Tanzania na Mfano wa Asiyenacho
Na Abraham Byamungu
Biblia inasema mwenye nacho ataongezewa na asiye
nacho hata kile kidogo alichokuwa nacho atanyang’anywa - Mathayo 25:29.
Huu mstari huwatatiza wengi. Wengi hujiuliza,
sasa huyu hana kitu inakuwaje ananyang’anywa kidogo alichokuwa nacho? Kidogo
hicho amekitoa wapi?
Baada ya tafakari ya muda mrefu juu ya neno hili,
Mungu aliweza kunifunulia tafsiri kwamba hakuna hasiye nacho. Kila mtu Mungu
humjalia kwa kadiri anavyostahili; sasa ni juu ya mtu huyo kukitumia vyema kile
alichopewa.
Mfano wa asiyenacho kunyang’anywa ni kwamba huyo
hujiona hana kitu ndipo Mungu mtoaji huamuru basi anyang’anywe hicho
alichonacho kwa sababu ya udanganyifu wake kwa kusema hana kitu. Kinyume chake
kwa yule anayejitambua kwamba anacho kitu na kumpa Mungu sifa, basi Mungu hutoa
baraka ili mtu huyo aongezewe!
Maandiko haya ni mfano halisi unaohakisi fikra na
maisha yetu watanzania. Mungu ametupa kila lililojema ndani ya nchi yetu.
Ametupa madini, ardhi yenye rutuba, maji ya kila aina (bahari, maziwa, mito,
mabwawa), mbuga za wanyama, misitu, hali ya hewa safi, milima, mabonde na
mambo mengine mengi mazuri ambayo yanazidi kuongezeka kila kukicha. Bahati
mbaya sana watanzania tumekumbwa na ugonjwa wa ‘asiyenacho’ na
kumkufuru Mungu kwa kujiona hatuna kitu hivyo kanuni ile ile inaendelea
kututafuna, ‘tunanyang’anywa na kupewa wale wanaojitambua’!
Tumeendelea kulia juu ya umaskini wetu na
kuwaangukia wale tunaodhani wanacho; nao bila hiyana wamekuja kutimiza agizo la
Mungu kwamba maadamu tumekiri hatuna kitu basi kile watakacho kikuta sio chetu
hivyo ni halali kuondoka nacho.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, sura ya 9(k) inatamka kwamba nchi inatawalika kufuata misingi ya
demokrasia na ujamaa. Sina tatizo sehemu hii ya katiba mpaka hapo labda kwa
mawazo ya wengi sehemu itakapo badilika kwenye katiba mpya na huenda neno ‘ujamaa’
au sehemu nzima ikabaki kama ilivyo. Ujamaa una misingi mizuri ya umoja na
upendo.
Sasa hili la ujamaa liko kwenye jamii
zetu na mioyoni mwetu pia. Katika jamii nyingi za kitanzania chakula kikisalia
kinakuwa ‘kiporo’ kwa ajili ya kesho hususani kwa watoto. Kwa familia
zenye upendo na kwa misingi ya kijamaa, huita hata watoto wa jirani
ili kiporo kiliwe na kuisha, kisiwe kiporo tena kwani
kitaharibika. Sasa masikitiko yangu ni kwamba rasilimali zetu tumezigeuza kiporo
na hivyo tunahitaji watu ‘majirani’ kutoka nje tusaidiane kiporo
hiki. Ndio, rasilimali zimekuwa kiporo hata kabla hatujala na kusaza;
na mbaya zaidi tunaita watoto wa jirani ambao ni warafi kupindukia!
Utaratibu wa kiporo ni kwamba yule aliye
mkubwa anakula kidogo na kuwaachia wadogo. Maajabu ni kwamba hawa watoto
wakubwa kutoka kwa jirani sio tu wanaenda sambamba na watoto wenyeji, ambao
ndio wametoa mwaliko, bali wanamaliza kabisa na nafasi inapopatikana
wanawashika wenyeji wao mkono! Haidhuru hiki ni kiporo!
Kesho tutaenda kwa jirani tena na kulalamika kuwa
hatuna kitu zaidi ya kiporo chetu, ‘Tanzania has abundance of
natural resources which are yet to be utilized'. Msisitizo ni kuwa sisi
hatuna kitu na wasitegemee chochote kutoka kwetu na pia sisi hatuhitaji
chochote kutoka kwao zaidi ya kutuongoza kukishughulikia kiporo hicho.
