Ukaribisho Maalum wa Prof. Mama Anna Tibaijuka Ndani ya JamiiForums!
Ndugu WanaJF,
Kwa niaba ya uongozi wa JF,
napenda kutumia fursa hii kumkaribisha rasmi Mh. Mama Prof. @Anna Tibaijuka
hapa jamvini. Tuna imani wasomaji wa JF wanamfahamu Prof. @Anna Tibaijuka,
ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu (NEC) na Kamati Kuu ya CCM, Mbunge wa Muleba
Kusini, Waziri wa Ardhi na Makazi, Mwanamama wa Kwanza Kuongoza Kurugenzi ya
UNHABITAT, mwanzilishi wa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) na mengine
mengi!
Mama Tibaijuka,
Jamiiforums.com ambapo watu
huthubutu kusema kwa uwazi; Ndipo mahala pekee Jamii zote zinapokutana. Karibu
ukutane na Jamii!
Wana JF,
Mgeni wetu anajiunga kujumuhika
na Watanzania akipitia dirisha la Wanachama waliohakikiwa na kuthibitishwa
(Verified Members) kutumia majina halisi. Katika kundi hili tayari tunao
Watanzania wa kawaida, Watu maarufu na Wanasiasa mashuhuri ambao miongoni mwao
ni @Dr F. Ndugulile, @Halima Mdee, @HKigwangalla, @Freeman A. Mbowe, @John
Mnyika, @Mohammed Dewji, @Nape Nnauye, @Omari R Nundu, @Peter Msigwa, @Salome
Sijaona, @Charles Kenyela, @Dr.W.Slaa, @Jerry Silaa, @Kitila Mkumbo, @Mwigulu
Nchemba, @Rachel Mashishanga, n.k
Kujiunga rasmi kwa Mama Tibaijuka
kwetu ni ishara njema kuwa na wengine walio katika utumishi wa umma na wenye
hadhi ya juu katika Taifa letu sasa watazidi kushawishika kufuata nyayo.
Uongozi wa JamiiForums unaotekeleza misingi ya usawa kwa wanachama wote,
unawahakikishia ushirikiano. Pia tunazidi kuwakaribisha na kuwashauri viongozi
wa Kisiasa, Serikali na Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma wanaotembelea mtandao
huu au wanaojadiliwa na wanachama wa mtandao huu, kujiunga kwa utaratibu wa
majina halisi yaliyothibitishwa. Nyongeza ya hapo, tunawashauri kuchangia au
kutoa majibu yaliyo ndani ya mamlaka yao katika mada/hoja zinazogusa nafasi zao.
Uzoefu hapa nchini na kwingineko
duniani umebainisha kuwa Jamii ya wasomaji wa habari mara nyingi hubaki katika
mtanziko (dilemma) juu ya taarifa au habari zitolewazo katika mitandao mpaka
pale zinapothibitishwa na wahusika wenye mamlaka. Na katika mitandao mingine
ukiachilia JamiiForums, mara nyingi tuhuma/taarifa hasi/kashfa zilizojengeka
juu ya hisia zimekuwa zikisambaa kwa kasi zaidi na kujenga sura ya kuonekana
kuwa ndiyo ukweli. Hivyo kujitenga na mitandao ya kijamii au kushiriki kwa
majina yasiyo halisi ni mbinu aghali katika kukabiliana na tuhuma/taarifa
hasi/kashfa. Mwisho wake husababisha gharama kubwa isiyo ya msingi katika
kusafisha jina la mhusika au Taasisi. Ni falsafa isiyoyumba kwamba; giza
huondolewa na nuru na vivyo hivyo uongo hudhihirishwa kwa kuletwa ukweli. Pamoja
na jitihada yetu kubwa kuhakikisha kwa kila namna kuwa haki za
wahusika/waathirika zinazingatiwa na wanachama katika kuhabarishana ndani ya
Jamiiforums.com, bado suala la kuthibitisha au kukanusha linabaki kuwa ni la
wahusika/waathirika (mtu au Taasisi) wanaojadiliwa ndani ya habari.
Ni furaha yetu kubwa kwamba
wanachama wote wa JamiiForums na wote wanaotembelea mtandao huu wanafahamu
sheria za JF na wanaijua vema dhana ya “User-Content-Generated-Website”. Hiyo
ndiyo dhana itumikayo katika upashanaji habari hapa JF. Ni vema kusisitiza
kwamba, yanayoandikwa katika JamiiForums ni maoni ya watumiaji wa mtandao huu
na Uongozi wa JF una jukumu la kuzingatia kuwa maoni hayo yanazingatia Sheria tulizojiwekea.
Mama Tibaijuka amejiunga rasmi
wakati ambapo Wana-JF na Watanzania kwa ujumla wana maswali mengi sana juu ya
uporwaji wa ardhi na hatma ya migogoro ya viwanja na mashamba nchini. Ili
kukidhi kiu hii tunafikiria kuandaa na kumualika Mama Tibaijuka katika Mjadala
wa Ardhi. Tunaamini atatupa ushirikiano na pia Wana-JF mtaonyesha ushirikiano
kama ilivyo ada yetu.
Mwisho, tunapenda kumtakia Mama @Anna
Tibaijuka na Wanachama wetu wote ushiriki kamilifu unaozingatia Sheria na
Taratibu tulizojiwekea katika kuanzisha, kuendeleza na kuchangia mijadala.
Hatuna shaka kabisa na uvumilivu mkubwa wa Mama Tibaijuka katika kukabiliana na
changamoto ya mijadala na hoja za aina na uzito wowote kutoka kwa Wana JF.
JamiiForums!