KAGERA WALIA NA OFISI YA MRAJISI WA VYAMA VYA USHIRIKA
Na Prudence
Karugendo
MRAJISI wa
Vyama vya Ushirika ni msimamizi na mlezi wa ushirika nchini. Kwa nafasi yake
hiyo tunategemea kuwaona wananchi wakiwa wameboresha maisha yao baadaya ya
kuunganisha nguvu zao kwa mtindo wa ushirika kujiinua kiuchumi. Hali hiyo
inajiweka wazi kutokana na kuwepo kwa ofisi ya Mrajis inayopaswa kutoa moungozo
wa kitaalamu na kuhakikisha ushirika unakuwa imara na kutoa matunda
yaliyokusudiwa.
Wananchi
wanatarajia kuyaona maisha yao yakishamiri yakiwa ndiyo matunda ya ushirika.
Sababu ushirika siyo mapambo, bali njia ya wananchi kuinuana kiuchumi, kujiondoa
kwenye ufukara.
Lakini katika
miaka ya karibuni ushirika nchini umeangukia pua. Vyama vingi vya ushirika,
katika maeneo mbalimbali ya nchi, vimezorota sana na vingine kufa kabisa. Tena
cha kusikitisha, vinakufa vifo vya kulazimishwa kutokana na kuhujumiwa.
Swali
linalojitokeza ni la kwa nini hali iwe hivyo ilhali ofisi iliyotengwa na serikali
kwa ajili ya kuvisimamia na kuvilea vyama vya ushirika, Ofisi ya Mrajis wa
Vyama vya Ushirika, inaendelea kufanya kazi? Kwa nini vyama vya ushirika
vionekane yatima wakati mzazi na mlezi wake bado yuko hai?
Swali hilo
linazidi kuwa tata na kuzidisha ugumu wa kujibika hasa pale zinapojitokeza
dalili za kwamba Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika, kwa njia moja au
nyingine, nayo inahusika na vitendo vya kudhoofisha shughuli za ushirika
nchini.
Dalili hizo
mbaya na za kushangaza zimeanza kujionyesha kupitia mkoani Kagera ambako
wanaushirika, chini ya chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd.,
wanailalamikia Ofisi ya Mrajis kwa kushindwa kuchukua hatua muafaka kukinusuru
chama chao cha ushirika.
Mbali na
malalamiko kadhaa ambayo yameishamfikia hata Waziri wa Kilimo na Ushirika, hasa
malalamiko ya kuhusu ukaribu husio na kheri kati ya Mrajis Msaidizi mkoani
Kagera na uongozi wa KCU (1990) Ltd., yapo vilevile malalamiko mengine kuhusu
Mrajis Msaidizi kupindisha mambo kinyume cha utaratibu katika uendeshaji wa
Benki ya Wakulima, Kagera Farmers’ Co-operative Bank, ambayo KCU (1990) Ltd. ni
mwanahisa.
Mwaka 2002 Bodi
ya KCU (1990) Ltd. ilitoa wazo la kuanzisha Benki ya Wakulima kwa kuwatafuta
wanahisa wengine ili kutimiza azima hiyo. Wazo hilo lilipata Baraka za
Mkutano Mkuu na hivyo Benki ya Wakulima, Kagera Farmers’ Co-operative
Bank (KFCB), ikawa imeanzishwa baada ya kupata leseni toka Benki Kuu ya
Tanzania.
Wanahisa
waanzilishi walikuwa ni KCU (1990) Ltd. yenyewe, Mfuko wa Mazao, na Vyama vya
Msingi. Baadaye Saccos na Maihanika (saccos kwenye vyama vya msingi) nao
wakapewa hisa.
Madhumuni ya
kuanzisha Benki ya Wakulima, pamoja na mambo mengine, yalikuwa kwamba KCU
(1990) Ltd. iweze kukopa kwenye benki hiyo ili kuepuka riba kubwa zinazotozwa
na mabenki mengine. Vilevile riba ndogo iliyotarajiwa kutozwa na benki hiyo
bado ilikuwa ni faida kwa wenye benki ambao ni pamoja na wakulima, wanaushirika.
Lakini ni jambo
la kushangaza kwamba tangu kuanzishwa kwa KFCB, KCU (1990) Ltd. haijawahi
kukopa kwenye benki hiyo kwa kiasi cha kuridhisha. Kisingizio mara zote
kimekuwa kwamba benki hiyo haijawa na mtaji wa kutosheleza mahitaji ya KCU
(1990) Ltd. Hata pale benki hiyo ilipopata pesa kutoka mfuko wa serikali kwa
ajili ya kuwainua wakulima (AGIPF), bado KCU (1990) Ltd. iligoma kukopa kwenye
benki hiyo na hivyo kuikosesha riba ndogo ambayo ingenufaika nayo kama faida,
wakati chama hicho cha ushirika kikiendelea kukopa kwenye benki za CRDB na
nyingine kwa riba kubwa!
