HISTORIA YA WATU WA MKOA WA KAGERA – ORIGINAL ZAO
HISTORIA MKOA KAGERA – KUITWA KAGERA Mkoa huu
haukuitwa Kagera bali ulikuwa moja ya maeneo yaliounda jimbo lililoitwa
Lake Province. Jimbo hili lilijumuisha Wilaya ya Bukoba, Musoma,
Shinyanga na Tabora. Baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa
‘West Lake Region’ (Ziwa Magharibi) na kujumuisha Wilaya 4 za Ngara,
Biharamuro, Karagwe na Bukoba. Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni mkoa
wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika
himaya 8. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi),
Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku
(Bukara). Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo ni pamoja na Emmanuel
Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe), Kasusura (Biharamulo),
Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayoza (Bugabo), Kahigi (Kihanja)
na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa na walinzi wake walioitwa
Warugaruga.Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wana asili
ya Bunyoro. Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro
na Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu
na Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine
Bantu) na yanafanana mila na desturi. Makundi hayo yaligawanyika kati ya
wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao
walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa. Bahima (Balangira) walikuwa na
koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango.
Bairu walikuwa na Koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa
Bairu lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi
walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware). Kila ukoo uliitwa jina la
Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa
kula (Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).Mkoa
ulibadilishwa jina na kuitwa Kagera mwaka 1979 baada ya vita ya Tanzania
na Uganda. Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo wakati huo
Capt. Peter Kafanabo jina la Kagera lilipendekezwa kwa sababu ya mto
Kagera unaogusa sehemu kubwa ya Wilaya zote zinazounda Mkoa wa Kagera.