TFF yasalimu amri ya serikali
HATIMAYE Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limelazimika kukubaliana na
maagizo ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo juu ya sakata la katiba ya
shirikisho hilo. Awali, serikali kupitia kwa waziri wa wizara hiyo, Dk.
Fenella Mukangara, iliiagiza TFF kutumia katiba ya mwaka 2006, badala ya
ile ya 2012 ambayo inadaiwa kuwa na kasoro nyingi lakini shirikisho
hilo likagoma. Katika kikao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam
kati ya serikali na TFF kikiwa ni cha pili baada ya kile cha awali
kuisha bila makubaliano, inaelezwa kuwa shirikisho hilo lilinyoosha
mkono na kukubali maagizo ya serikali. “Kikao kilikuwa kizito kwa kweli,
rais (Leodegar Tenga) alizungumza mengi juu ya kile wanachokiona kama
TFF juu ya maagizo waliyopewa na serikali na waziri akawasikiliza lakini
ilibidi mwisho msimamo wa serikali ubaki vilevile kama ilivyokuwa awali
na sasa itatubidi tufuate, hakuna jinsi,” kilisema chanzo cha kuaminika
kutoka TFF ambacho kilihudhuria kikao hicho. Katibu Mkuu wa TFF,
Angetile Osiah, amekiri kufanyika kwa kikao hicho ingawa aligoma
katakata kuzungumzia juu ya kile kilichojiri huku akiahidi kila kitu
kitazungumzwa leo. “Kikao kimefanyika lakini siwezi kuzungumzia lolote
kwa sasa mpaka hapo kesho (leo) mtakapopewa taarifa kamili,” alisema
Osiah.
source: Global Publishers
source: Global Publishers