Mchungaji Moshi ashtakiwa kutorosha watoto
Mchungaji Jean Felix Bamana amefikishwa mahakamani mjini Moshi
kwa tuhuma za kuwatorosha wanafunzi wawili kutoka wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro hadi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka baadaye mchungaji
huyo, ambaye anadaiwa kuwa ni raia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC), alikuwa awasafirishe wanafunzi hao ambao ni ndugu wa familia moja
hadi katika nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Afrika
Kusini ambako aliwaahidi angewatafutia shule katika nchi hizo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi chini ya Hakimu, Naomi
Mwerinde, hata hivyo, ililazimika kuhamia wodi namba moja katika
Hospitali ya Mawenzi alikokuwa amelazwa mchungaji huyo ili kumsomea
mashtaka yake.
Mchungaji huyo, ambaye ni mlemavu wa miguu,
alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa na
kupelekwa Gereza Kuu la Karanga kwa kuwa mashtaka yanayomkabili hayana
dhamana.
Katika shtaka la kwanza, Wakili Majaliwa alidai
kuwa Februari 18 mwaka huu katika Kijiji cha Mbwera Masama wilayani Hai,
Mchungaji Bamana alimtorosha mwanafunzi (jina limehifadhiwa) wa Shule
ya Sekondari ya St. Merigoret hadi jijini Dar es Salaam.
Hali kadhalika katika shtaka la pili, Majaliwa
alidai kuwa Februari 20, mwaka huu katika kijiji hicho cha Mbweera,
mshtakiwa huyo alimtorosha mwanafunzi mwingine (jina limehifadhiwa) wa
Sekondari ya St. Merigoret na kumsafirisha hadi jijini Dar es Salaam.
Baadaye mchungaji huyo alikuwa awasafirishe
wanafunzi hao hadi katika nchi za DRC, Zambia na Afrika Kusini, makosa
yanayoangukia chini ya sheria ya kusafirisha binadamu namba sita ya
mwaka 2008, ambayo hairuhusu dhamana kwa mshtakiwa.
Mchungaji Bamana alikana mashtaka hayo huku
akilalamika kukosa huduma ya choo kwa walemavu katika Hospitali ya
Mawenzi alikolazwa kwa wiki moja baada ya kuugua ghafla magonjwa ya
maambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI) na shinikizo la damu.