Bukobawadau

Unachotakiwa kufahamu kuhusu ndoa kisheria

Kutokana na sheria ya ndoa ya Mwaka 1971, ndoa inatafsiriwa kuwa ni muungano wa hiari baina ya mwanaume na mwanamke, muungano unaokusudiwa kudumu kwa muda wote wa maisha yao.
Kutokana na tafsiri hiyo kuna mambo makuu matatu yanayotiliwa mkazo na tafsiri hiyo. Kwanza muungano huo lazima uwe wa hiari yaani usitokane na kushurutishwa ama na mzazi au mtu yeyote yule.
Ikiwa wawili hao watakuwa wamelazimishwa kufunga ndoa, basi ndoa hiyo haitakuwa ndoa kwa mujibu wa tafsiri ya ndoa katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Wapo ambao wakati mwingine unaweza kuona kwa mfano mzazi au mlezi anamlazimisha kuoana na fulani kwa sababu zake, ndoa kama hiyo kisheria sio haki na mwenye kulazimishwa anaweza kuamua akipenda kuachana na aina hiyo ya ndoa. Jambo la msingi ni kuhakikisha anayelalamika anakuwa ana ushahidi kwa kile ambacho analalamikia, kwa mfano anaweza kueleza namna alivyolazimishwa.
Ni kweli inawezekana fulani anafaa kuwa na mwanao, kisheria inashauriwa kutomlazimisha, badala yake lililo la msingi ni kushauri, kisha mtu mwenyewe aamue.
Pili ndoa lazima iwe muungano wa watu wawili na ni lazima watu hao wawe wa jinsia mbili tofauti yaani mwanaume na mwanamke. Kwa maana hiyo ndoa ya watu wa jinsia moja yaani mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke haitambuliki katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Siku hizi kuna watu wameanza kuja na mambo ya ndoa za jinsia moja, hizo ni aina ya ndoa ambazo kwa mujibu wa sheria za Tanzania hazikubaliki.
Tatu ni uhusiano huo uwe wenye kukusudiwa kudumu kwa muda wote. Lengo la kufunga ndoa ni ndoa hiyo idumu kwa kwa kipindi chote cha maisha ya wanandoa. Ndio kusema kwamba hakuna ndoa za mikataba, ya kusema labda mtaishi kwa muda fulani, kwa mfano mwaka mmoja.
Ndoa inayofungwa ikiwa na lengo ya kuvunjwa baada ya kipindi fulani si ndoa halali kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Ndoa itavunjwa ikiwa kutabainika/kutajitokeza mambo yanayoweza kupelekea ndoa kuvunjika kama inavyobainishwa kwenye sheria ya ndoa na si vinginevyo.
Kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakikaa tu bila kuangalia namna gani wanaweza kuzingatia sheria za ndoa.Kwa mfano wapo watu ambao wamekuwa wakiishi tu, huku wao wakifikiri kwamba kuishi kwao kunatosha kuifanya ifahamike kama ndoa.
Kisheria ni kwamba kuna taratibu zake za kuzingatiwa ili watu wafahamike kama wanandoa.Kukubali kuishi tu bila kuzingatia taratibu za kisheria kunaondoa maana halisi ya ndoa hasa kwa mfano watu wenyewe wanapokuwa hawako tayari kuzifuata taratibu hizo.
 Aina Za Ndoa
Kutokana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ndoa zimemegawanyika katika aina mbili ambazo ndoa ya mke mmoja ambapo huhusisha mume mmoja na mke mmoja.

 Aina ya pili ni ndoa ya wake wengi ambayo mume mmoja anakuwa na wake zaidi ya mmoja, waweza kuwa wawili ama zaidi kulingana na vile ambayo wahusika wenyewe wataona inafaa au kulingana na imani zao za dini, hata hivyo ni lazima kuwepo na makubaliano.
Next Post Previous Post
Bukobawadau