Gazeti la mwananchi limeandika Kifaa chanjo ya Ukimwi chagundulika
Dk. Rashid pichani
Dar es Salaam. Wanasayansi nchini Marekani wamebaini kifaa kipya kitakachoharakisha upatikanaji wa chanjo ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Taarifa kwa Mwananchi Jumapili iliyotolewa
Alhamisi wiki hii na Taasisi ya Tafiti Kukabiliana na Magonjwa ya Mzio
na Kuambukiza (NIAID) ya nchini Marekani ilieleza kuwa mfumo wa kifaa
hicho siyo tu utasaidia kurahisisha chanjo kukabiliana na VVU, bali hata
kwa magonjwa mengine yanayosababishwa na virusi kama mafua na yale
yanayosababisha uvimbe wa ini.
“Ni mfumo wa hali ya juu wenye uwezo wa haraka wa
kuchambua chembechembe kinga zenye uwezo wa kuangamiza aina mbalimbali
za VVU zinazopatikana duniani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliyoambatanisha majina ya
wanasayansi nguli wa NIAID ambao wamethibitisha kifaa hicho chenye mfumo
mpya katika teknolojia ya kuchambua VVU, umeweka wazi kuwa matatizo
waliyokuwa wakipata wanasayansi katika kudhibiti virusi sasa imepata
ufumbuzi.
Uzuri wa kifaa hicho unaelezwa kwamba ni kuweza
kuchambua na kutofautisha chembe kinga za aina mbalimbali, hata kujua
idadi na uwezo wake katika kushambulia adui katika mwili wa binadamu.
“Uchambuzi wa kifaa hiki unaweza kutumika
kuchunguza namna mwili wa binadamu unavyoweza kukabili maradhi mengine
yanayosababishwa na virusi kama vile mafua na uvimbe wa ini,” anaeleza
sehemu ya taarifa hiyo.
Wanasayansi nguli wa NIAID waliothibitisha uwezo
wa kifaa hicho ni Mtaalamu wa Dawa na Mifumo ya Kibiolojia, ambaye pia
ni Mkuu wa Idara ya Chanjo, Profesa Peter Kwong na Mkuu wa Idara ya
Kinga, Profesa John Mascola.
Wataalamu hao wanaeleza kuwa kifaa hicho kina
uwezo wa kutofautisha ni chembechembe gani za kinga zenye uwezo wa juu
katika kukabili virusi vya maradhi.
Kupitia njia hiyo, inaelezwa kuwa ni rahisi
kubaini chanjo yenye nguvu, hivyo kuharakisha upatikanaji wa chanjo
itakayothibitishwa kukabiliana na VVU.
Kulingana na teknolojia na tafiti mbalimbali, VVU
bado hajaipata tiba au chanjo madhubuti, ingawa wameweza kupata dawa
zenye uwezo mkubwa wa kupunguza makali ya virusi hivyo (ARVs).
Hadi sasa tafiti mbalimbali zimeonyesha uwezekano wa kupatikana tiba na chanjo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kwa sasa tafiti nyingi zipo kwenye majaribio,
NIAID inaeleza kuwa kupatikana kwa kifaa hicho kutaharakisha kazi ya
kuchanganua uwezo wa chanjo hizo katika kukabiliana na VVU.