Magufuli amkana Sitta, asema hana ubia naye urais 2015
Dodoma. Siku chache baada ya Waziri wa Afrika Mashariki Samuel
Sitta kumhusisha Dk John Magufuli na kundi la urais la mwaka 2015,
Waziri huyo wa Ujenzi, ameibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza
hafikirii kuwania nafasi hiyo.
Waziri Sitta alinukuliwa na gazeti hili juzi
akieleza kuwa wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli
na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao
watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Alisema
hayo juzi kwenye Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la
wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine
(SAUT), Mwanza.
Kabla ya hapo alikuwa amewataja rafiki zake hao
wakati wa hafla ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia
ya Igoma, Mwanza, Jumapili iliyopita.
Alisema hatagombea tena ubunge mwaka 2015, baada
ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia
namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania
urais ambao alieleza anamwachia Mungu.
“Kwa ubunge nimekwishawaeleza inatosha, sitagombea
tena kwani miaka 35 inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi
kujua lakini nina afya nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya
nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,”
alisema Sitta.
Kauli ya Magufuli
Akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa Bunge
jana, Dk Magufuli alisema haelewi msingi wa kauli ya waziri mwenzake
huyo, kwani hajui chochote katika mtandao wa urais alioutaja.
Magufuli alisisitiza kusema hana kundi, hakuwahi
kuzungumza wala kuhudhuria vikao vya kundi lolote, na kwamba kundi lake
ni CCM na Mwenyekiti wake ni Jakaya Kikwete.
“Sina kundi. Sijawahi kuwa na kundi na sitarajii
kuwa na kundi lolote. Ninachojua kundi langu ni CCM na kiongozi wake ni
mwenyekiti wake, Rais Kikwete,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, Dk Magufuli pia alipuuza taarifa kuwa
alichangia harambee hiyo akisema, “Si kweli, Mwanza sijatoa hata senti
na hata siku ilipofanyika hafla hiyo, nilikuwa Dar es Salaam katika
mkutano na makandarasi.” Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara wa
urais 2015, Magufuli alieleza kuwa hakuwahi kuzungumza na Sitta suala
hilo linalohusu makundi ya urais mwaka 2015.
Sitta azungumza
Akizungumza na gazeti hili baadaye jana, Sitta
alikiri kuwa hawakuwahi kuzungumzia suala la kuwania urais isipokuwa ni
hisia zinazojengwa na kuwa majina yanatajwa kuwa wanautaka urais.