YA KCU (1990) LTD NI MAKUBWA KULIKO YANAVYOONEKANA .
Na Prudence Karugendo
PAMOJA na serikali kukiri kwamba
matatizo yaliyomo kwenye Chama Kikuu cha Ushirika, mkoani Kagera, KCU (1990)
Ltd., ni makubwa kuliko yanavyoonekana na kuthibitisha kwamba inayafanyia kazi
kwa njia inazozijua yenyewe baada ya kuzishtukia mbinu chafu za wafanyakazi na
viongozi wa chama hicho za kuingilia mara kwa mara uchunguzi wa serikali
unaofanywa dhidi ya tuhuma ndani ya chama hicho, pamoja na ahadi ya kwamba
serikali inaunda tume itayojitegemea katika kuudhibiti uendeshaji wa vyama vya
ushirika, bado wanachama wa KCU (1990) Ltd. wanayo mengi ambayo wasingetaka
yabaki nyuma ya pazia.
Wanachama hao wanayo madai ya
kwamba, mbali na ufisadi wa aina mbalimbali ambao wameishaupigia sana kelele
kwenye chama chao, kuna ufisadi unaofanyika kupitia kwenye
matengenezo ya magari ya chama chao hicho cha ushirika.
Inasemekana kwamba baadhi ya
madereva wa KCU (1990) Ltd. waliandika barua kwa uongozi wa ushirika wakiomba
kubadilishiwa sehemu ya kutengenezea magari (gereji) kwani uwezo wa sehemu
waliyokuwa wakiitumia ulikuwa ni mdogo mno. Lakini eti uongozi haukufanya kitu
chochote zaidi ya kuwasimamisha kazi madereva walioandika barua hiyo. Wapo
madereva waliobambikiwa makosa, kama ya kuiba vifaa vya magari, katika
kuhalalisha kuondolewa kwao kazini. Lakini sababu hasa ikiwa ni hiyo ya
kuikataa gereji bubu kwa ajili ya kutengeneza magari ya chama cha ushirika.
Inasemekana pia kwamba mmiliki mmoja
wa gereji inayolalamikiwa aliwahi kumuapia dereva mmojawapo kwamba atafanya
kila njia ahakikishe anafukuzwa kazi.
Yapo madai mengine ya kwamba hayo
yote yanatokea kwa vile Meneja Mkuu na baadhi ya wajumbe wa Bodi wamekuwa
wakigawana pesa wanazodai ni za matengenezo ya magari.
Aidha, inasemekana kwamba
Meneja Mkuu anaoa nyumba moja na mmoja wa wamiliki wa gereji hiyo
inayolalamikiwa kuwa mojawapo ya matundu yanayopoteza pesa za wanaushirika.
Kwa hali hiyo basi, bado chama cha
ushirika, KCU (1990) Ltd., kimefanywa kiendelee kuonekana ni mali ya mtu
binafsi na siyo chombo kinachowapa tija wakulima wa kahawa ambao ndio wamiliki
wa chombo hicho.
Shutuma nyingine zinaelekezwa kwa
Mwenyekiti wa Bodi ya KCU (1990) Ltd.. Inasemekana, kwa kawaida, mwenyekiti
anatakiwa kufika ofisini mara mbili kwa wiki, kama ilivyokuwa ikifanyika miaka
ya nyuma wakati chama hicho kilipokuwa kikiendesha shughuli zake kwa ufanisi na
kuleta tija kwa wanaushirika, ili kufanya mambo yasiyokuwa ya muda wote ofisini
kama vile kusaini hundi na kuangalia shughuli nyingine za kiutendaji.
Lakini baadaye, kutokana na
kuhitajika mara kwa mara, basi ikaonekana ni bora mwenyekiti awe ofisini mara
tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Lakini hatahivyo inasemekana
mwenyekiti wa sasa amekuwa akienda ofisini kwa siku zote za wiki na kulipwa
posho siku zote hizo. Mbali na hilo mwenyekiti anatumia gari la KCU (1990) Ltd.
kumfuata nyumbani kwake, Muhutwe, Muleba, kuja ofisini, Bukoba Mjini, na
kumrudisha kwa umbari ambao ni kama kilometa 86 kwenda na kurudi.
