Bukobawadau

Kifo cha Mutula Kilonzo na maswali kibao

Nairobi. Serikali ya Jubilee ina mengi ya kutatua mwezi mmoja tu tangu iingie madarakani.
Wiki jana, mwanasiasa maarufu, Mutula Kilonzoalikutwa akiwa amefariki dunia nyumbani kwake, Maanzoni, Machakos.
Wabunge nao wamekuwa wakilia wakitaka nyongeza za mshahara la sivyo watatatiza shughuli za Serikali bungeni! Watoto wa chekechea na shule za msingi nao wanasubiri kupewa tarakilishi za mapajani (laptop) walizoahidiwa na Kenyatta na Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. Tusisahahu kwamba hii ni Serikali ya ugatuzi (kutawanya Amadaraka) na kuna shida chungu nzima kuhusu ofisi na idara kadhaa wa kadhaa zilizomo katika Serikali Kuu na za kaunti zote 47 zilizobuniwa kulingana na Katiba iliyozinduliwa Agosti 2010.
Kuna kutoaminiana kati ya magavana na makamishna wa kaunti hizo huku kila mmoja akitaka kuwa mkubwa wa mwingine hali ambayo imeleta kizungumkuti katika ngazi za Serikali zote mbili.
Nani ni mkubwa kati ya gavana aliyechaguliwa rasmi na wananchi na kamishna aliyeteuliwa na Serikali Kuu? Hapa kuna kitendawili na atakayekitegua atakuwa ameokoa wengi wasije wakaugua maradhi ya moyo kwa kukosa amani.
Kuzaliwa ni kwa bahati lakini kufa ni lazima kwa kiumbe yeyote yule, lakini vifo vingine huzua maswali mengi kuliko majibu, hasa vikitokea ghafla.
Wiki jana, kifo cha Mutula kilishtua wengi nchini Kenya kwa kuwa kilipokonya nchi kiongozi aliyeenziwa na wengi.
Mutula ni kiongozi aliyezungumza bila kuogopa yeyote hata walio mamlakani. Kwa hivyo, alipofariki ghafla kitandani mwake Aprili 27, wingu jeusi kilitanda nchini na maswali mengi yasiyo na majibu yakaanza kutiririka.
Wanasiasa wa Jubilee na wa Muungano wa Cord waliunganishwa na kifo cha Mutula na wengi wao wameweka kando tofauti zao na kutembelea mjane wake, Nduku Kilonzo kumpa rambirambi zao.
Kenyatta hakuachwa nyuma. Alienda kutoa pole zake kwa familia ya Mutula, Alhamisi.
Ingawa si nadra kwa wanasiasa maarufu kufariki ghafla au kupatikana wakiwa wamefariki katika hali ya kutatanisha, hiyo pekee haijazuia Wakenya kutoa dhana mbalimbali kuhusiana na kifo hicho.
Wengi, haswa katika mitandao ya ‘Facebook’ na ‘Twitter’ wanaweza kuapa kwamba Mutula aliuawa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kinywaji kwa sababu za kisiasa.
Madaktari waliohusika na uchunguzi walidai kuwa pengine alipewa sumu ama alikunywa mwenyewe sumu hiyo ili kujitoa uhai. Dhana nyingine ni kwamba alipatwa na mshutuko wa moyo ama aliuawa na mchanganyiko wa dawa alizokuwa pengine anazitumia kutibu maradhi fulani.
Kwa hakika, hakuna anayejua kiini cha kifo chake kwa kuwa matokeo ya uchunguzi wa mabaki ya mwili wake hayajakamilika na Wakenya watasubiri kwa wiki nane ili wajue sababu ya kifo hicho cha kusikitisha.
Mutula alifariki wiki chache baada ya kumdokezea mwanahabari mmoja wa gazeti la kila siku la Standard kwamba alikuwa na habari ambayo kama ingechapishwa, ingetetemesha nchi nzima kutokana na uzito wake.
Habari hiyo ambayo sasa Mutula ameenda nayo kaburini ilikuwa inahusu nini na nani katika ulingo wa kisiasa? Mbona hakuwa tayari kutoboa siri hiyo? Awali marehemu mwanasiasa huyo aliyekuwa amechaguliwa tu mwezi mmoja uliopita kama Seneta wa kwanza wa Machakos alikuwa ameelezea kuhofia maisha yake lakini aliendelea kutembea bila ulinzi wowote na hata kujiendesha mwenyewe.
Mnamo Ijumaa, Aprili 26, Mutula aliyekuwa Waziri wa Haki na baadaye wa Elimu kabla ya kuchaguliwa Machi 4 kama Seneta wa kwanza wa Machakos, alikuwa ameenda kufanya mazoezi ya kila asubuhi katika hoteli ya kifahari ya Hilton saa 12:00 asubuhi na baadaye akaondoka Nairobi kuelekea shambani kwake barabara ya Mombasa ambapo aliwasili saa nane mchana kisha akatembea kwenye shamba hilo lenye ekari 1,500 kuangalia wanyama wake wa pori kama vile simba.
Next Post Previous Post
Bukobawadau