Bukobawadau

SHUGHULI YA NDOA YA MZEE MANGULA NI KESHO


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Phillip Mangula anatarajia kufunga ndoa kesho katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini, mjini Njombe.

Mzee Mangula anafunga ndoa na Mkuu wa Sekondari ya Philip Mangula, iliyopo wilayani Wanging’ombe, mkoani Njombe, Yolanda Kaberege.


Hatua hiyo ya Mzee Mangula kuoa inakuja baada ya aliyekuwa mke wake kufariki dunia mwaka 2004, kutokana na ugonjwa wa saratani.

Msemaji wa familia ya Mzee Mangula ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) tawi la Njombe, Dk Lechion Kilimike alilieleza Mwananchi kuwa ndoa hiyo itaongozwa na Askofu Mstaafu wa Kanisa hilo, Solomon Swalo.

Dk Kilimike alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye anatarajia kuwasili kesho mkoani hapa akitokea Mbeya ambako atatua leo saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Songwe.

Waziri Mkuu Pinda anatarajiwa kufuatana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali walioalikwa kwenye sherehe hiyo.

Habari zinaeleza kuwa, baada ya kumalizika kwa ndoa hiyo itakayofungwa saa 3:00 asubuhi, Pinda ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, atakwenda Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti linaloanza Aprili 9

Na Shaban Lupimo na Brandy Nelson | Mwananchi | Aprili 5, 2013
Next Post Previous Post
Bukobawadau