Baada ya maswali
kuwa mengi juu ya kwa nini aliyetarajiwa kuwa mteja mkubwa na wa kutumainiwa na
KFCB, KCU (1990) Ltd., anagoma kuitumia benki hiyo, maswali na mshangao hasa
vilivyokuwa vinatoka kwenye uongozi wa KFCB, ndipo ikaanza kufanyika mizengwe
ya kuuondoa uongozi wa benki hiyo kusudi uwekwe uongozi unaotokana na KCU
(1990) Ltd. kwa lengo la kuendelea kuidhoofisha benki hiyo kimyakimya.
Ni kweli kwamba
KCU (1990) Ltd. ndiye mwanahisa mkubwa kuliko wote katika Benki ya Wakulima,
lakini katika sheria za ushirika hakuna panaposemwa kwamba mwenye hisa kubwa
ndiye awe kiongozi.
Kwahiyo ni wazi
kwamba, mizengwe hiyo ambayo kwa sasa tayari imefanikiwa, ya KCU (1990) Ltd.
kukamata uongozi wa KFCB, ililenga kuyazima maswali ya kwa nini chama hicho
kikuu cha ushirika hakiitumii benki hiyo kama yalivyokuwa madhumuni ya
uanzishwaji wake.
Jambo la
kushangaza ni namna Mrajis Msaidizi alivyoidaka mizengwe hiyo, iliyoonekana
tayari ilikuwa na Baraka zake, na kuigeuza ya kwake kiasi cha kuitumia
yeye mwenyewe dhidi ya uongozi wa KFCB uliokuwa unamaliza kipindi kimoja kabla
ya kuendelea na kipindi kingine.
Mrajis Msaidizi
aliingiza kinyemela kwenye masharti ya Bodi ya KFCB kipengere ambacho hakikuwa
na Baraka za Bodi. Kipengere hicho kilichoingizwa kinyemela kinasema kwamba
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KFCB ni sharti watoke kwenye Bodi za vyama vya
msingi, kitu kinachowatenga baadhi ya wenye hisa, wenye mali, kwa kuwanyima
fursa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwenye benki yao isipokuwa kupiga
kura tu, tena kwenye vyama vyao vya msingi.
Kipengere hicho
kilichochomekwa na Mrajis Msaidizi, moja kwa moja, kinaubatilisha Mkutano Mkuu uliofanyika mwaka
jana na kuuondoa madarakani uongozi wa KFCB kwa vile kilikuwa kimewafukuza
wajumbe halali wa mkutano mkuu. Hivyo Mkutano Mkuu wa mwaka jana ulifanywa na
wajumbe waliopatikana kinyemela kwa juhudi binafsi za Mrajis Msaidizi. Na mkutano
huo ndio ukaja kutoa Baraka za marekebisho ya masharti hayo mapya yaliyoletwa
na Mrajis Msaidizi na kuwafukuza wajumbe halali wa Bodi na Mkuatano Mkuu wa
KFCB.
Kwa vielelezo
vinavyoonyeshwa na wahusika ni kwamba masharti mapya hayakupitia kwenye mkutano
wa Bodi ya KFCB wala Mkutano Mkuu, na hata Mrajis Msaidizi alikuwa hajayasaini,
lakini cha kushangaza yakatumika kuendesha Mkutano Mkuu!
Wanaushirika
wanasema kwamba Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Kagera yupo kumsaidia Mrajis wa
Vyama vya Ushirika nchini. Lakini eti badala yake anaonekana kumpotosha, sasa
haieleweki kama huo upotoshaji ndio msaada unaotakiwa na mtu kutoka kwa
msaidizi wake.
Eti Mrajis
Msaidizi alimweleza Mrajis kwamba watu hawa, wajumbe wa Bodi ya KFCB, wamekaa
kwa muda mrefu wakati ukweli ni kwamba wajumbe hao wa Bodi walikuwa na
kipindi kimoja na mmoja tu ndiye aliyekuwa na vipindi viwili. Wakati kanuni ya
theluthi inaagiza mtu akae vipindi vitatu. Katika mkutano wa mwaka jana mtu
mmoja ndiye aliyekuwa anaingia katika theluthi ya tatu wakati wengine walikuwa
wanaingia theluthi ya pili.
