Bukobawadau

MAKALA YA KITILA MKUMBO;Lini Serikali ilijua kwamba matokeo ya 2012 yalikosewa?

UENDDESHAJI wa sekta ya elimu nchini hauishi vituko. Kituko cha hivi karibuni kabisa ni uamuzi wa Serikali kufuta matokeo ya kidato cha nne na kuliamuru Baraza la Mitihani liyaendae upya.
Niwakumbushe wasomaji kwamba hiki si kituko cha kwanza na cha mwisho katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Miaka ya 1980 tuliwahi kutumia watu waliohitimu darasa la saba kuwa walimu, maarufu kama walimu wa UPE. Baadaye tukaamua kujenga shule za sekondari katika kila kata bila maandalizi yeyote ya maana. Matokeo yake kila kitu kikawa hakitoshi, isipokuwa majengo yaliyojengwa chapuchapu na bila usimamizi wa kihandisi.
Tulipoona walimu hawatatoshi kukidhi mahitaji ya shule zilizoongezeka sana, tukaibuka na walimu wa voda fasta, tukichukua vijana waliomaliza kidato cha sita  na'kuwafundisha’ ualimu chapuchapu.
Sasa hili la kufuta matokeo linahitaji mjadala kama tulivyojadili mambo mengine huko nyuma. Tunajua mijadala haisaidii kwa Serikali hii lakini ni vizuri wengine tukasema ili isijeonekana wote tumeridhika na hatua hii ya Serikali au kwamba maamuzi ya Serikali yapo sawa. Ukweli ni kwamba uamuzi wa kufuta matokeo ya kidato cha 2012 haujakaa sawa kama nitakavyoonesha katika makala haya.
Katika kuhalalisha uamuzi wake wa kufuta matokeo ya kidato cha nne 2012, Serikali inasema kwamba Baraza la Mitihani la Tanzania lilitumia viwango vipya vya ufaulu bila kuwashirikisha na kuwaandaa walimu na wanafunzi, na kwamba kiwango kipya hakikutenda haki kwa walimu na wanafunzi waliofanya juhudi kubwa katika mazingira ya elimu ya sasa.
Swali la kwanza la kujiuliza ni je, tangu lini Baraza la Mitihani linawahusisha wanafunzi na walimu katika kupanga viwango vya ufaulu? Ukweli ni kwamba maamuzi ya Baraza la Mitihani siku zote hufanywa na vikao mbalimbali vya Baraza lenyewe, ambapo wadau mbalimbali ni wajumbe, ikiwamo Serikali yenyewe na kwa pande zote za Muungano! Shule, walimu na wanafunzi hupokea taarifa tu kuhusu maamuzi ya Baraza.
Swali la pili la kujiuliza ni je, Serikali ilijua lini kwamba matokeo haya yalipangwa kwa viwango vipya vya ufaulu? Kama nilivyosema hapo juu, Serikali ni mjumbe kamili wa Baraza la Mitihani Tanzania, ikiwakilishwa na Makamishna wa Elimu wa Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na taasisi nyingine za elimu nchini. Kwa hiyo ni wazi kwamba Serikali ilijua na kuridhia matumizi mapya ya viwango vya ufaulu kabla ya kuanza kutumika, na wala hapakuwa na haja ya kuunda tume kujua jambo hili.
Kwa kawaida, kabla matokeo hayajatangazwa siku zote hufanyika uhakiki na kufanya marekebisho muhimu, ikiwamo kufanya uwiano (standardisation). Sasa swali la kujiuliza ni lini Serikali ilijua kwamba matokeo ya kidato cha 2012 yalikuwa mabaya kwa kiwango tulichokiona? Je, ni kweli kwamba Serikali ilikuwa haijaona matokeo haya hadi Waziri Dk. Shukuru Kawambwa anayatangaza?
Mantiki hapa inatuambia kwamba Serikali ilikuwa inayajua matokeo kabla ya kutangazwa na kuridhia kwamba yatangazwe.  Kuamini vinginevyo ni kujidanganya. Kwa mantiki hii ni wazi kwamba Serikali ilishituka baada ya watu mbalimbali kupaza sauti kubwa wakiyazomea matokeo yale kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea.
