gazeti la Mwanahalisi, ambako mhariri mtendaji wa gazeti hilo,
Saidi Kubenea, pamoja na mshauri wa taaluma, Ndimara Tegambwage, walijeruhiwa
na watu wasiojulikana.
Mbali na
tukio hilo likafuatia tukio lingine la kushambuliwa kwa mwanahabari, Daudi
Mwangosi, na watu wanaojulikana, tena wa vyombo vya usalama wa raia, ambapo
mwanahabari huyo aliyekuwa anatekeleza majukumu yake alipoteza maisha baada ya
kulipuliwa na bomu lililoelekezwa tumboni kwake chini ya usimamizi wa Kamanda
wa Polisi wa mkoa Iringa, Michael Kamuhanda.
Baada ya
tukio hilo la kijijini Nyololo, Mfindi, Iringa, likafuatia tukio la mwanahabari
Shabani Matutu kuvamiwa nyumbani kwake, Kuduchi Machimbo, nje kidogo ya jiji la
Dar es salaam, na kikosi cha wanausalama
waliomjeruhi kwa risasi begani kwa visingizio visivyo na mashiko.
Matukio hayo
yasiyolenga kwenye kitu kingine zaidi ya uhai wa mtu tunawezaje kuyachukulia ni
ya kawaida tukiwa tumeyafananisha na matukio ya vibaka?
Tulizoea
ujambazi unaolenga kwenye mali, lakini ujambazi unaolenga tu kwenye uhai wa mtu
tunawezaje kuuita ni wa kawaida? Mali inaweza ikaporwa na ikapatikana nyingine,
lakini uhai unapoporwa unawezaje kupatikana mwingine? Je, Mheshimiwa Nchimbi
tukubali hii ni kawaida?
Na kwa nini
ujambazi huu uchague taaluma? Tuuchukulie unakuja kama ajali, lakini mara zote
ajali hizo ziwakute wanahabari tu! Dukuduku langu lingepungua kama mashambulizi
haya ya kinyama yangekuwa yanaelekezwa kwa watu wa taaluma mbalimbali bila
kuiandama taaluma moja tu.
La muhimu
ninalotaka kukumbusha na kuhoji ni kwamba Waziri Nchimbi anayo dhamana ya mambo
ya ndani ya nchi yetu. Chini yake ndiko kuna Jeshi la Polisi ambalo lipo
kuulinda usalama wa raia, na kwahiyo jeshi hilo likajulikana kwa kifupi kama
Usalama wa Raia.
Kutokana na
kuwepo wa jeshi hilo wananchi wanapaswa kutembea wakijidai bila hofu
wakijivunia uwepo wa jeshi lao hilo. Ndiyo maana wanalipa kodi ili kodi hizo,
pamoja na mambo mengine, zihakikishe chombo hicho kinabaki imara kuwakikishia
usalama wao.
Kwahiyo
kinachotarajiwa na wananchi kutoka kwenye chombo hicho ni habari za kuyazima
matukio yoyote ya uhalifu yanayokuwa yamepangwa kutekelezwa na wahalifu dhidi
ya raia wema na mali zao.
Jambo la
kusikitisha ni kwamba mambo yamekuwa kinyume chake katika siku za karibuni hapa
nchini. Uhalifu limegeuka jambo la kawaida hapa kwetu. Wananchi wanadhurika na
wengine kupoteza mali zao au vyote viwili. Chombo kilichopaswa kuwahakikishia
usalama, wao na mali zao, kinajigeuza
chombo cha kufanya uchunguzi kana kwamba hakihusiki na ulinzi wa usalama!
Kila baada
ya tukio la uhalifu chombo kilichopaswa kuhakikisha uhalifu hautendeki ndicho
kinajipa jukumu la kuchunguza kwa nini uhalifu umetendeka na umetendekaje!
Wakati uhalifu umeishafanyika na madhara yasiyoponyeka yameishatokea, chombo
cha usalama kinahangaika na uchunguzi!
Na yumkini
chombo cha kulinda uhalifu usitokee kinapojigeuza cha kuchunguza, uhalifu unapata mvuto sababu unakuwa hauna
kinga, utafanyika ili baadaye ukachunguzwe.
Swali la
muhimu la kujiuliza ni kwamba Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya kuulinda usalama
wa raia au ni la kufanya uchunguzi kila baada ya usalama wa raia kutibuka?
