GAZETI LA MWANANCHI LIMEANDIKA;Alex Massawe mtegoni nchini Afrika Kusini
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu Alex
Massawe ameingia kwenye mtego wa Polisi wa Afrika Kusini ambao wamekuwa
wakimsaka baada ya kuombwa na Serikali ya Tanzania.
Habari kutoka katika Jeshi la Polisi zinaeleza
kuwa baada ya Polisi wa Tanzania kuthibitishwa na maofisa wa Afrika
Kusini kuwa wamefahamu aliko wameandaa maombi kwenda Shirika la Polisi
la Kimataifa (Interpol) ili akamatwe na kurejeshwa nchini.
Licha ya kutokufahamika kwa sababu za kusakwa
kwake, hakuna kiongozi yeyote wa polisi aliyekuwa tayari kuzungumzia
tukio hilo lakini chanzo cha kuaminika kutoka katika jeshi hilo
kilieleza kuwa wenzao wa Afrika Kusini wamewaeleza kuwa wamefahamu
aliko.
Kusakwa kwa Massawe kumezua maswali kadhaa
kutokana na kutokuwekwa wazi. Lakini Aprili 4, mwaka huu alitajwa
mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly
ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa
nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni
mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshitakiwa
mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu
Mkazi, Agnes Mchome mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo
kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya
kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao
lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa
ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe
akamatwe.
“Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza
ili Massawe akamatwe. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa
Interpol juu ya kumsaka mtu huyo ili aletwe. Ndiyo maana Polisi wa
Tanzania hawawezi kuzungumza chochote hadi watakapomweka mikononi
mtuhumiwa huyo,” kilieleza chanzo cha gazeti hili.
Awali, kulikuwa na habari kwamba Massawe, ambaye
hufanya biashara za hoteli na mambo ya utalii katika Jiji la Dar es
Salaam, Arusha na Moshi, amekamatwa katika mji mmojawapo ulioko katika
Pwani ya Afrika Kusini.
Habari hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia
hufadhili masuala ya kisiasa na michezo, zilianza kusambaa jana mapema
asubuhi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter na
Jamii Forum huku ikidaiwa amekamatwa.
Kulikuwa kuna mkanganyiko wa taarifa huku wengine
wakidai alinaswa akiwa ndani ya boti huko Afrika Kusini, wengine wakidai
alikamatwa wakati akijaribu kuingia Msumbiji akitokea Malawi.