Ndio tutasema hatuna kitu, hatuna wasomi, hatuna ujuzi, zana hatuna, hatuna
teknolojia, na zaidi sana hatuna uelewa juu ya thamani ya rasilimali zetu.
Masikitiko yangu ni pale ikifika siku hata hicho kiporo
kikaisha. Picha iliyojaa uchungu na huzuni inanijia, namuona ‘baba’
ameweka mikono nyuma akienda kwa jirani na kumwaambia hatuna kitu na
kile kiporo tulichozoea kuwaita watoto wake waje washiriki nasi sasa
hakipo! Tuamke sasa majuto ni mjukuu.
Haya yote yametokea, yanatokea na huenda
yakaendelea kutokea kwa sababu hatujitambui. Hatuijui thamani yetu, zaidi sana
kosa letu kubwa ni kujiona kuwa sisi sio kitu. Wasomi kimya, wataalamu tafiti
zao mpaka pesa na msaada kutoka kwa jirani, walio bahatika kupata
elimu wameikumbatia na imebaki vichwani mwao badala ya kuieneza kwa jamii,
wachache ‘walalahai’ waliofanikiwa kujikwamua ndio wametoka hivyo na
familia zao hawajui watu baki wanaamkaje, na mwisho ukombozi wa matatizo yetu
tumewatwisha watu wachache kisa ‘wanaharakati’ kama vile wao hawana
roho za nyama!
Natoa wito kwa watanzania wote kuitambua thamani
yetu na mali alizotujalia mwenyezi Mungu. Tunaomba viongozi tuliowaweka
madarakani watuongoze vema katika hili. Tukienda nje ya mipaka yetu tusimame
imara, tujivunie tunu hizi na tuzitangaze kwa faida yetu. Kwenye mikataba ya
rasilimali zetu, tuangalie maslahi yetu kwanza na daima tusikubali chini ya
masilahi ya wote-watanzania na wageni yazingatiwe, ‘win-win’. Hapa
naomba nisisitize kwamba tunapoingia mikataba, wajibu wetu ni kuangalia na
kutetea maslahi ya watanzania na tuache upande wa pili ufanye ya kwake.
Watanzania tumeumizwa sana na kauli mambo ya haibu kwamba baada ya miaka 50 ya
Uhuru bado mikataba ya kubadilishana ‘shanga’ kwa ‘dhahabu’
inaendelea. Kauli za wataalamu wetu hawakuwa makini kwenye mikataba ni jambo
lililozoeleka kwenye masikio ya watanzania.
Tujifunze kwa familia za majirani,
Marekani na washirika wake. Ukifuatilia kauli mbalimbali za Rais yoyote wa
wakati wowote na wa kutoka upande wowote wa itikadi aliyewahi kutawala
Marekani, kauli mbiu na sera huwa hazibadiliki ‘kwa faida ya raia wa
Marekani’. Kauli zenye mlengo huo kamwe hazibadiliki hata kama Rais huyo
anahutubia kwenye majukwaa ya kimataifa. Mara nyingi imekuwa kawaida ya dunia
kutafsiri kwamba lile lililo jema kwa Marekani basi ni jema kwetu pia, jambo
ambalo sio sahihi mara zote na hivyo kupelekea ‘sisi kukosa wao kupata’.
Imeendelea kuwa hivyo kwa sababu dunia, kuondoa majirani hawa,
imekiuka kanuni ya kwanza ya mikataba ambayo ni kuangalia maslahi yako kwanza
kwani usipofanya hivyo hakuna atakayefanya kwa ajili yako!
Sisi sio kwamba hatuna kitu, bali tuna kitu tena
chenye thamani, hivyo tunahitaji kukitambua ili tuongezewe! Sisi tuna mali wao
wana mahitaji, tusijinyenyekeze! Tuko sawa katika mizania ya kibiashara,
tuzungumze kama wenye mali na tuwasikilize wale walio wateja wetu kwa kutumia
kanuni za kimasoko. Pale ambapo tunafaida ya ziada kwa vitu hadimu, tuitumie
vizuri nguvu ya soko, ‘monopoly’ kujinufaisha. Tusipotimiza vema
wajibu wetu, wenzetu watatimiza wa kwao na hakuna atakaye tuonea huruma siku
tukiwa wateja wao.
Mungu ibariki Tanzania!