Je, wananchi
wanapaswa waishi kwa kuutegemea usalama wao na mali zao au kwa kuutegemea
uchunguzi unaofanyika baada ya kuwa wamedhurika? Tulitegemee Jeshi la Polisi
katika lipi? Kuulinda usalama wetu na mali zetu au kutufanyia uchunguzi wakati
baadhi yetu wamepoteza mali na hata maisha?
Absalom
Kibanda ni kijana aliyekuwa buheri wa afya kabla ya usalama wake kuyeyuka na
kujikuta ameangukia mikononi mwa majahili. Kwa sasa tayari afya yake ni mgogoro,
akipona hawezi tena kurudia hali yake ya kawaida, na si ajabu akawa chongo
kulingana na mashambulizi aliyofanyiwa na majahili hayo. Ni jambo linalouma
sana.
Lakini
tunaambiwa kwamba polisi wamejipanga kufanya uchunguzi wa “kufa mtu”! Je, baada
ya uchunguzi huo wa nguvu Kibanda atarudia hali yake ya kawaida? Jicho lake
litapona?
Kilichopaswa
kufanywa na polisi ni kutumia walau moja ya miamoja ya nguvu inayotumika
kufanya uchunguzi ili kuulinda usalama wake, sio kufanya uchunguzi wakati Kibanda
kaishapoteza jicho na meno. Usalama wa raia si kusubiri raia adhurike au afe
kusudi Jeshi la Polisi lionyeshe manjonjo yake katika uchunguzi, kinachopaswa
kuangaliwa ni usalama kwanza. Raia asidhurike wala kufa katika mazingira
yanayoweza kuepusha vitu hivyo.
Mfano,
mwandishi mmoja anayeishi nchini Scotland, majuzi tu katueleza jinsi vyombo vya
usalama vya wenzetu vinavyofanya kazi kwa ufasaha. Vyenyewe vinafanya uchunguzi
kabla ya tukio lenye madhara na kuliepusha.
Alieleza
jinsi polisi walivyokwenda nyumbani kwake alfajiri na kujitambulisha kisha wakamweleza
kuwa anafuatiliwa na watu wasio wema kwake ili akachukue tahadhari. Polisi hao
hawakutaka mtu huyo adhurike kwanza ndipo waanze uchunguzi wa nini kimemsibu.
Kwahiyo hata
hapa kwetu ningetegemea polisi wamfuate Kibanda, au walau kumpigia simu,
kumweleza kuwa usalama wake ulikuwa hatarini kusudi achukue tahadhari. Hapo
ningeamini kwamba vyombo vyetu vya usalama kweli viko kazini na vinaitumia kwa
umakini intelijensia yake kwa manufaa ya wananchi. Lakini sio ile intelijensia
inayotumika tu kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani.
Nimalizie kwa
kukumbusha ya enzi za nyuma. Wakati wanahabari kwa sasa wanaonekana ni maadui
kwa baadhi ya watumishi wa umma hasa walio katika vyombo vya dola, mfano kama
RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda, miaka ya nyuma wanahabari walikuwa vipenzi
vya watu kama hao.
Katika Vita
ya Kagera, 1978 – 79, Jenerali David Msuguri, akiwa Brigedia wakati huo,
aliwapenda sana waandishi wa habari waliokuwa wanaripoti mwenendo wa vita
kutokea uwanja wa mapambano kiasi cha kuwaita makomandoo wake. Hiyo ilitokana na
wanahabri kutaka kufika katika kila eneo la tukio ili wakapate cha kuuhabarisha
umma katika uhalisia wake. Wanahabari walifika hata mahali ambapo askari
hawakuona umuhimu wa kufika zaidi ya kutuma salaamu za makombora. Wanahabari
walifanya hivyo kwa kujitoa mhanga mpaka Msuguri akaona wanafaa kuitwa
makomandoo. Walikuwa wanatimiza jukumu lao kwa moyo mmoja. Ukomandoo huo bado
upo nap engine unaongezeka, lakini je,
kwa nini kwa sasa ukomandoo huo hauthaminiwi?
Nakutakia
kupona kwa haraka ndugu yangu Komandoo Absalom Kibanda, pole sana. Wahaya wanasema
“Bishanga abashaija”, yaani hayo huwakuta wanaume.
0784 989 512