Mbinu chafu za
Mrajis Msaidizi. Wajumbe wa zamani waliotaka kugombea tena ujumbe wa Bodi ya
KFCB, katika uchaguzi wa mwaka jana, ambao walikuwa hawabanwi na kipengere
kipya cha Mrajis Msaidizi, walinyimwa fomu kwa hadaa kuwa fomu zao za zamani
zilikuwepo, zinatosha. Lakini baadaye Mrajis Msaidizi akatangaza bila aibu
kwamba wajumbe ambao hawakujaza fomu walikuwa wamejiondoa wenyewe kwenye
kugombea. Matokeo yake Mrajis Msaidizi akashindwa kuwapata wagombeaji wa kutosha,
mkutano ikabidi uahirishwe.
Wanaushirika
wanasema kwamba hayo yote yamefanyika kwa shinikizo la KCU (1990) Ltd. kwa vile
chama hicho kikuu cha ushirika hakikuwa katika mahusiano mazuri na mwenyekiti
wa Bodi ya KFCB aliyeondolewa kinyemela.
Nilipomtafuta
mwenyekiti huyo aliyeondolewa, Bw. Rweyongeza Bagyemu, kuona kama analo la
kuongea juu ya sakata hilo, akasema kwa sasa amelazwa anaumwa. Hivyo hawezi
kuongelea suala hilo kwa wakati huu. Ila akathibitisha kwamba niliyoelezwa yote
yana ukweli uliokamilika. Na kuahidi kwamba akiwa mzima kuna mengine
atayaongeza katika kuzidi kuliweka wazi suala hilo.
Kwa mwenendo huu
Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Kagera akiendelea kukalia nafasi yake hiyo masuala
yote ya ushirika mkoani Kagera yatabaki tu kwenye masimulizi. Hiyo ni kutokana
na Mrajis huyo Msaidizi kuonekana anatanguliza maslahi binafsi badala ya
maslahi ya ushirika.
Linalopaswa
kuzingatiwa ni kwamba wanaushirika wameamua kuanzisha benki. Ieleweke kwamba
benki ni chombo kinachotakiwa kuendeshwa kwa weledi bila kufuata tu uwakilishi
wa ilmaradi. Hicho ni chombo muhimu cha kiuchumi kinachohitaji watu wenye sifa
zilizo katika taaluma hiyo. Kuichezea benki ni kuuchezea uchumi wa watu na
hivyo kuyachezea maisha na uhai wao.
Pamoja na kwamba
Mrajisi Msaidizi ndiye anayefanya mchujo wa mwisho wa wajumbe wa KFCB,
anatakiwa kuzingatia kwamba benki hiyo imesimama kwenye mihimi miwili. Wa
kwanza ni Ushirika na wa pili ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Lakini
ikiangaliwa itaonekana kwamba wajumbe wa KFCB waliopitishwa na Mrajis Msaidizi
wengi wanakidhi vigezo vya mhimili mmoja tu, ushirika, wakati wako nje kabisa
ya vigezo vya BOT. Hiyo ni kwa sababu wengi wao ni wa darasa la 7. Haitegemewi
hata kidogo mhitimu wa darasa la saba awe na vigezo vya BOT.
Swali
wanalojiuliza wanaushirika ni kwamba, hivi kweli Mrajis Msaidizi wa Kagera
anayo dhamira ya dhati ya kuiona benki hiyo ya wakulima ikishamiri?
Mfano, Kamati ya
Usimamizi inayotakiwa kuwa na wajumbe watatu mpaka sasa inasemekana inaye
mjumbe mmoja tu. Hiyo imesababishwa na mizengwe ya Mrajis Msaidizi ya
kupindisha masharti ya kuwapata wajumbe kwamba ni lazima watoke kwenye Bodi za
vyama vya msingi, kitu ambacho hakimo katika sheria za ushirika, badala ya
wanachama wote. Ni vigumu kuwapata wajumbe wenye vigezo vya BOT kwenye vyama
vya msingi.
Pamoja na
malalamiko ya wanaushirika mkoani Kagera juu ya utendaji usioridhisha wa Mrajis
Msaidizi mkoani humo, bado wadau hao wa ushirika wanayo machache, lakini muhimu, ya kuisemea ofisi ya Mrajis
Msaidizi mkoani mwao.
Wanasema kwamba
ofisi hiyo ni kama imetelekezwa na wahusika kitu kinachomlazimisha Mrajis
Msaidizi ajipendekeze kwa Chama Kikuu cha Ushirika, KCU (1990) Ltd., ili kujinusuru kimaslahi. Ni katika hali hiyo
ambamo Mrajis Msaidizi anajikuta chini ya usimamizi wa chama hicho cha ushirika
kama mwajiriwa wake na hivyo kuuondoa uwezekano wa yeye kukisimamia chama hicho
kama sheria ya vyama vya ushirika inavyoelekeza.