Bukobawadau

Wanasheria watishia kuifikisha Serikali mahakamani

RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla amesema msimamo wa kufikisha serikali mahakamani kutokana na kuvunja sheria za nchi, upo palepale.
Akizungumza ofisini kwake jana, Stolla alisema kitendo cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza kuporomoka kwa ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne,  ni mwendelezo wa serikali kuvunja sheria.
“Sheria inayoruhusu serikali kuunda tume za kuchunguza matukio mbalimbali kwa maslahi ya taifa, inatoa mamlaka hayo kwa Rais kama taasisi siyo mtu mwingine yeyote,” alisema Stolla.
Stolla alisema sheria hiyo imemwekea hata Rais mipaka katika utekelezaji wa jukumu hilo, hana mamlaka ya kuunda tume kuchunguza baadhi ya mambo, mathalan vifo vinavyotokana na matumizi ya nguvu ya dola au vilivyoghubikwa na utata.
Vifo vya aina hiyo vilielezwa na Stolla kuwa, kisheria vinatakiwa kuundiwa tume na kuchunguzwa na Mahakama ya Corona, ikiwezeshwa na serikali.
Alisema TLS wanayo majukumu mawili ya msingi, kushauri serikali na kulinda umma juu ya mambo yanayohusu sheria.
Kwa mujibu wa Stolla, taasisi hiyo itatumia haki yake kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba, kufungua kesi mahakamani kuhusu suala hilo.
“Msimamo wetu juu ya tafsiri ya sheria ya uundaji tume maalumu ni kwamba mwenye mamlaka hayo ni taasisi ya Rais tu, isipokuwa ya vifo vya aina niliyotaja, msimamo wetu unabaki kuwa Pinda na Nchimbi wamevunja sheria,” alisema Stolla.
Stolla alisema moja ya mambo yaliyo mezani kusubiri baraka za baraza jipya la taasisi hiyo lililochaguliwa Februari 23 mwaka huu, ni kufikisha kortini serikali juu ya kuvunja sheria inayohusu kuunda tume za uchunguzi.
“Mfano taifa zima kuwa na wanafunzi 28,000 tu waliofaulu kati ya daraja I, II na III, huku asilimia 65 ya watahiniwa wote wakiambulia sifuri ni tishio lisilohitaji mzaha,” alisema Stolla.

Dokezo:
Mapema Februali mwaka huu, Stolla alikaririwa na vyombo vya habari wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria, akisema taasisi hiyo itaifikisha mahakama kuu serikali kwa kuvunja sharia inayohusu kuundwa tume za kuchunguza mtukio mbalimbali nchini.
Alisema tume zinazoundwa na viongozi wasiyo katika taasisi ya Rais, kuchunguza matukio mbalimbali kwa maslahi ya umma ni batili kisheria.
Kumbukumbu
Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa mambo ya ndani, Emmanuel Nchimbi aliunda tume kuchunguza kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari, wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten mkoani Iringa ambaye aliuawa kwa mripuko wa bomu, kijijini Nyololo.
Hivi karibuni, waziri mkuu Mizengo Pinda ameunda tume ya kuchunguza kuporomoka kiwango cha ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne kitaifa, kwa lengo la kupata suluhisho la tatizo hilo.
Source; Mwananchi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau