Kama kidato cha kwanza hawajui kusoma na kuandika watashindaje mtihani wa kidato cha nne?
Na Prudence Karugendo
KWA sasa kumejitokeza kashfa ya kitaifa baada ya
matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne ya mwaka jana kuonyesha kuwa
zaidi ya nusu ya watahiniwa wameshindwa vibaya. Matokeo hayo machafu
yanaonekana kuitikisa nchi kiasi cha viongozi wa kisiasa, ngazi ya taifa,
kufikiria kujificha kwa njia ya utamaduni uliozoeleka wa kuunda tume zisizo na
tija yoyote kila baada ya mambo kwenda mrama.
Utamaduni
huu wa kuunda tume au kamati za uchunguzi, na ulaaniwe kwa nguvu zote, umegeuka
kichocheo cha kuendeleza uzembe ndani ya mfumo wa utawala wa nchi yetu kwa
kuyafunika madhambi na uzembe vinavyokuwa vimejitokeza na kusababisha mambo
kwenda kombo.
Nasema hivyo
kwa sababu katika hawamu hizi tatu za serikali yetu, awamu ya pili, ya tatu na
hii ya nne, imegeuka mazoea kwamba kila inapotokea kashfa ya kitaifa inayovuta
hisia za wananchi kiasi cha kuonekana kwamba wananchi wanaweza kufikia uwamuzi
wa kuiwajibisha serikali yao, ni lazima serikali iunde tume au kamati ya
uchunguzi. Tume hiyo itatumia pesa ya wananchi walipa kodi kwa mtindo wa kufa
kufaana kufanya uchunguzi ambao matokeo yake yatabaki ni siri ya serikali bila
ya wananchi waliogharamia uchunguzi huo kuelezwa kilichobainika au walau
kuyaona mabadiliko yanayoweza kuaminika kwamba yameshinikizwa na uchunguzi
husika.
Mambo
yataendelea kuvurunda kama kawaida yakiwa yanawatesa wananchi yakisubiri
kuundiwa tume nyingine ya uchunguzi na pesa ya walipa kodi ikizidi kuteketea
bila dalili zozote za kupatikana ufumbuzi.
Kwa ufupi,
tume au kamati za uchunguzi zinazoundwa kila baada ya kujitokeza uzembe katika
mfumo wa uwajibikaji wa serikali yetu ni za kuwapofua macho wananchi ili
wasiendelee kuyaangalia madudu yanayofanywa na serikali yao na badala yake
wayaweke matumaini yao kwenye tume au kamati za uchunguzi zinazoundwa.
Sasa
angalia, eti matokeo machafu ya kidato cha nne ya mwaka uliopita nayo
yanaundiwa tume ya uchunguzi! Ni kipi cha kuchunguza kisichoonekana? Wakati
mwaka juzi tuliambiwa na kujionea wenyewe jinsi karibu robo ya wanafunzi
waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka jana walikuwa hawajui kusoma
wala kuandika. Sasa tunaweza kushangaa vipi matokeo ya kidato cha nne kwamba
zaidi ya nusu ya watahiniwa wameshindwa mtihani?
Kwangu mimi
ningeona maajabu iwapo ingetangazwa kwamba matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
ya mwaka jana yanaonesha watahiniwa wamefaulu kwa kiasi cha kutisha. Ingebidi
niunde tume yangu mwenyewe ya kuchunguza ni jinsi gani mtoto wa chekechea, baada ya miaka mine, anavyoweza
kufanya mtihani wa kidato cha nne akafaulu kwa kiwango cha kutisha. Hayo kweli
yangekuwa maajabu ya dunia.
Maana mtu wa
kidato cha kwanza asiyejua kusoma na kuandika ni sawa na chekechekea. Sasa
aanze kufundishwa a e i o u, kisha ba be bi bo b u, baba mama nakadhalika, na
baadaye masomo yote ya darasa la pili mpaka la saba yakifuatiwa na Biolojia,
Kemia, Fizikia na mengine yote ya sekondari, halafu tumtegemee ashinde mtihani
wa taifa wa kidato cha nne kwa kishindo! Kama hayo si maajabu ni kitu gani?
Ndiyo maana
nasema kwamba siwezi kuyashangaa matokeo ya zaidi ya nusu ya watahiniwa
kushindwa vibaya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, sababu ni matokeo
yanayoonekana kuwa yaliandaliwa. Sielewi uchunguzi hapo ni wa nini!
Ninachoweza
kusema kwamba kinahitaji uchunguzi ni matokeo yanayotofautiana na haya. Matokeo
yanayoonyesha kwamba wanafunzi wamefaulu kwa wingi. Hapo ndipo kuna cha
kujiuliza, kwamba wamefaulu vipi wakati muda wote wameandaliwa ili washindwe?
Fikiria
wanafunzi wasio na walimu wa kutosha wanawezaje kushinda mtihani, wanafunzi
wenye walimu wasio na motisha wanawezaje kushinda mtihani? Wanafunzi wasio na
zana za kutosha za kujifunzia, maktaba, vitabu vya kutosha, maabara
nakadhalika, watawezaje kushinda mtihani? Hayo ndiyo mambo ya kuyaangalia
tunapohitaji kuchunguza ni namna gani wanafunzi wanaweza kushinda kwa wingi
katika mazingira haya tata ya ufundishaji. Lakini linapokuja suala la kushindwa
sioni uchunguzi una maana gani kwa vile kila kitu kinaonyesha kwamba kushindwa
ni halali yao.
Mazingira
haya tata ya kielimu hapa nchini kwetu sio suala la kumlaumu mtu mmoja mmoja
kama baadhi ya watu wanavyolichukulia kwa sasa. Kuwalaumu walimu ni kuwaonea
kabisa, hata kumlaumu waziri wa elimu ni kumuonea vilevile. Hili ni tatizo
lililo katika mfumo wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Tatizi hili ni sawa na
saratani ambayo imeishautafuna mwili mzima kiasi kwamba kukiondoa kiungo
chochote katika mwili wa mtu, uwe mkono au mguu, hakuwezi kumrudishia mtu
matumaini ya kuishi. Kitu pekee kinachobaki kama tegemeo la kumuondolea maumivu
mtu ambaye mwili mzima umeishatafunwa na saratani ni kifo.
Kwahiyo hata
sisi Tanzania matumaini pekee tunayoweza kuwa nayo katika suala hili la elimu
kwa sasa ni ya kuuona mfumo mzima uliopo chini ya CCM unakufa na kujaribiwa
mfumo mpya chini ya chama kipya.
Kinachothibitisha
usahihi wa mtazamo wangu ni msimamo wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru
Kawambwa, wa kwamba katu hawezi kujiuzulu kufuatia elimu nchini kuangukia pua.
Katika nchi
zenye mifumo isiyotia shaka, kujiuzulu kwa waziri ambaye chini yake mambo
yamekwenda kombo sio suala la kubembelezana, ni suala la kuamrishana. Lakini
hapa kwetu nani amlaumu nani? Sababu hayo yote ni kushindwa kwa mfumo, na mfumo
hajaubeba mtu mmoja.
Bilashaka
Kawambwa anaelewa kuwa kila mmoja anajua kiini cha tatizo hili kiko wapi na
kwamba kumtoa mtu mmoja kafara hakuwezi kuponya tatizo lililopo hata kama
analetwa malaika kukalia nafasi aliyopo yeye. Tatizo ni mfumo.
Kuisimamia
elimu bora hakuhitaji mtu aliye na elimu ya ajabu isipokuwa umakini katika
kuusimamia mfumo unaoendesha mambo yote ikiwemo elimu. Nitatoa mfano wa Dikteta
Idd Amin aliyekuwa mtawala wa Uganda katika miaka ya 1970.
Amin alikuwa
mtu ambaye hakwenda shule, lakini alikuwa na umakini wa kutosha kuhakikisha
elimu nchini kwake inabaki katika kiwango bora au kiwango kinachopanda badala
ya kushuka!
Amin
aliagiza kwamba kila watahiniwa waliokuwa wanapata daraja la kwanza kuanzia
kidato cha nne wapelekwe kwenye vyuo vya uwalimu ili wakatayarishwe
kuwafundisha wengine. Na wale wa madaraja ya chini ndio waendelee na ngazi za
juu ili kuongeza uelewa.
Hoja ya Amin
ilikuwa kwamba mwanafunzi anayepata daraja la kwanza, iwe kidato cha nne, cha
sita au Chuo Kikuu, ana akili za kutosha kuweza kuwafundisha wengine walio
chini yake wakaelewa vizuri. Matokeo yake Uganda ikawa na walimu bora na
kiwango cha elimu kilicho bora.
Hiyo ni
tofauti kabisa na hapa kwetu ambako ilifikia hatua ya kushindwa kugeuzwa sifa
ya kuwa mwalimu! Wanaokumbuka wataukumbuka mpango wa Universal Primary
Education (UPE). Katika mpango huo wanafunzi waliokuwa wanashindwa darasa la
saba walikuwa wanafanywa walimu ili wakawafundishe wengine! Wangewafundisha
nini zaidi ya kuwafundisha kushindwa ilmradi wamepata elimu ya msingi? Mtu
ambaye kashindwa atamfundishaje mwingine ashinde?
Baada ya
hapo angalia jinsi mambo yalivyo kwa sasa. Wahitimu wa kidato cha nne
wanaofaulu kwa daraja la kwanza na la pili, wengi wao, kama sio wote,
wanapitishwa kuendelea na kidato cha tano au kwenye vyuo vingine tofauti na
vyuo vya elimu. Wale wa daraja la tatu, la nne na wakati mwingine waliopata
sifuri, ndimo wanamopatikana wa kupelekwa kwenye vyuo vya uwalimu! Vivyo hivyo
kwa wahitimu wa kidato cha sita. Tuseme kwenye uwalimu ndiko kunakoonekana kunawafaa watu wenye
uwezo mdogo kiakili!
Katika hali
hiyo ya kuifanya elimu ndiyo sekta isiyohitaji watu wenye vichwa vikali
tutayashangaaje haya tunayoyaona? Tutawashangaa vipi watoto wanaochukua karatasi
za kujibia maswali ya mtihani na kuchora picha za wanasoka wa Ulaya akina
Lionel Messi?
Mtahiniwa
anachora picha ya Messi badala ya picha anayoulizwa, pengine picha ya amoeba au
paramecium katika mtihani wa Biolojia. Hiyo ni kwa sababu anamuona sana Messi
kutokana na uwekezaji uliofanywa na wahusika upande huo, wakati hajawahi
kuviona hata mara moja viumbe hao anaulizwa kwenye mtihani. Anakichora
anachokijua.
Wakati
mwingine katika kutafuta kuboresha kiwango cha elimu walimu wanaomba
kuboreshewa mafao yao japo kwa kiasi kidogo tu, kinyume chake wanakutana na
mabavu ya serikali yaliyojaa vitisho vya kila aina! Kumbuka mkoani Kagera
walimu walichapwa viboko chini ya usimamizi wa kiongozi wa serikali aliyekuwa
anatafuta cheo kwa nguvu zote! Sasa hivi ni serikali hiyohiyo inayopiga ramli
kumtafuta mchawi anayeiroga elimu hapa nchini!
Nimalizie
kwa kusema kwamba hatupaswi kumtafuta mchawi katika kashfa hii iliyoikumba nchi
upande wa elimu. Maana haya ndiyo matokeo ya kutaka kuvuna mahali ambapo
hatujapanda kitu. Kama tunaona raha ya mavuno mazuri ni lazima tujitahidi
katika upandaji, vinginevyo tuyakubali matokeo jinsi yalivyo pasipo kukamatana
uchawi.
0784 989 512