Bukobawadau

SIMULIZI LA LEO ADUI USIMLILIE!!

By George Iron

Mama yangu aliwahi kunyanyaswa sana, aliwahi kudharauliwa sana….wakasema maneno mabaya juu yake….wakamsemea familia yake.
Waliomsema walitegemea kuwa atawajibu, au ataanza kulia na kutangaza kwa watu kuwa anaonewa…lakini la…hakuwahi kulalamika.
Lakini alipojifungia ndani akiwa nasi watoto wake alilia sana yaani alikuwa analia kweli.
Siku moja kaka yangu alimuuliza.
“Mama mbona ukiwa nje unacheka tu na watu, kila mara una tabasamu? Ukifika ndani unalia usiku kucha?”
Mama akalazimisha tabasamu kisha akamjibu.
“Najilazimisha kufurahi ili adui yangu atambue kuwa kero zake haziniumizi, maneno yake ni bure kwangu hayaniathiri hata kidogo…..kwa kufanya hivyo mimi nakuwa mshindi na mwisho adui anakosa mbinu za kuniumiza….NALIA mbele yenu maana ninyi mnanifahamu, na hapa muelewe kuwa naumia kweli kweli maneno yao ni makali sana zaidi ya miiba, yananipondaponda moyo na kunikatisha tamaa…lakini sitaki wajue. Wakijua watakutana kupongezana…..sikilizeni wanangu…..MSIJE MKAMPA NAFASI ADUI AKAGUNDUA MADHAIFU YENU…….KAMWEUSILIE MBELE YA ADUI”

Kwa miaka ile sikumuelewa…….ilipita miaka kadhaa nikaingia katika mahusiano ya kimapenzi……baada ya muda mpenzi wangu wa kwanza kabisa tangu nijitambue aliniacha kisa siwezi kumuhudumia..na kweli sikuwa naweza kumuhudumia….nilikuwa maskini……akaamua kuwa na mtu mwingine…..nikayakumbuka maneno ya mama enzi zile….
Kila siku nikawa mtu wa kutabasamu, furaha ikazidi, alijaribu kunionyesha mambo mengi na mpenzi wake mpya lakini sikuonyesha kushtuka.
Kitanda changu na godoro langu pekee vilitambua ni jinsi gani nilikuwa nalia usiku, nililia bila mtu yeyote kuona.
Moyo ulipondeka nikayachukia mapenzi lakini haya yote adui yangu hakuyajua……
Mwisho akajiona mjinga…….akaacha madharau. Na hatimaye waliachana na bwana yule mwenye mbwembwe.
Aliporejea kwangu, moyo wangu ulikuwa umekufa ganzi tayari…..sikumpa nafasi…..sikumpa nafasi kamwe.
Ile hali ya yeye kunibembeleza, moyo nao ukaanza kupona…..
HAKUWAHI KUJUA KAMA NILIWAHI KUMLILIA……AKAWA MJINGA AKANILILIA HADHARANI.
Nilitabasamu na kumsikitikia, natamani angeyajua maneno yale matamu ya mama huyu katika picha…huenda angeyashinda maumivu yake.
Next Post Previous Post
Bukobawadau