Kwahiyo mwenyekiti huyo tangu aingie
madarakani ameishatumia kiasi kisichopungua shilingi 65, 000, 000/= zilizolipwa
kwake kama posho. Vilevile ametumia kiasi cha shilingi 68, 640, 000/= kama
gharama ya mafuta ya gari linapomfuata na kumrudisha kwake mara tano kwa wiki
tangu awe mwenyekiti. Hiyo haihusishi gharama za matengenezo ya gari
linalotumika kwa ajili yake.
Hali hiyo imesababisha hadi
akawekewa tangazo kwenye mlango wa ofisi yake angalau kumkumbusha siku
anazotakiwa kuwa ofisini ijapokuwa utekelezaji wa tangazo hilo ni wa matata
sana.
Shutuma nyingine ni kwamba chama
kilinunua magunia ya kuwekea kahawa safi ambayo hayakuwa na ubora unaotakiwa na
hivyo kulazimika kununua magunia mengine tena kwa ajili ya kusafirisha kahawa
safi kwenda nje. Ikumbukwe kwamba yote hiyo ilifanyika bila kufuata taratibu za
manunuzi, na pia bila kuhusisha wataalamu, na hivyo kukisababishia chama cha
ushirika hasara ya takriban shilingi milioni 60.
Madai mengine ni kwamba Meneja Mkuu,
kwa kutumia ubabe wake, alifanya mabadiliko katika utaratibu wa ulinzi wa mali
za chama. Alibadilisha walinzi katika hoteli zinazomilikiwa na KCU (1990) Ltd,
Lake na Bukoba Co-op. zilizopo Bukoba Mjini, pamoja na walinzi wanaolinda
kwenye mradi wa kuosha kahawa wa Birabo wilayani Muleba, na kuwaweka walinzi wa
kampuni yake mwenyewe ya Kamweruka Security. Kampuni hiyo ya ulinzi inamilikiwa
na yeye Meneja Mkuu kwa kushirikiana na Afisa Ardhi na Majengo wa KCU (1990)
Ltd.. Na kibaya zaidi ni kwamba kampuni hiyo haikupata zabuni yoyote wala
mkataba wa ulinzi uliopitishwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kampuni hiyo inafanya
kazi kinyemela kwa maslahi yao binafsi yanayokinzana na ya kampuni ya Salu
Security yenye mkataba halali wa kufanya shughuli za ulinzi kwenye mali za KCU
(1990) Ltd..
Lakini inadaiwa kwamba yote hayo
yanasababishwa na uongozi wa Bodi kutokuwa makini katika usimamizi mzima wa
uendeshaji wa shughuli za ushirika. Eti inaonekana Mwenyekiti na Meneja Mkuu,
kwa kwa makusudi mazima, wanafanya makosa hayo wakiamini kwamba hayawezi
kujulikana kwa wanaushirika, ambao kwa asilimia iliyo kubwa ni wakulima wa
vijijini wanaochukuliwa kuwa na uelewa mdogo wa mambo. Meneja Mkuu, mtu msomi,
ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za kila siku za chama cha ushirika.
Kwahiyo usomi wake unapaswa uwape
faida kwa wakulima, ndiyo maana wakamuajiri, na siyo kuwafilisi kwa vile
eti wao hawajasoma na wana uelewa mdogo. Hivyo akautumia uelewa huo mdogo wa
wanaushirika kama mtaji wa kujineemesha akiwa amejitajirisha kwa njia haramu.
Wanaushirika wanasema kwamba lenye
uzito kwa watu hao wawili, Meneja Mkuu na Mwenyekiti, ni lile linalogusa kwenye
maslahi yao binafsi tu basi.
Kwahiyo wanaushirika hao wanasema
kwamba kwa vile Bodi ya Wakurugenzi imeshindwa kuleta amani na mshikamano ndani
ya ushirika, basi vyombo vinavyohusika katika kushughulikia kadhia za aina hiyo
vijaribu kuingilia kati angalau kuinusuru hali inayozidi kuwa tete kabla
haijawa mbaya zaidi na ya kutisha.
Wanasema kwamba taarifa
zilishapelekwa kwenye vyombo mbalimbali, ikiwemo Takukuru, lakini kwa mshangao
wao wanasema hakuna chochote kilichofanyika, jambo linalowaletea hisia za
kwamba kuna namna ya kupozana miongoni mwa wahusika kusudi mambo yabaki jinsi
yalivyo.
0784 989
512