Ndiyo kusema kwamba Serikali iliwajibika kuunda tume kwa sababu ya shinikizo la umma na ilikuwa haijajiandaa katika hili kwa kuamini kwamba tutalalamika na kisha litapita kama ilivyo ada ya sisi Watanzania.
Tukiangalia maudhui yenyewe ya sababu za Serikali za kufuta matokeo utakuta kwamba hapakuwa na sababu za kuunda tume. Kiwango kipya cha ufaulu kinacholalamikiwa na Serikali kupitia katika taarifa iliyowasilishwa na William Lukuvi ni jambo ambalo limekuwa likijadiliwa na wadau wa elimu kwa muda mrefu.
Tulikuwa tunalalamikiwa sana katika ukanda wa Bara la Afrika kwamba viwango vyetu vya ufaulu vipo chini sana, na hili limekuwa likisababisha vijana wetu wanaoenda kusoma nchi mbalimbali kupata taabu katika kukubalika moja kwa moja.
Kwa mfano, kiwango cha chini cha ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne katika nchi nyingi za Kiafrika ni 40. Ndiyo kusema yeyote anayepata chini ya alama hii katika somo lolote inamaanisha amefeli somo husika. Nchi hizi ni pamoja na Ethiopia, Sudan, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Gambia, Liberia, Sierra Leone na Uganda.
Kwa hiyo utaona kwamba ni sisi peke yetu katika ukanda huu wa Afrika ambao tulikuwa tunatumia kiwango cha ufaulu cha alama 21, ambacho kwa kweli ni kidogo mno na ni udanganyifu ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika tunazofanana nazo.
Nieleze pia hapa kwamba hiki kiwango kipya kinacholalamikiwa kimeshajaribiwa kwa kuangalia matokeo ya 2010 na 2011 yangekuwaje kama Baraza lingetumia viwango hivi vipya. Katika mithani hii ilionekana tofauti ndogo sana katika ufaulu katika kutumia kiwango kipya na cha zamani.
Kwa mfano, tofauti katika mitihani ya mwaka 2010 ilikuwa 1.24 na asilimia 0.5 kwa mitihani ya 2011. Ndiyo kusema wazazi na wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha nne 2012 wasichekelee sana kwa sababu uwezekano ni mdogo kwamba kutakuwa na tofauti  kubwa kati ya matokeo yaliyofutwa na yale yatakayokokotolewa upya.
Serikali inaposema kwamba Baraza litumie viwango vya ufaulu vya mwaka 2011 ni kana kwamba matokeo ya mwaka huu yalikuwa bora. Nikumbushe kwamba matokeo ya mwaka 2011 yalikuwa mabaya vilevile na hayana tofauti kubwa na matokeo yaliyofutwa.
Hii ni  kwa sababu asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2011 walipata madaraja ya IV na sifuri ukilinganisha na asilimia 93.6 waliopata madaraja haya katika matokeo yaliyofutwa ya mwaka 2012.
Niikuikumbushe Serikali kwamba Baraza la Mitihani lilibadilisha pia viwango vya ufaulu kwa Kidato cha Sita ambapo sasa kiwango cha chini cha ufaulu ni 40-44. Ni vizuri sasa serikali isisubiri matokeo yatoke ndipo ishtuke. Nashauri Serikali iwaamuru Baraza la Mitihani watumie kiwango cha zamani cha ufaulu ili kuepuka usumbufu kama ulivyojitokeza kwa matokeo ya kidato cha nne ya 2012.
Nimalizie kwa kuwaasa Watanzania wenzangu na Serikali yetu kwamba matatizo yetu ya elimu hayawezi kutatatuliwa kwa kutumia viwango vya chini vya ufaulu ambavyo haviendani na viwango katika nchi nyingine za Kiafrika na dunia kwa ujumla. Tuache kufanya mambo rahisi kwa kujifurahisha muda mfupi na kutengeneza maumivu kwa muda mrefu ujao. Sababu za wanafunzi kufeli zimeanishwa katika tafiti mbalimbali na Serikali inajua, lakini haijachukua hatua za maana kwa sababu tumezoea kufanya mambo kukidhi haja ya leo. 
Kufuta matokeo na kuyapanga upya hakutatua matatizo ya msingi yanayoikabili elimu yetu. Suluhisho ni kuwa na mipango endelevu katika kuwekeza kwa walimu na miundo mbinu ya ufundishaji na kujifunza.
Next Post Previous Post
Bukobawadau