HAYAWIHAYAWI, SASA YAMEKUWA! USIKU WA HIP HOP, THE VODACOM MIC KING KURINDIMA J’MOSI HII DAR LIVE
Wakali tisa wa Hip Hop wanaowania gari aina ya Toyota FunCargo (new model), katika pozi mbele ya gari lao.
Na Mwandishi Wetu
ILIPANGWA, ikapangika. Baada ya kusubiririwa kwa muda mrefu, hatimaye msimu mpya wa shoo ya Usiku wa Hip Hop (2013) unachukuwa nafasi Jumamosi hii ndani ya Ukumbi wa Dar live, Mbagala-Zakhem, jijini Dar.
Wasanii wanaotamba kwenye gemu la Hip Hop, Kala Jeremiah, Fid Q, Nay wa Mitego, Joh Makini, Stamina na wengine kibao pamoja na washiriki wa Shindano la The Vodacom Mic King watakamua shoo baab’kubwa kuweka historia mpya ya burudani.
Meneja Matukio wa Ukumbi wa Dar Live, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ amewahakikishia mashabiki wote wa muziki wa Hip Hop kuwa Jumamosi kutasheheni matukio kibao, ulinzi mzito utakuwepo pamoja na parking kubwa ya magari hivyo watu wafike kwa wingi watainjoi kwa nafasi na kuondoka salama ukumbini.
“Vijana tisa waliosalia katika Shindano la The Vodacom Mic King watapanda jukwaani na kushusha mistari ambapo mshiriki mmoja anatarajiwa kuondoka na gari jipya aina ya Toyota FunCargo (new model),” alisema Abby Cool na kuongeza:
“Mashabiki wanaweza kulifuatilia shindano hilo kupitia Runinga ya DTV kuweza kujua jinsi ya kuwapigia kura.”
Washiriki hao na namba zao za ushiriki kwenye mabano ni Ally (MK 02), Anold (MK 03), Bahati (MK 05), Boniface (MK 07), Emmanuel (MK 10), Ibrahim (MK 12), Karrys (MK 13), Lusajo (MK 14) na Martin (MK15). Jinsi ya kuwapigia kura, wasomaji wanatakiwa kuandika neno MK wakiambatanisha na namba ya mshiriki kisha kutuma ujumbe huo kwenda namba 15564.
OFA ZAIDI KWA MSHINDI
Mbali na mshindi kuondoka na gari, Mrisho aliongeza kuwa washindi watatu wa nafasi za juu watajipatia dili la kurekodi singo mojamoja kutoka kwa prodyuza kiwango aliyezalisha ngoma kali Bongo ikiwemo ya Kundi la Kigoma All Stars iitwayo Leka Dutigite, Tudd Thomas.
TUZO KUTOLEWA
Mrisho alitiririka na mistari kuwa, mbali na shoo kali kutoka kwa wakali hao wa Hip Hop, kutakuwa na kipengele cha kutoa tuzo za muziki wa Hip Hop katika vipengele tofauti hivyo mashabiki pia waendelee kuwapigia kura wasanii wanaowapenda.
Vipengele vitakavyotolewa tuzo ni Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Legendary) ambapo yamepita majina matatu; Fid Q, Joh Makini na Profesa Jay. Pia kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Chipukizi) ambacho kina majina kama Young Killer, P The Mc na Tabla huku akianisha kipengele cha mwisho ambacho ni Wimbo Bora wa Hip Hop (2012/13) chenye nyimbo kali za Dear God (Kala Jeremiah), Sihitaji Marafiki (Fid Q) na Najuta Kubalehe (Stamina).
“Ili kuwapigia kura, mashabiki wanatakiwa kuandika neno BHL wakiambatanisha na jina la msanii husika kwenda namba 15564 katika kipengele cha Msanii Bora wa Hip Hop (Legendary).
“Kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Chipukizi), mashabiki waandike neno BUA na kufuatiwa na jina la msanii wanayempenda kwenda namba 15564,” alisema Abby Cool na kuongeza:
“Kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka, mashabiki waandike neno BHS likifuatiwa na jina la msanii wanayempenda kisha watume ujumbe huo kwenda namba 15564.”
KUWAENZI WASANII/SOKA KWENYE SKRINI KUBWA
Abby Cool aliweka bayana kuwa katika shoo hiyo kutakuwepo na documentary maalumu ya kuwakumbuka wasanii wa Hip Hop waliotangulia mbele za haki kupitia skrini kubwa bila kusahau mashabiki wa soka watapata fursa ya kushuhudia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) kati ya Bayern Munich na Borrusia Dortmund. Twendeni Dar Live J’mosi!