Waliomteka Kibanda hadharani kesho Jumatatu
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
Hatimaye sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, (TEF), Absalom Kibanda, limepata mwanga na watuhumiwa wa kadhia hiyo wataanikwa hadharani kesho.
Hatimaye sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, (TEF), Absalom Kibanda, limepata mwanga na watuhumiwa wa kadhia hiyo wataanikwa hadharani kesho.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova, amesema timu iliyoundwa kuchunguza kutekwa,
kuteswa na kujeruhiwa kwa Kibanda, itatoa taarifa kamili na idadi ya
watu waliowakamata kuhusiana na tukio hilo.
Wakati Kova akieleza hilo, mitandao ya
kijamii jana ilieleza kuhusu taarifa za kukamatwa kwa mtu aliyejulikana
kwa jina la Ludovick Joseph kwa tuhuma za kuhusika kuteswa kwa Kibanda.
Kova alipoulizwa kuhusiana na taarifa
hizo, aliomba apewe muda ili awasiliane na mwenyekiti wa timu
iliyoundwa kuchunguza tukio hilo.
“Tangu asubuhi nilikuwa Mabwepande, ndiyo
nimerudi ofisini muda sio mrefu, kuhusu hilo nimelisikia kupitia kwa
waandishi wenzako walionipigia simu, nipe muda nilifuatilie,” alisema.
Baada ya kupigiwa tena, Kova alisema kwa
mujibu wa maelekezo aliyopewa na timu hiyo, haikuwa muda muafaka
kulizungumzia suala hilo jana.
“Wameniambia taarifa kamili ya kile
walichokuwa wakikichunguza kwa muda wote, kitatolewa siku ya Jumatatu
(kesho) kupitia mkutano wa waandishi wa habari. Huko mtaelezwa wangapi
walikamatwa na kuhojiwa na nini kitafuata,” alisema Kova na kukata simu.
Awali, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilieleza kuwa, Joseph alikamatwa akiwa mkoani Iringa.
Gazeti hili lilipowasiliana na Kaimu
Kamanda wa mkoa huo, Wankyo Nyigesa, alisema tangu juzi amekuwa akipokea
simu za waandishi wa habari zikiulizia tukio hilo.
Alisema amewasiliana na polisi kwenye eneo
lake na kuthibitishiwa hakuna tukio la aina hiyo na kumwomba mwandishi
ajaribu kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe.
Kupitia mtandano wa kijamii wa ‘Mjengwa’,
katika ukurasa wake aliandika kuwa usiku (bila kutaja ni lini) akiwa
kwenye shughuli ya shule ya watoto wake Highlands Hall Iringa, alipata
habari kuwa Joseph amekamatwa.
Katika ukurasa huo alidai kuwa Joseph alikamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kuteswa mwandishi Absalom Kibanda.
Pia alidai jinsi anavyomfahamu kijana huyo
toka akiwa Chuo Kikuu (DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania
anaowafahamu kupitia kazi zake za magazeti.
Taarifa hiyo ilisema, Joseph amekuwa
akiishi Dar es Salaam na ni miongoni mwa waliokuwa wakimsaidia kwa
kujitolea kwenye kazi zake za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na
website (tovuti) ya kwanza ya Jamii.
Kadhalika, alisema miezi ya hivi karibuni
Joseph ndiye aliyekuwa akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwa
blog kila asubuhi.
“Akiwa Dar es Salaam na mimi nikiwa
Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali
amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa
na pale ikiwamo kunipelekea invoice (ankara ya malipo) kwa watangazaji
kwenye Mjengwa blog. Mara nyingi nimekuwa nikimtambulisha kama '
Msaidizi wa Mwenyekiti” alisema.
Aliongeza kuwa juzi alimwomba aende Iringa
ampelekee vitabu vyake vya invoice na risiti kutokana na kutegemea
ugeni kutoka Mfuko wa Ruzuku kwa Vyombo vya Habari (TMF).
Mjengwa blog katika ukurasa huo, amedai
kuwa katika hilo lililomtokea, hawezi kumtetea wala kumtia hatiani kwa
kuwa naye ni binadamu kama wengine na hawezi kusema anamfahamu zaidi.
“Kwa vile yuko mikononi mwa vyombo vya
usalama, nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili
kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima…”
“Na kama ni kweli kwa namna yoyote ile
itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo ya
kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo,” alisema.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa
New Habari (2006), alijeruhiwa usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita na
watu wasiofahamika.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI