Bukobawadau

KIKAO CHA USHAURI CHA MKOA WA KAGERA CHAPITISHA RASMU YA MGAWANYO WA MALI ZA WILAYA YA KARAGWE NA KYERWA.

Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. Massawe,(Kushoto)  Katibu Tawala Mkoa Mhe. N. Mnambila (Katikati) na Katibu wa CCM Mkoa Bw. Mushi Wakiimba Wimbo wa Mkoa Uliozindiliwa Siku ya Kikao cha Ushauri cha Mkoa.
 Wajumbe wa Kikao cha Ushauri cha Mkoa Kagera Wakiimba kwa Pamoja Wimbo wa Hamasa wa Maendeleo  Mkoa wa Kagera


Serikali katika kuhakikisha inamuudumia mwananchi mpaka ngazi ya chini na kusogeza huduma zote za  kijamii kufikia ngazi ya kitongoji, hatimaye Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Kagera  (RCC) kimebariki rasmi rasmu ya mapendekezo ya mgawanyo wa rasilimali na madeni kati ya Halmashauri ya Karagwe na Kyerwa.
Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika tarehe 15.03.2013 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera kilikuwa maalum kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya mgawanyo wa rasilimali, madeni na  watumishi kati ya  Halmashauri ya Karagwe na Kyerwa  ili yatumwe kwa Waziri Mkuu na Kupitishwa rasmi.
Hapo awali Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ilikuwa imegawanyika katika tarafa tisa na kata 40. Baada ya kutangazwa kwa Wilaya mpya ya Kyerwa mwaka jana 2012 Halmashauri imegawanyika katika Halmashauri mbili Karagwe na Kyerwa.
Halmashauri ya Karagwe itakuwa na tarafa tano ambazo ni Bugene, Nyaishozi, Nyabiyonza, Kituntu na Nyakakika. Kata 22, vijiji 73, vitongoji 737 na idadi ya watu  245,888. Aidha Halmashauri ya Kyerwa itakuwa na tarafa nne ambazo ni Kaisho, Murongo, Mabira na Nkwenda. Kata 18, Vijiji 93, vitongoji 647 na idadi ya watu 240,590.
Mapendekezo ya rasmu ya mgawanyo wa rasilimali, madeni na watumishi ilipitia hatua zote muhimu kwa kuhusisha halmashauri zote mbili ikiwa ni pamoja na kupitishwa katika balaza la Madiwani ambapo madiwani walikubalina kwa pamoja na kupitisha rasmu hiyo bila malumbano na manunguniko yoyote kwa ajili ya hatua za  mbele zaidi.
Wadau wa kikao cha Ushauri cha Mkoa walilipongeza Balaza la Madiwani kwa ukomavu wa siasa ambapo katika hatua zote  za mgawanyo hakukutokea ugomvi  wowote wala kutoelewana. “Nawapongeza Madiwani wa Karagwe kwani nilipokuwa Rorya kulitokea ugonvi mkubwa mpaka watu kujeruhiana.” Alishukuru Mkuu wa Wliya ya Kyerwa Luten Kanali Benedict Kienga.
Mkoa wa kagera una Wilaya saba na Kyerwa ilianzishwa mwaka  2012 baada ya Wilaya ya Chato kuhamishiwa katika mkoa mpya wa Geita  mwaka huo wa 2012. Mwaka 1947 mkoa wa Kagera ukijulikana kama Ziwa Magharibi na  ulikuwa na Wilaya nne tu za kiutawala ambazo ni Biharamuro, Ngara, Karagwe na Bukoba.
Mwaka 1975 Wilaya mpya ya Muleba ilianzishwa kwa kuigawa Wilaya ya Bukoba.  Aidha Wilaya mpya za Chato na Missenyi zilianzishwa mwaka 2007. Wilaya ya Chato ilianzishwa kwa Kuigawa Wilaya ya Biharamulo na Wilaya Missenyi ilianzishwa kwa kigawa Wilaya ya Bukoba.
Baada ya Wilaya ya Kyerwa kugawanywa kutoka Wilaya ya Karagwe mwaka 2012 tayari wilaya hiyo inaye Mkuu wa Wilaya ambaye ni Luten Kanali Benedict K. Kitenga na hivi karibuni serikali ilimteua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya  kuanza kuwahudumia wananchi wa Kyerwa.
Imeandliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI MKOA
KAGERA @ 2013

Next Post Previous Post
Bukobawadau