NDUGU zangu,
Afrika vurugu zetu nyingi zinaanzia kwenye chaguzi. Joseph Stalin wa
Urusi aliwahi kutamka: “Anayepiga kura hana anachoamua, anayehesabu kura
ndiye anayeamua kila kitu.”
Na hapa ndipo lilipo tatizo la msingi. Watu kukosa imani na wenye
kusimamia uhesabuji wa kura zenyewe. Kuna wanaojisikia kuwa kura zao
hazina umuhimu; kwani, mwisho wa yote, kura zitaibwa.
Katika nchi zetu hizi, kukosa imani na wenye kusimamia mchakato wa
uchaguzi hadi kuhesabu kura ndio chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.
Tuliyaona hayo kwa jirani zetu kule Kenya mwaka 2007.
Wakenya wale walishiriki mchakato wa kujiandikisha na hata kupiga kura bila matatizo makubwa.
Kazi ikaja kwenye kuhesabu kura. Ndipo hapo hesabu zikaanza kuwa
ngumu. Kukawa na kufuta hapa na pale. Kukawa na kushinikizana matokeo na
kadhalika. Hatimaye damu ikamwagika.
Kila mwenye kufikiri alielewa kuwa kiini cha vurugu za Kenya ni Tume
ya Uchaguzi ambayo haikuwa huru. Wakenya wale wakajifunza. Leo wana
katiba mpya. Katiba ya watu wa Kenya.
Hivyo basi, tunachojifunza hapa ni kuwa, dawa ya kuepuka au kupunguza
shari kama iliyotokea Kenya ni kwa nchi zetu hizi kuangalia upya katiba
zetu na hususan inapohusu uchaguzi na tume ya uchaguzi.
Na kikubwa kinachosababisha vurugu na watu kuchinjana ni kukosekana kwa imani kwa wenye kusimamia uchaguzi.
Hapa kwetu tuliyaona hata kwenye uchaguzi mdogo wa kule Arumeru.
Mliokuwa kwenye runinga mkiangalia usiku ule wa uchaguzi na kusubiri
matokeo mtakuwa mlikiona pia nilichokiona mimi.
Hakika niliogopa kwamba televisheni inatumika kuendesha propaganda za
kuwaonesha vijana kuwa ni wenye vurugu wakati hatuoneshwi vijana hao
wakifanya vurugu.
Mtangazaji mmoja alipokuwa hewani moja kwa moja cha kwanza kutuambia
ni: “Kuna milio ya risasi inasikika” bila kutuacha watazamaji tuisikie
pia hiyo milio ya risasi.
Ndiyo, kule Arumeru tumeona jinsi baadhi ya vyombo vya habari na
wanahabari wakishiriki kusambaza hofu ya vijana kufanya vurugu bila
kutuonesha vijana wanaofanya vurugu. Bila wanahabari hao kutambua au
labda walitambua wangeweza kabisa kuwa chanzo cha vurugu na hata mauaji.
Jirani zetu Kenya wameshajifunza kutokana na maafa ya uchaguzi wa 2007 yaliyolifika taifa hilo.
Wakenya wamegundua kuwa si tu polisi wanaoweza kuchochea vurugu na mauaji, bali hata wanahabari kama ilivyokuwa mwaka 2007.
Ndiyo maana, kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa juzi, Wakenya
walishaamua, tangu mwaka jana kuendesha mafunzo maalumu kwa wanahabari
watakaoripoti habari za Uchaguzi Mkuu. Lengo kuu hapo ni kuwafanya
wanahabari hao wasijikite kuandika habari za uchochezi na zilizoegemea
kwenye vyama na makundi. Ni hatua sahihi na ya kuigwa.
Na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya yatakuwa kama ‘litmus paper’ - ni
kipimo watakachotumia wakubwa katika mahusiano yao na nchi zetu hizi.
Kama Wakenya watafanya uchaguzi wao kwa amani na matokeo yakatangazwa
na tume huru, rais akaapishwa na shughuli zikaendelea, basi, huenda
matokeo hayo yakaifanya Kenya kuwa ‘ Kaka Mkubwa’ kwa nchi zetu hizi za
Afrika Mashariki na Kati.
Tutakuwa ni watu wa kuambiwa; “Waangalieni wenzenu Wakenya!”
Kila la heri jirani zetu wa Kenya.
|